Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Urusi yaongeza mashambulizi dhidi ya wakosoaji wake nje ya nchi
- Author, Will Vernon
- Nafasi, BBC News
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Maafisa wawili wa polisi ambao hawakuwa wamevalia sare rasmi walikuwa wakimsubiri Dmitry Gudkov katika Uwanja wa Ndege wa Luton wa London majira ya joto yaliyopita. Mwanasiasa huyo wa upinzani wa Urusi, ambaye anaishi uhamishoni katika nchi ya Umoja wa Ulaya, alikuwa akisafiri kuelekea Uingereza kuhudhuria siku ya kuzaliwa ya rafiki yake.
"Waliku hapo ili kunizuia punde tu nitakapoondoka kwenye ndege," Dmitry anasema. "Hilo halijawahi kunitokea hapo awali."
Lakini polisi hawakuwa na nia ya kumkamata - bali walitaka kumuonya.
"Waliniambia niko kwenye orodha ya watu ambao wako hatarini. Waliniuliza nitakaa wapi na nitatumia simu gani.”
Dmitry Gudkov ndiye mwanzilishi mwenza wa Kamati ya Kupambana na Vita, shirika linaloratibu juhudi za kupinga vita nchini Ukraine. Anatafutwa nchini Urusi kwa "kueneza uwongo" kuhusu jeshi la Urusi.
Kuanza kwa uvamizi kamili wa Urusi nchini Ukraine mnamo 2022 kulisababisha ukandamizaji mkubwa dhidi ya wapinzani ndani ya Urusi. Takriban wanaharakati wote na waandishi wa habari wa kujitegemea walikimbia nchi.
Sasa, wakosoaji kadhaa wa Kremlin wanaoishi Ulaya wameiambia BBC kwamba Urusi inaongeza juhudi zake za kuwanyamazisha, kuwatishia na kuwatesa wapinzani nje ya nchi. Baadhi yao wanahofia kuasimulia yale yanayowakabili hadharani. Ubalozi wa Urusi huko London haukujibu ombi la kupata maoni yake.
'Wanaweza kuwafikia watu karibu kila mahali'
Mchambuzi Mark Galeotti, anayesomea huduma za usalama za Urusi, anakubali kwamba msako dhidi ya "maadui" wa Urusi nje ya nchi unazidi kuongezeka. "Nadhani inaashiria kuongezeka kwa hofu ya Kremlin," anasema, "kwamba inahusiana na mapambano ya kisiasa."
Huku upinzani ukiwa umezimwa nyumbani, Urusi inaelekeza mawazo yake kwa wapinzani ambao wametafuta hifadhi katika nchi za Magharibi. Dmitry Medvedev, rais wa zamani wa Urusi ambaye sasa ni naibu mkuu wa Baraza la Usalama la Urusi, aliwataja kama "wasaliti ambao wamekimbilia kwa adui na kutaka Nchi yao ya iangamie".
Mwanaharakati mwingine dhidi ya Kremlin pia aliwasiliana na polisi wa Uingereza. "Walisema walihitaji kujadili usalama wangu na wa familia yangu," Ksenia Maximova aliiambia BBC.
Mwanzilishi wa Jumuiya ya Kidemokrasia ya Urusi huko London anasema polisi walimshauri asisafiri hadi nchi fulani ambapo maajenti wa Urusi wanafanya kazi kwa uhuru zaidi.
"[Kremlin] inaimarisha mapambano dhidi ya 'maadui', hiyo ni kweli kabisa," anasema, "wanabana pande zote."
Yeye na wanaharakati wenzake wamegundua ongezeko la mashambulizi ya mtandaoni na kujaribu kujipenyeza kwenye kikundi mtandaoni.
Katika taarifa kwa BBC, msemaji wa Polisi wa Kupambana na Ugaidi wa Uingereza alisema, "Tumekuwa tukiongeza rasilimali zilizopo kukabiliana na shughuli za mataifa yenye uadui.”
Mnamo Desemba, sheria mpya ya Uingereza ilianza kutekelezwa, na kuwapa polisi mamlaka zaidi ya kukabiliana na vitisho kutoka kwa mataifa yenye uhasama kama vile Urusi.
"Vimelea haviwezi kulala kwa amani ..." ilikuwa moja ya ujumbe ambao mwandishi mpekuzi Alesya Marokhovskaya alipokea mwaka jana.
Vitisho hivyo viliambatana na jina la mtaa wa Prague alikokuwa akiishi. "Nilihama nyumba ili kufanya iwe vigumu kwao," anasema Alesya.
"Tulidhani ni raia wa Czech na mfuasi wa Putin ambaye huenda amenitambua."
Lakini ujumbe huo mbaya uliendelea kuongezeka - ukimuita "mchafu" na kutishia kumpata "popote atakapomtembeza mbwa wake mkorofi".
Mbwa wa Alesya kweli hupenda kubweka anapotembea. Alitoa taarifa kwa polisi wa Czech.
Baadaye, Alesya alipaswa kusafiri hadi Uswidi kuhudhuria mkutano. Hapo ndipo alitumiwa ujimbe wa vitisho zaidi: maelezo ya safari yake ya ndege, nambari ya kiti na hoteli aliyokuwa anatarajia kukaa kwa muda atakaokuwa safarini. "Ilikuwa wazi walikuwa na uwezo wa hali ya juu wa kufikia hati zake," Alesya anasema. "Inaonekana kama mwenendo ya serikali ya Urusi."
Alesya alikuwa ametajwa kuwa 'wakala wa kigeni' miaka iliyopita na serikali ya Urusi, kutokana na kazi yake katika tovuti huru ya habari ya Urusi iStories.
"Nilipoondoka Urusi na kuja Prague, nilikuwa na hofu juu ya wangu usalama," Alesya asema. "Sasa ninatambua kwamba [huduma za kijasusi za Urusi] zinaweza kuwafikia watu kila mahali barani Ulaya. Siwezi kusema kwamba siogopi, kwa sababu ninaogopa."
Lakini kwa nini hii inatokea sasa? Wataalamu wanasema huduma za usalama za Urusi zimeanza kudhibiti shughuli nje ya nchi baada ya kipindi cha machafuko. Mamia ya wanadiplomasia wa Urusi wanaoaminika kuwa mawakala wa kijasusi wanaofanya kazi chini ya ulinzi wa kidiplomasia walifukuzwa kutoka nchi za Magharibi kufuatia uvamizi kamili wa Ukraine.
"Kulikuwa na kipindi cha machafuko baada ya 2022," anasema Andrei Soldatov, mwandishi wa habari wa Urusi ambaye anaangazia huduma za ujasusi. "Mnamo 2023, mashirika yalijipanga tena na kupata ushawishi. Walipata rasilimali na kuanza kuongeza shinikizo.
Mark Galeotti anasema mamlaka inazidi kuwageukia washirika kufanya kazi zao chafu - magenge ya wahalifu: "Ikiwa unataka mtu apigwe au hata kuuawa, ni rahisi sana kushiriki," anasema Bw Galeotti, ambaye amekuwa akiandika kuhusu uhusiano kati ya serikali ya Urusi na uhalifu uliopangwa kwa miaka kadhaa.
Serikali ya Poland inaamini hicho ndicho kilimkuta Leonid Volkov, mwanaharakati mashuhuri na mshirika wa marehemu Alexei Navalny. Alishambuliwa kikatili kwa nyundo nchini Lithuania miezi minne iliyopita, lakini akanusurika.
Waziri Mkuu wa Poland, Donald Tusk, alisema mwanamume mmoja raia wa Belarus anayefanya kazi katika idara ya ujasusi ya Urusi amewalipa wahuni wawili wa mpira wa miguu wa Poland kutekeleza shambulio hilo. Wote watatu wamekamatwa.
"Vitisho ndio dhamira," anasema Mark Galeotti. "Wazo la kuwataka watu wafya midomo yao. Ni mbinu inayotumiwa kuzuia kuibuka kwa aina fulani ya upinzani thabiti wa kisiasa [dhidi ya Kremlin].
Mamlaka ya Urusi pia hujaribu kufanya maisha ya kila siku kuwa magumu iwezekanavyo kwa wapinzani waliyo nje ya nchi.
Mwanaharakati Olesya Krivtsova, 21, alitoroka Urusi baada ya kukamatwa na kutishiwa kufungwa kwa machapisho ya kupinga vita kwenye mitandao ya kijamii. Sasa anaishi Norway, lakini hivi majuzi aligundua muta wa matumizi ya pasipoti yake ya Urusi umeisha kumaanisha kuwa hawezi kutuma ombi la hati za kusafiri.
"Nadhani hii ni [mbinu] mpya ya ukandamizaji," Olesya anasema. "Kila wakati wanafikiria tunawezaje kuwahangaisha zaidi, tunawezaje kuwashinikiza?"
Wanaharakati kadhaa wanaoishi nje ya nchi pia wamefutiwa pasi zao bila ya kupewa arifa. Wengi wana kesi za jinai zilizofunguliwa dhidi yao nchini Urusi - bila pasipoti halali, hawawezi kuajiri mawakili au kufanya malipo ya nyumbani. Njia pekee ya kutatua suala hilo ni kurudi Urusi.
Kwa Olesya, kurudi kungemaanisha kukamatwa na kufungwa. Sasa ametuma maombi ya kitambulisho cha muda cha Norway kama mkimbizi.
"Nchini Urusi, sasa nina haki moja tu - haki ya kwenda gerezani. Pasipoti yangu imefutwa. Hii inaonyesha kiwango cha ukatili wao,” anasema mwanaharakati huyo kijana.
"Tayari wameharibu kabisa maisha yangu na maisha ya familia yangu ... Hawatakoma kabisa."
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi