Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wanajeshi wa Ukraine wapo kilomita 30 ndani ya eneo la Urusi
Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema ilikabiliana na mapigano karibu na vijiji viwili, kati ya kilomita 25-30 ndani ya Urusi.
Muhtasari
- Ukraine inadhibiti vijiji 28 vya Kursk, Urusi - Gavana
- Uvamizi wa Ukraine Urusi: Tunachojua kufikia sasa
- Putin: 'Lazima tumfukuze adui nje ya eneo letu
- Hamas yasema usitishaji mapigano lazima uzingatie makubaliano ya mwezi Julai
- Mashambulizi ya Ukraine Urusi: Urusi yawahamisha raia wake
- 'Kutakuwa na tofauti ya pointi 25 kati ya Man Utd na Man City'
- Uganda: Idadi ya waliofariki katika maporomoko ya ardhi yafika 21
- Wanasiasa wa upinzani nchini Tanzania wakamatwa
- Marekani yatuma nyambizi Mashariki ya Kati huku hali ya wasiwasi ikiongezeka
- Michezo ya Olimpiki ya Paris yafika tamati
- Rubani afariki dunia baada ya helikopta kuanguka juu ya hoteli Australia
- Mazungumzo ya kusitisha mapigano lazima yazingatie mpango wa Biden- Hamas
- Ukraine na Urusi zalaumiana kuhusu moto katika kituo cha nyuklia
- Biden aeleza kwa nini alijiondoa kutoka kinyang’anyiro cha Ikulu
- Wanajeshi wa Ukraine sasa wamefika kilomita 30 ndani ya Urusi
Moja kwa moja
Na Asha Juma & Yusuf Jumah
Habari za hivi punde, Polisi watakiwa kuwaachilia waandishi waliokamatwa Mbeya ,Tanzania
Jukwaa la wahariri habari nchini Tanzania limetoa wito kwa vyombo vya dola kuwaachilia mara moja na bila masharti waandishi wa habari waliokamatwa mjini Mbeya.
Kulingana na taarifa iliotumwa kwa vyombo vya habari na Jukwaa hilo, waandishi hao walikuwa wakisubiri kufanya mahojiano na viongozi wa Chadema waliokuwa wanaendelea na kikao cha ndani ofisini.
Taarifa hiyo imeongezea kwamba waandishi hao wanaotoka mjini Dar es salaam kwasasa wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Mbalizi.
‘’ Tunavisihi vyombo vya dola kuwaachia mara moja waandishi hao na bila masharti kwa sababu kuwapo kwao katika eneo la tukio, tunaamini walikuwa wanafanya kazi na si sehemu ya siasa au chochote kilichokuwa kinaendelea’’, alisema taarifa iliotiwa sahihi na mwenyekiti wa jukwaa hilo bwana Deodatus Balile.
Vilevile Jukwaa hilo limelaani tukio hilo likisema linaharibu heshima kubwa ya Tanzania katika kulinda Uhuru wa Vyombo vya Habari aliyoujenga Rais Samia Suluhu Hassan tangu alipoingia madarakani.
Habari za hivi punde, Ukraine inadhibiti vijiji 28 vya Kursk, Urusi - Gavana
Kaimu gavana wa Kursk Alexei Smirnov amezungumza katika mkutano wa Putin na maafisa.
Smirnov amemwambia kuwa Ukraine inadhibiti vijiji 28 katika eneo hilo.
"Hali bado ni ngumu," amesema.
Vikosi vya Ukraine viko maili 7.4 (kilomita 12) ndani kabisa ya eneo hilo, na mstari wa mbele kuna upana wa kilomita 40, anasema.
Putin anakatiza, akisema "wizara ya ulinzi itaripoti kina na upana" na kumtaka "atueleze kuhusu hali ya kijamii na kiuchumi na jinsi watu wanasaidiwa".
Smirnov amemwambia Putin kwamba takriban raia 2,000 wa Urusi wamesalia katika maeneo yanayokaliwa na vikosi vya Ukraine huko Kursk.
"Hatujui chochote kuhusu hatima yao", anaongeza.
Uvamizi wa Ukraine Urusi: Tunachojua kufikia sasa
- Tishio la Putin: Rais wa Urusi anasema Ukraine itapata "jibu linalostahili" kwa uvamizi wake katika eneo la Urusi - na kwamba vikosi vya Urusi "vitamfukuza adui", katika mkutano na magavana wa kanda.
- Udhibiti wa Ukraine: Gavana wa eneo la Kursk - ambalo Ukraine iliingia Jumanne iliyopita - alimwambia Putin kwamba wanajeshi wa Ukraine sasa wanadhibiti vijiji 28. Wanajeshi wa Ukraine wako umbali wa maili 7.4 (kilomita 12) ndani ya eneo hilo, amesema
- Uhamisho wa watu: Gavana wa Kursk aliongeza kuwa watu 121,000 sasa wamehamishwa kutoka katika nyumba zao - na wengine 59,000 wamesalia. Huko Belgorod, eneo karibu na Kursk, karibu watu 11,000 waliambiwa kuondoka asubuhi ya Leo.
- Nini kinafuata? Tunasubiri kusikia maelezo yoyote kutoka Ukraine leo kuhusu uvamizi wao. Mwanahabari wetu Sarah Rainsford anaangalia kama hii itabadilisha maoni ya umma wa Urusi kuhusu vita - anasema ni wazi baadhi wanajiuliza maswali.
Habari za hivi punde, Putin: 'Lazima tumfukuze adui nje ya eneo letu
Tumekuwa tukipata maelezo kutoka Urusi - ambapo Rais Vladimir Putin ameitisha mkutano wa maafisa kuhusu hali katika mikoa ya mpakani.
Anauambia mkutano huo unaoenda moja kwa moja hewani katika runinga ya serikali kwamba "kazi kuu ya wizara ya ulinzi ni kusukuma, kuwafukuza adui kutoka katika eneo letu".
Pia anasema kuwa lengo la Ukraine katika shambulio hilo ilikuwa kuboresha nafasi yake ya mazungumzo.
Hamas yasema usitishaji mapigano lazima uzingatie makubaliano ya mwezi Julai
Hamas imesema mpango wa kusitisha mapigano Gaza lazima uzingatie wapi mazungumzo yalifanyika mwezi mmoja na nusu uliopita badala ya duru zozote mpya za mazungumzo.
Katika taarifa yake Jumapili usiku, kundi hilo lilitoa wito kwa wapatanishi "kuwasilisha mpango wa kutekeleza kile kilichokubaliwa na harakati mnamo Julai 2, 2024, kwa kuzingatia maono ya (Rais Joe Biden na azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa".
Mnamo tarehe 2 Julai, Hamas ilitoa majibu yake kwa muhtasari wa mpango wa kusitisha mapigano uliotangazwa na Bw Biden mnamo Mei 30.
Maelezo ya majibu ya Hamas hayajawekwa wazi lakini kundi hilo linaeleweka kuwa limetupilia mbali matakwa ya kusitishwa kikamilifu kwa mapigano hapo mwanzo badala ya usutishaji wa awali wa wiki sita uliotolewa na rais.
Mazungumzo yalianza tena wiki moja baadaye, huku Hamas ikiishutumu Israel kwa kuanzisha masharti mapya.
Unaweza kusoma;
Mashambulizi ya Ukraine Urusi: Urusi yawahamisha raia wake
Urusi inawahamisha wakaazi wake kutoka eneo la pili la mpaka, huku Ukraine ikiendelea na mashambulizi ya wiki moja ndani ya nchi hiyo.
Takriban watu 11,000 katika eneo la Belgorod wamehamishwa, vyombo vya habari vya serikali ya Urusi viliripoti, kwa sababu ya "hatua ya adui" karibu na mpaka.
Belgorod iko karibu na Kursk - ambapo wanajeshi wa Ukraine walianzisha shambulio lao la kushtukiza katika eneo la Urusi Jumanne iliyopita.
Vikosi vya Ukraine vimesonga mbele hadi maili 18 (km 30) ndani ya Urusi –ikiwa ni uvamizi mkubwa zaidi nchini humo tangu uvamizi kamili wa Moscow nchini Ukraine.
Kyiv inadai maelfu ya wanajeshi wanahusika.Siku ya Jumatatu asubuhi, wakaazi katika sehemu za Belgorod - ambayo iko kusini mwa Kursk - waliambiwa wasiwe na hofu lakini lazima wahame.
Gavana wa Belgorod Vyacheslav Gladkov alisema raia katika wilaya ya Krasnaya Yaruga walikuwa wakihamishwa kutokana na "shughuli za adui kwenye mpaka".
Pia alisema eneo lote lilikuwa chini ya tahadhari ya makombora, na aliwaambia watu wajifiche katika vyumba vyao vya chini.
Lakini aliongeza kuwa "ana uhakika kwamba wanajeshi wetu watafanya kila kitu kukabiliana na tishio ambalo limetokea".
Watu pia walikuwa wakiendelea kuhamishwa kutoka Kursk Jumatatu - na maelfu ya watu waliambiwa waondoke majumbani mwao katika wilaya ya Belovsky.
Gavana wa Belovsky Alexei Smirnov pia alitoa onyo la kombora - akisema watu walihitaji kujificha katika vyumba visivyo na madirisha na kuta thabiti.
Kasisi wa kanisa la 'kufunga hadi kufa' Paul Mckenzie akana mashtaka ya mauaji
Kiongozi wa kanisa la kufunga hadi kufa nchini Kenya Paul McKenzie amekana mashtaka ya Mauaji ya kutokusudia kufuatia vifo vya waumini zaidi ya 400 katika mkasa unaohusiana na ibada katika pwani ya Kenya.
McKenzie pamoja na washukiwa wengine 94, walifikishwa mahakamani mjini Mombasa leo siku ya Jumatatu na kukanusha mashtaka.
Kasisi huyo na washtakiwa wenzake wanakabiliwa na mashtaka mengi ya kuua bila kukusudia katika mauajiambayo yamepatiwa jina la mauaji ya Shakahola.
McKenzie ambaye alikamatwa Aprili iliyopita, baada ya miili kugunduliwa katika Msitu wa Shakahola, anatuhumiwa kuwahimiza wafuasi wake wafe kwa njaa ili "kumlaki Yesu," habari iliozua mshtuko mkubwa nchini Kenya na kote duniani.
Mwendesha mashtaka Alexander Jami Yamina amesema kuwa kesi hiyo ni ya kipekee nchini Kenya, na washukiwa watashtakiwa chini ya sheria inayohusiana na makubaliano ya kujitoa uhai.
Takriban mashahidi 420 wameandaliwa na upande wa mashtaka huku kesi hiyo ikipangwa kuendelea kwa siku nne hadi Alhamisi.
Mwezi Machi mwaka huu, mamlaka ilianza kutoa miili ya baadhi ya waathiriwa kwa ndugu zao baada ya miezi kadhaa ya kazi kubwa ya kuwatambua kwa kutumia chembechembe za DNA. Hadi sasa milii 34 imerejeshwa.
Mackenzie alikuwa ameanzisha Kanisa lake la Good News International Church mwaka wa 2003, lakini akasema alilifunga mwaka wa 2019 na kuhamia Shakahola kujiandaa na kile alichotabiri kuwa mwisho wa dunia Agosti mwaka jana.
Uganda: Idadi ya waliofariki katika maporomoko ya ardhi yafika 21
Takriban watu 21 hadi kufikia sasa wamethibitishwa kufariki dunia baada ya maporomoko ya ardhi katika eneo kubwa la kutupa taka katika mji mkuu wa Uganda, Kampala.
Waokoaji wanaendelea kuchimba uchafu huo kwa matumaini ya kupata manusura zaidi baada ya maporomoko hayo yaliyofuatia mvua kubwa iliyonyesha kwa wiki kadhaa.
Eneo la kutupa takataka la Kiteezi lenye ukubwa wa ekari 36 (hekta 14) ndilo pekee linalohudumia Kampala nzima, jiji ambalo linakadiriwa kuwa na watu milioni nne.
Meya wa Kampala Erias Lukwago aliliambia shirika la habari la AFP "ni janga [ambalo] lazima lingetokea", na kwamba "wengi, wengi zaidi bado wanaweza kuwa bado wamezikwa".
Soma zaidi:
'Kutakuwa na tofauti ya pointi 25 kati ya Man Utd na Man City'
Meneja wa Kidderminster Phil Brown anaamini kuwa Manchester City bado itamaliza pointi 25 bora zaidi kuliko wapinzani wao Manchester United kwenye Ligi ya Premia msimu huu, licha ya Erik ten Hag kununua wachezaji wapya katika soko la usajili ili kuimarisha kikosi chake.
Mabingwa wa Kombe la FA United walimaliza katika nafasi ya nane kwenye ligi msimu uliopita, pointi 31 nyuma ya mabingwa City.
"Manchester United kwa sasa, sio klabu ambayo wachezaji wanaingia na kuanza kujituma sio kulala na kuchukua muda muda," Brown aliambia Football Daily.
"Ulikuwa msimu mgumu sana kwa [Manchester] United, lakini walimaliza kifua mbele kidogo kwa [kushinda Kombe la FA], unaweza kusema.
"Sikuona mechi ya kombe la Ngao ya Jamii Jumamosi, lakini bado nasema kutakuwa na tofauti ya pointi 25 kati ya Manchester United na Manchester City msimu ujao."
Wanasiasa wa upinzani nchini Tanzania wakamatwa
Wanasiasa wa upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu na Freeman Mbowe wanashikiliwa na Jeshi la Polisi tangu usiku wa kuamkia leo kwa kile walichodaiwa kuhusika kuandaa maandamano ya vijana kwenye maadhimisho ya Siku ya vijana duniani hii leo.
Kadhalika, Jeshi hilo lilidaiwa kuwashikilia na kisha kuwaachia kwa kuwalazimisha vijana wa chama hicho kurejea mikoa wanayotokea ili wasishiriki maadhimisho hayo waliyoyapanga mkoani Mbeya, kusini mwa Tanzania.
Msemaji wa chama hicho cha upinzani, John Mrema ameiambia BBC kuwa hadi asubuhi ya leo hawajui ni kituo gani cha polisi ambapo viongozi hao watatu wanashikiliwa.
“Hatufahamu wanashikiliwa wapi ila wapo mikononi mwa polisi, tunafuatilia sambamba na mawakili wetu… Tutatoa taarifa zaidi baadaye mchana,” alisema.
Pia alisema makundi makubwa ya vijana waliokuwa kwenye mabasi ya kukodi yalisimamishwa na kukamatwa walipokuwa wakisafiri kwenda Mbeya kwa ajili ya sherehe hizo.
Mrema alisema hadi kufikia asubuhi ya leo polisi hawajaruhusu vijana hao kufika Mbeya na badala yake wamewalazimisha vijana hao kurejea katika mikoa yao wakiwa chini ya ulinzi.
Siku ya jana, Jeshi la Polisi lilitoa taarifa kuwa vijana hao wa Chadema walipanga maandamano ambayo yalikuwa yana viashiria vya kuvunja amani.
Katika taarifa iliyotolewa na jeshi hilo ilisema kuwa kiongozi mmoja wa vijana wa chama hicho alikuwa akihimiza kuwepo maandamano kama yale yaliyofanyika nchini Kenya yaliyohusisha vijana maarufu Gen Z.
Jitihada za kupata jeshi la polisi bado zinaendelea kuhusiana na taarifa hii.
Katika hatua nyingine, Jeshi la polisi nchini Tanzania limesema kuwa halijapiga marufuku kufanyika kwa mikutano ya nje ya hadhara na ile ya ndani, ili mradi inafuata matakwa ya sheria ya nchi.
Polisi imefafanua kuwa kilichopigwa marufuku ni mkusanyiko uliokuwa umeitishwa na viongozi wa Chadema huko jijini Mbeya kwa kivuli cha kuadhimisha Siku ya Vijana Duniani. Taarifa imeeleza.
Pia unaweza kusoma:
Marekani yatuma nyambizi Mashariki ya Kati huku hali ya wasiwasi ikiongezeka
Marekani imetuma manowari inayoongozwa na kombora Mashariki ya Kati, huku hali ya wasiwasi ikiongezeka katika eneo hilo.
Waziri wa Ulinzi Lloyd Austin pia alisema meli ya kubeba ndege ambayo tayari inaelekea eneo hilo itafanya safari yake kwa haraka.
Hatua hiyo inawadia kutokana na hofu ya kutokea kwa mzozo mkubwa wa kikanda, baada ya mauaji ya hivi majuzi ya viongozi wakuu wa Hezbollah na Hamas.
Inaashiria dhamira ya Marekani ya kusaidia kuilinda Israeli dhidi ya mashambulizi yoyote ya Iran - huku Bw Austin akisema Marekani "itachukua kila hatua iwezekanayo" kumtetea mshirika wake.
Iran inafuatiliwa kwa karibu katika dalili zozote za jinsi na lini inaweza kujibu mauaji ya kiongozi mkuu wa kisiasa wa Hamas Ismail Haniyeh yaliyotokea huko Tehran tarehe 31 Julai.
Wairani waliilaumu Israeli kwa mauaji ya Bw Haniyeh katika ardhi yao, na wameapa kulipiza kisasi.
Israeli haijatoa maoni yoyote lakini inaaminika kuwa ilihusika katika mauaji hayo.
Katika taarifa yake siku ya Jumapili, Ikulu ilisema Bw Austin ametuma manowari inayoongozwa kombora ya USS Georgia katika eneo hilo.
Pia ilikuwa imeamuru meli ya USS Abraham Lincoln, yenye kubeba ndege za kivita za F-35C, kuharakisha safari yake huko. Meli hiyo tayari ilikuwa njiani kuchukua nafasi ya meli nyingine ya Marekani katika eneo hilo.
Soma zaidi:
Michezo ya Olimpiki ya Paris yafika tamati
Nyota wa michezo na muziki walikusanyika pamoja katika sherehe za Paris 2024 ili kukamilisha mashindano ya Michezo ya 33 ya Olimpiki.
Mwigizaji Tom Cruise alikuwa katika uwanja wa Stade de France na kuchukua bendera ya Olimpiki kama sehemu ya makabidhiano kwa jiji la Marekani la Los Angeles, ambalo litakuwa mwenyeji wa Michezo inayofuata mnamo mwaka 2028.
Red Hot Chili Peppers, Billie Eilish, Snoop Dogg na Dr. Dre kisha wakatumbuiza kwenye Ufuo wa Venice kama sehemu ya kuhitimisha sherehe hiyo.
Hapo awali, ndani ya uwanja wa michezo wa Paris, washindi wa medali za dhahabu Alex Yee na Bryony Page walikuwa washika bendera wa Uingereza kwenye sherehe hiyo.
Uingereza ilimaliza katika nafasi ya saba kwenye jedwali la medali ikiwa na dhahabu 14, fedha 22 na shaba 29. Ikiwa ni jumla ya idadi ya medali 65, moja zaidi ya 64 walizoshinda Tokyo 2020.
Katika hotuba yake ya mwisho, rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) Thomas Bach alizungumzia Michezo hiyo "ya kuvutia".
Michezo ya Olimpiki ya Walemavu ya 2024 itafanyika katika mji mkuu wa Ufaransa kutoka 28 Agosti hadi 8 Septemba.
Soma zaidi:
Rubani afariki dunia baada ya helikopta kuanguka juu ya hoteli Australia
Rubani mmoja amefariki baada ya helikopta kuanguka kwenye paa la hoteli moja katika mji wa Cairns kaskazini mwa Queensland.
Ndege hiyo ilianguka kwenye hoteli ya DoubleTree mwendo wa 01:50 usiku kwa saa za eneo hilo siku ya Jumatatu, na kuwaka moto ambapo mamia ya wageni walihamishwa eneo salama.
Mamlaka inasema mtu pekee aliyekuwa kwenye helikopta hiyo ndiye aliyefariki katika eneo la tukio, huku wageni wawili wa hoteli hiyo - mwanamume mwenye umri wa miaka 80 na mwanamke mwenye umri wa miaka 70 - walipelekwa hospitalini na wako katika hali nzuri.
Polisi wa Queensland na waangalizi wa usalama wa anga wanachunguza mazingira ya ajali hiyo, huku kampuni inayokodisha helikopta hiyo ikisema ilikuwa katika safari ambayo "haikuidhinishwa".
Amanda Kay, ambaye alikuwa akiishi katika hoteli kwenye eneo kuu la esplanade huko Cairns, alielezea kuona helikopta ikiwa eneo la "chini zaidi", bila taa katika hali ya hewa ya mvua.
"[Imegeuka] na kuanguka kwenye jengo," alisema, akiongeza kuwa ndege "iliwaka moto".
Mtu mwingine alisema aliona helikopta hiyo ikipita karibu na hoteli hiyo mara mbili kabla ya kuanguka.
Pia unaweza kusoma:
Mazungumzo ya kusitisha mapigano lazima yazingatie mpango wa Biden- Hamas
Hamas imesema kuwa kuanzishwa tena kwa mazungumzo yoyote ya kusitisha mapigano kuhusu mzozo wa Gaza kunapaswa kuzingatia mipango ya awali badala ya kuanza duru mpya za mazungumzo.
Wiki iliyopita, wapatanishi wa kimataifa kutoka Qatar, Misri na Marekani walizitaka Israel na Hamas kuhudhuria mazungumzo ya kusitisha mapigano na kuwaachilia mateka tarehe 15 Agosti.
Israel ilijibu siku ya Alhamisi, ikisema itatuma timu ya wapatanishi kushiriki katika mkutano huo.
Mazungumzo yalikwama mwezi uliopita, baada ya masharti mapya kuanzishwa kwa mfumo uliowasilishwa na Rais wa Marekani Joe Biden mnamo mwezi Mei.
Katika taarifa ya pamoja wiki iliyopita, wapatanishi walisema mazungumzo yanaweza kufanyika tarehe 15 Agosti huko Doha au Cairo.
Ilitoa wito kwa Israel na Hamas "kuziba mapengo yote yaliyosalia na kuanza utekelezaji wa mpango huo bila kuendelea kuchelewa".
Ilisema "mkataba wa mfumo" unaozingatia "kanuni" zilizoainishwa hapo awali na Bw Biden mnamo mwezi Mei 31 ulikuwa tayari - ambao ulipendekeza mpango ambao ungeanza na usitishaji kamili wa mapigano na kuachiliwa kwa mateka kadhaa.
Katika taarifa, Hamas ilijibu shinikizo kutoka kwa wapatanishi kwa kutaka makubaliano yafanyike kulingana na "maono" ya Bw Biden kuanzia mwezi Mei - kimsingi wakikubali kuanza tena mazungumzo kutoka mahali walipoachia badala ya mpango wowote mpya.
Vyanzo vya habari viliiambia BBC kwamba kuanzishwa kwa masharti mapya ya Israeli - kwamba Wapalestina waliokimbia makazi yao wanapaswa kuchunguzwa wanaporejea kaskazini mwa Gaza, pamoja na suala la udhibiti wa ukanda wa Philadelphi unaopakana na Misri – ndio vimekuwa kikwazo.
BBC inaelewa kuwa Hamas iko tayari kuanzisha tena mazungumzo kuanzia pale yalipoachiwa.
Mapigano ya hivi majuzi huko Gaza na mauaji ya kiongozi wa kisiasa wa Hamas Ismail Haniyeh na kamanda mkuu wa Hezbollah yamehatarisha kuongezeka kwa mvutano katika eneo hilo.
Soma zaidi:
Ukraine na Urusi zalaumiana kuhusu moto katika kituo cha nyuklia
Ukraine na Urusi zimelaumiana baada ya moto kuzuka katika kinu kikubwa cha nyuklia cha Zaporizhzhia siku ya Jumapili.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema kuwa vikosi vya Urusi vimeanzisha moto katika kiwanda hicho ambacho kimekaliwa na wanajeshi wa Moscow kwa zaidi ya miaka miwili. Gavana wa Zaporizhzhia aliyewekwamadarakani na Kremlin alisema mashambulizi ya makombora ya Ukraine yalisababisha moto huo.
Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia masuala ya nyuklia lilisema liliona "moshi mkali mweusi" ukitoka kwenye kituo hicho - lakini wakasema "hakuna madhara yaliyoripotiwa" kwa usalama wa nyuklia.
Hatua hiyo inakuja wakati wanajeshi wa Ukraine wamesonga mbele hadi kilomita 30 ndani ya Urusi, katika uvamizi wa kina na muhimu zaidi tangu Moscow ilipoanza uvamizi wake kamili mnamo Februari 2022.
Siku ya Jumapili, Yevgeny Balitsky, gavana wa Zaporizhzhia aliyewekwa na Kremlin, alisema moto ulizuka kwenye minara ya kupozea umeme ya kiwanda hicho cha kuzalisha umeme.
Alilaumu makombora ya Ukraine, lakini akaomba "utulivu", akiongeza kuwa hakukuwa na mionzi karibu na mtambo huo.
Bw Zelensky pia alisema hakukuwa na ongezeko la mionzi iliyogunduliwa au hatari ya uvujaji wa nyuklia - lakini aliishutumu Urusi kwa kukusudia kuanzisha moto huo kwa kujaribu "kukashifu" Kyiv.
Mapema Jumatatu, Vladimir Rogov, afisa mwingine aliyewekwa madarakani na Kremlin, alisema moto "umezimwa kabisa" katika chapisho la Telegraph.
Kiwanda hicho cha nguvu za nyuklia kimekuwa chini ya udhibiti wa wanajeshi na maafisa wa Urusi tangu 2022. Kiwanda hicho hakijazalisha umeme kwa zaidi ya miaka miwili na vinu vyote sita vimezimwa tangu Aprili.
Unaweza pia kusoma
Biden aeleza kwa nini alijiondoa kutoka kinyang’anyiro cha Ikulu
Rais wa Marekani Joe Biden anasema alijiondoa katika azma yake ya kugombea tena urais kwa sababu alihofia kwamba vita vya ndani ya chama kuhusu kugombea kwake vingekuwa "usumbufu wa kweli" kwa wademocrat na kwamba kipaumbele chake kikuu kilikuwa kumshinda Donald Trump mnamo Novemba.
Katika mahojiano yake ya kwanza tangu ajiondoe kwenye kinyang'anyiro hicho, Biden mwenye umri wamiaka 81, alisema "hana tatizo kubwa" na afya yake. Alilaumu utendakazi wake duni katika mdahalo kwa kuwa mgonjwa wakati huo, na kutupilia mbali wasiwasi kuhusu umri wake na hali yake ya kiakili.
Rais huyo wa Marekani aliahidi kumfanyia kampeni Kamala Harris akisema atafanya chochote ambacho makamu wake "anafikiri naweza kufanya kumsaidia pakubwa".
"Lazima, lazima, lazima tumshinde Trump," aliambia shirika la utangazaji la Marekani CBS News.
Bw Biden alisema kama angeendelea na kampeni yake, kinyang'anyiro cha urais kingekuwa "na ushindani wa karibu sana".
"Baadhi ya wenzangu wa chama cha Democratic katika Ikulu na Seneti walidhani kwamba ningewaumiza katika kinyang'anyiro," alisema.
"Na nilikuwa na wasiwasi kama ningesalia kwenye kinyang'anyiro hicho, hiyo ndiyo ingekuwa mada. Ungekuwa ukinihoji kuhusu, Kwa nini Nancy Pelosi alisema, kwa nini alifanya hivyo - na nilifikiri itakuwa ni usumbufusana."
Spika wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Nancy Pelosi aliripotiwa pakubwa kuongoza vuguvugu la kumtimua Bw Biden - madai ambayo hajakanusha haswa - baada ya kusitisha mjadala wake dhidi ya Trump mnamo 27 Juni.
Wakati wa mahojiano yaliyorekodiwa kabla ya kutangazwa Jumapili, Bw Biden alikosea mara kadhaa lakini kwa ujumla alionekana kuelewekazaidi kuliko wakati wa mjadala wa moja kwa moja wa televisheni. Alisisitiza utendakazi wake duni wa mdahaloulisababishwa na ugonjwa - hapo awali pia alitaja uchovu wa safari yandege na ukosefu wa kupumzika kama sababu.
Shinikizo zilipokuwa zikiendelea kupanda, alitangaza kujiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho tarehe 21 Julai.
Mapambano yaliyotarajiwa yakuchukua nafasi yake ya tiketi ya chama cha Democratic hayakutokea na uungwaji mkono wa chama ulishikana haraka nakumuunga mkono Makamu wa Rais Harris, ambaye hadi sasa amemshinda Bw Biden katika kura za maoni.
Rais amesema alinuia kuwa daraja kwa kizazi kijacho alipowaniakuingia Ikulu mnamo 2020.
"Nilipogombea mara ya kwanza, nilijiona kama rais wa mpito. Siwezi hata kusema nina umri gani. Ni vigumu kwangu kuitoa kinywani mwangu."
Unaweza pia kusoma
Wanajeshi wa Ukraine wapo kilomita 30 ndani ya eneo la Urusi
Wanajeshi wa Ukraine wamesonga mbele hadi kilomita 30 ndani ya Urusi, katika hali ambayo imekuwa uvamizi mkubwa na muhimu zaidi tangu Urusi ilipoanza uvamizi wake dhidi ya Ukraine mnamo Februari 2022.
Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema kuwa vikosi vyake vimewakabili wanajeshi wa Ukraine karibu na vijiji vya Tolpino na Obshchy Kolodez, huku mashambulizi katika eneo la Kursk yakiingia siku ya sita.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje Maria Zakharova alishutumu Ukraine kwa "kuwatisha watu wenye amani wa Urusi".
Rais Volodymyr Zelensky, ambaye alikiri moja kwa moja shambulio hilo kwa mara ya kwanza katika hotuba jana usiku, alisema mashambulizi 2,000 ya kuvuka mpaka yameanzishwa na Urusi kutoka Kursk majira haya ya joto.
"Silaha, makombora, ndege zisizo na rubani. Pia tumerekodi mashambulio ya makombora, na kila shambulio kama hilo linastahili jibu sahihi," Bw Zelensky aliiambia nchi katika hotuba yake ya usiku kutoka Kyiv.
Afisa mmoja mkuu wa Ukraine aliliambia shirika la habari la AFP kwamba maelfu ya wanajeshi walishiriki katika operesheni hiyo, ikiwa ni zaidi ya uvamizi mdogo ulioripotiwa hapo awali na walinzi wa mpaka wa Urusi.
Wakati vikundi vinavyoungwa mkono na Ukraine vimeanzisha mashambulizi ya mara kwa mara ya kuvuka mpaka, mashambulizi ya Kursk yanaashiria shambulio kubwa lililoratibiwa katika eneo la Urusi na vikosi vya kawaida vya Kyiv.
Soma zaidi:
Habari ya asubuhi msomaji wetu, karibu katika matangazo ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 12/08/2024.