Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Paris Olimpiki 2024: Kwa mara ya kwanza yaweka maeneo kwa wanaonyonyesha
- Author, Nishat Ladha
- Nafasi, BBC Sport Africa
- Author, Marina Daras
- Nafasi, BBC Africa
- Muda wa kusoma: Dakika 5
"Nililia sana kwenye basi nikielekea kwenye kijiji cha mashindano ya Olimpiki. Nilikuwa nikitazama tu video za mtoto wangu na kuangalia picha zake.”
Huyo ni mkimbiaji wa mbio za marathoni, Aliphine Tuliamuk alipokuwa anaelekea kwenye Michezo ya Olimpiki ya Tokyo mwaka 2021, akimzungumzia bintiye wa miezi sita, Zoe.
Michezo hiyo ilikuja katikati ya janga la Covid-19, na mbio za marathoni zilifanyika katika jiji la kaskazini mwa Japani la Sapporo.
Wana michezo hawakuweza kuchukua watoto wao. Tuliamuk alikuwa mbali na mtoto wake ambaye alikuwa akinyonya.
"Zoe na mume wangu walikaa hotelini. Ilikuwa ngumu sana," anasema Tuliamuk. “Kisha niliwapigia simu, na alikuwa akilia, kwa sababu hakuelewa kwa nini mama yake hayupo."
Mkimbiaji huyo Mmarekani, mzaliwa wa Kenya amefurahishwa na utaratibu mpya kwa ajili ya mama wenye watoto na walezi huko Paris 2024, wa kuweka maeneo maalumu kwa watoto katika maeneo ya wana michezo.
Olimpiki kwa akina mama na walezi
Shirika la Afya Duniani (WHO) na Unicef wanapendekeza watoto wanyonyeshwe maziwa ya mama pekee katika miezi sita ya kwanza ya maisha yao na waendelee kuwanyonyesha na kuwapa chakula hadi watakapofikisha miaka miwili au zaidi.
Bodi kuu ya Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) na Paris 2024, wameandaa maeneo kwa ajili ya watoto kwa mara ya kwanza katika historia ya Olimpiki.
"Tumejifunza mengi kutoka Tokyo na Michezo ya awali na tunataka kuboresha maisha ya wana michezo," anasema Emma Terho, mwenyekiti wa tume ya wanariadha wa IOC.
"Tuna wanariadha wengi ambao wana watoto wadogo, na akina mama ambao huacha kushindana mara tu baada ya kujifungua.
"Kwahiyo wataweza kuendelea na mashindano ikiwa kuna kituo kinachowawezesha kuwa na mtoto na mlezi karibu na Michezo ya Olimpiki."
Kituo hicho kitatoa nafasi na faragha kwa akina mama wanaonyonyesha ambao wataweza kukamua na kuhifadhi maziwa yao. Pia kutakuwa na maeneo ya kubadilishia nepi na sehemu za kuchezea.
Malazi ya usiku pia yatapatikana nje ya kijiji cha Olimpiki, ikiwa Kamati za Kitaifa za Olimpiki (NOCs) zitakubali kufadhili.
Tuliamuk anasema eneo la marathoni la Sapporo mwaka 2021, halikuwekwa kwa ajili ya akina mama wenye watoto.
"Kulikuwa na hema la Timu ya Marekani, lakini hapakuwa na mahali pa kunyonyesha au kukamua maziwa," anasema mama huyo wa miaka 35.
"Ilikuwa inanibidi niende bafuni kukamua maziwa, lakini sikuwa na muda wa kutosha.
"Ingekuwa vyema kama kungekuwa na hema la faragha, lakini hakuna mtu aliyefikiri huenda kuna wanariadha ambao wananyonyesha."
Mabadiliko makubwa
Terho anasema ushirikiano kati ya kamisheni ya wanariadha wa IOC na kamisheni kama hiyo ya Paris 2024, ulisaidia kufanikisha mpango wa maeneo kwa wenye watoto.
Bingwa mstaafu wa Olimpiki wa mita 200, Allyson Felix wa Marekani, amekuwa mstari wa mbele kwenye kampeni hizo.
Nyota wa judo wa Ufaransa, Clarisse Agbegnenou, ambaye ni bingwa mara mbili wa Olimpiki, pia ametetea kuwepo kwa maeneo kwa ajili ya wanawake wenye watoto.
"Inaniuma kusikia watu wakisema 'Tunaweza kufanya jambo moja tu kwa wakati mmoja, huwezi kuwa mwanariadha wa kiwango cha juu' huku ukiwa mama," Agbegnenou aliiambia Olympics.com.
Mwanariadha wa mbio za kati wa Marekani, Alysia Montano ndiye mwanzilishi wa kikundi cha &Mother, kilichoanzishwa ili kutetea hali bora, mikataba na ufadhili. Felix yuko kwenye bodi ya wakurugenzi ya kikundi hicho.
Montano aliwahi kukimbia katika mbio za raia wa Marekani 2014, huko Sacramento akiwa na ujauzito wa miezi minane.
Miezi michache baadaye, akiwa amebanwa na mkataba ambao ungemfanya apoteze msaada wa kifedha ikiwa angechukua likizo yoyote ya uzazi, Montano alilazimika kufunga tumbo lake baada ya kujifungua ili aendelee na mazoezi.
Kutafuta namna ya kuendelea kunyonyesha wakati wa kusafiri pia ilikuwa changamoto.
"Nilishinda medali ya dhahabu ya Ubingwa wa Dunia. Tulivunja rekodi ya Marekani. Nilitafuta njia za kukamua maziwa yangu na kuyafunga na kuyarudisha kwa binti yangu huko Marekani wakati nikiwa safarini.
"Na niligundua kuwa hakuna mfumo ambao unaunga mkono jambo hili. Ndiyo sababu ni jambo gumu sana."
Montano anasema utaratibu mpya wa Paris 2024 ni hatua muhimu katika mwelekeo sahihi.
"Tumekuwa watetezi wa kubwa wa kile kinacho paswa kufanywa, kwa lengo la kuunga mkono wanariadha wote wa Olimpiki, tukijua hii ni hatua kubwa kwa ulimwengu wote."
Ya kwanza katika historia
Mojawapo ya vikwazo vikubwa kwa akina mama ambao wanataka kulala kwa usiku mmoja na watoto wao nje ya kijiji cha Olimpiki, itakuwa ni kuzishawishi kamati za michezo kufadhili gharama hizo.
Terho wa IOC anasema shirika linaangazia hili kwa ajili ya Olimpiki zijazo, lakini kwanza wanahitaji kufuatilia hali huko Paris.
Kwa wanaharakati kama Montano, mengi zaidi yanahitajika kufanywa kabla ya Olimpiki za Los Angeles 2028.
“Ningependa kuona viwanja viko salama vikiwa na makazi ya heshima ya kunyonyesha, vikiwa na sehemu yenye umeme ili kukamua maziwa na kuwepo sehemu salama ya kuhifadhi maziwa," anasema Montano.
"Bado ni gharama kubwa kuwa na nyaya au mtu ambaye anaweza kuwa nawe kwa siku 14 nje ya nchi. Tungependa kuona mashirika na serikali za kitaifa zikisaidia familia wakati huu."
Tuliamuk, amekosa kucheza Paris 2024 kutokana na jeraha, anatazamia kushiriki LA 2028, akitumai atapata usaidizi anaouhitaji ikiwa atakukuwa na mtoto mwingine wakati huo.
"Kuwa na mtoto wako katika kijiji cha Olimpiki, hakutobadilisha kile unachoweza kufanya. Tumeona akina mama wanachoweza kufanya wakipewa usaidizi wa 100%. Tuendelee kufanya hivyo.”
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla