Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Siri ya silaha ya siri ya urusi iliyoanguka Ukraine
Njia mbili za moshi mweupe zinapoonekana kuvuka anga karibu na mstari wa mbele wa mapigano mashariki mwa Ukraine, huwa inamaanisha jambo moja: Ndege za Urusi zinakaribia kushambulia.
Lakini kilichotokea karibu na jiji la Kostyantynivka hakikuwa cha kawaida. Njia ya chini iligawanyika mara mbili na kitu kipya kikaongeza kasi kuelekea njia nyingine ya wingu hadi zilipovuka na mwangaza mkali wa rangi ya chungwa ukamulika angani.
Je, ilikuwa, kama wengi walivyoamini, ndege ya kivita ya Urusi iliyotungua ndege nyingine katika kile kinachoitwa shambulio la kirafiki umbali wa kilomita 20 kutoka mstari wa mbele, au ndege ya Ukraine ndiyo iliyoiangusha ndege ya Urusi?
Wakiwa na shauku, Waukraine waligundua punde kutokana na vifusi vilivyoanguka kwamba walikuwa wamejionea tu uharibifu wa silaha mpya zaidi ya Urusi - ndege isiyo na rubani ya S-70.
Hii sio droni ya kawaida. Ndege hiyo nzito isiyo na rubani inayoitwa Okhotnik (Hunter), ni kubwa kama ndege ya kivita lakini haina chumba cha marubani. Ni vigumu sana kuigundua na watengenezaji wake wanadai kuwa "haina ya kulinganishwa nayo" ulimwenguni.
Hiyo yote inaweza kuwa kweli, lakini ilipotea njia waziwazi, na inaonekana njia ya pili iliyoonekana kwenye video ilikuwa ni ya ndege ya Urusi ya Su-57, ikiifuata.
Huenda ndege ya Urusi ilikuwa ikijaribu kurejesha mawasiliano na ndege hiyo isiyo na rubani, lakini zote mbili zilipokuwa zikipaa katika eneo la ulinzi wa anga la Ukraine, inadhaniwa uamuzi ulifanywa wa kuiangamiza Okhotnik ili kuizuia kuishia mikononi mwa adui.
Moscow na Kyiv hazijatoa maoni rasmi juu ya kile kilichotokea angani karibu na Kostyantynivka.
Lakini wachambuzi wanaamini kuwa huenda Warusi walipoteza udhibiti wa ndege zao zisizo na rubani, labda kutokana na kukwama kwa mifumo ya vita vya kielektroniki ya Ukraine.
Vita hivi vimeshuhudia ndege nyingi zisizo na rubani lakini hakuna kama S-70 ya Urusi.
Ina uzani wa zaidi ya tani 20 na inasemekana inauwezo wa masafa ya kilomita 6,000 (maili 3,700).
Ikiwa na umbo la mshale, inaonekana kuwa na umbo sawa na ya Marekani X-47B, ndege nyingine isiyo na rubani ya kivita iliyoundwa muongo mmoja uliopita.
Ndege hiyo ya Okhotnik inadaiwa kuwa na uwezo wa kubeba mabomu na roketi kwa ajili ya kupiga shabaha za ardhini na angani pamoja na kufanya uchunguzi.
Na, kwa kiasi kikubwa, imeundwa kufanya kazi kwa kushirikiana na ndege za kivita za Urusi za Su-57 za kizazi cha tano.
Imekuwa ikifanyiwa matengenezo tangu 2012 na safari ya kwanza ya ndege hiyo ilifanyika mnamo 2019.
Lakini hadi mwishoni mwa juma lililopita hakukuwa na ushahidi kwamba ilitumika katika vita vya Urusi vilivyodumu kwa miaka miwili na nusu nchini Ukraine.
Mapema mwaka huu iliripotiwa kuonekana katika uwanja wa ndege wa Akhtubinsk kusini mwa Urusi, moja ya maeneo ya uzinduzi wa mashambulizi ya Ukraine.
Kwa hivyo inawezekana kusafiri kwa ndege juu ya Kostyantynivka ilikuwa moja ya majaribio ya kwanza ya Moscow kujaribu silaha yake mpya katika hali ya mapigano.
Mabaki ya moja ya bomu la masafa marefu la D-30 la Urusi yalipatikana katika eneo la ajali ya ndege hiyo.
Silaha hizi hatari hutumia muongozo wa satelaiti na hivyo kuwa hatari zaidi.
Hivyo basi Okhotnik alikuwa akifanya kwa kusafiri pamoja na ndege ya Su-57? . Kwa mujibu wa mtaalamu wa masuala ya usafiri wa anga anayeishi Kyiv Anatoliy Khrapchynskyi, huenda ndege hiyo ya kivita ilituma ishara kutoka kwenye kituo cha ardhini hadi kwenye ndege isiyo na rubani ili kuongeza kiwango cha operesheni yao.
Kufeli kwa ndege hiyo isiyo na rubani bila shaka ni pigo kubwa kwa jeshi la Urusi. Ilipaswa kuanza kutumika mwaka huu lakini ni wazi ndege isiyo na rubani haiko tayari.
Aina nne za S-70 zinafikiriwa kutengenezwa na inawezekana ile iliyolipuka kutoka angani juu ya Ukraine ndiyo ilikuwa ya hali ya juu zaidi kati ya hizo nne.
Ingawa iliharibiwa, vikosi vya Ukraine bado vinaweza kukusanya habari muhimu kuhusu Okhotnik.
"Tunaweza kujifunza kama ina rada zake za kutafuta shabaha au kama risasi zimeratibiwa mapema na kuratibu mahali pa kupiga," anaelezea Anatoliy Khrapchysnkyi.
Kwa kusoma tu picha kutoka kwa tovuti ya ajali, anaamini ni wazi kwamba uwezo wa siri wa droni ni mdogo.
Kwa vile injini yake ina umbo la duara, anasema inaweza kutambuliwa na rada.
Bila shaka mabaki hayo yatachunguzwa na wahandisi wa Ukraine na matokeo yao yatapelekwa kwa washirika wa Kyiv wa Magharibi.
Na bado, tukio hili linaonyesha Warusi wameweza kujisimamia, wakitegemea rasilimali zao kubwa za watu na silaha za kawaida.
Wanafanya kazi kwa njia mpya na nadhifu za kupigana vita. Na kilichoshindikana leo kinaweza kufanikiwa wakati ujao.
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi