Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Putin achora 'mstari mwekundu' kuhusu matumizi ya makombora ya masafa marefu dhidi ya Urusi
Kichwa cha habari katika gazeti la Kommersant la leo asubuhi kilisema hivi.
"Vladimir Putin achora mstari mwekundu."
Je, Magharibi itavuka? Na ikiwa itafanya hivyo, Urusi itajibu vipi?
Akizungumza mjini St Petersburg, Rais Putin alituma onyo la wazi kwa nchi za Magharibi: usiruhusu Ukraine kutumia makombora yako ya masafa marefu kushambulia eneo la Urusi.
Moscow, alisema, itachukulia hatua hiyo kama "ushiriki wa moja kwa moja" wa nchi za Nato katika vita vya Ukraine.
"Hatua hiyo ingebadilisha kwa kiasi kikubwa kiini, asili cha mzozo," kiongozi wa Kremlin aliendelea.
"Hii itamaanisha kuwa nchi za Nato, Marekani na mataifa ya Ulaya, zinapigana na Urusi."
Alidai kwamba, kwa kurusha makombora kwenda Urusi, Ukraine ingehitaji data kutoka kwa satelaiti za Magharibi na kwamba wanajeshi kutoka nchi wanachama wa Nato pekee ndio wanaweza "kuingiza misheni ya ndege kwenye mifumo hii ya makombora".
Urusi imechora mistari myekundu hapo awali. Na kuwaona wakivuka hapo awali.
Tarehe 24 Februari 2022, alipotangaza kuanza kwa "operesheni yake maalum ya kijeshi" - uvamizi kamili wa Ukraine - Rais Putin alitoa onyo kwa "wale ambao wangejaribu kuingilia kutoka nje".
"Haijalishi ni nani anayejaribu kusimama katika njia yetu au kuunda vitisho kwa nchi yetu na watu wetu, lazima wajue kwamba Urusi itajibu mara moja," kiongozi wa Kremlin alikuwa ametangaza.
"Na matokeo yake yatakuwa ambayo haujawahi kuona katika historia yako yote."
Viongozi wa Magharibi walipuuza kile ambacho kilitafsiriwa sana wakati huo kama nubabe wa silaha za nyuklia.
Nchi za Magharibi zimeipatia Ukraine mizinga, mifumo ya hali ya juu ya makombora na, hivi majuzi, ndege za kivita za F-16 za Marekani.
Mwaka huu Urusi tayari imeishutumu Ukraine kwa kutumia makombora ya masafa marefu ya Marekani ya ATACMS kulenga rasi ya Crimea, ya Ukraine iliyotwaliwa na Urusi.
Zaidi ya hayo, zaidi ya miaka miwili iliyopita, maafisa wa Urusi na vyombo vya habari vya serikali hapa mara nyingi wameshutumu Magharibi kwa "kupigana na Urusi" au kuanzisha "vita" dhidi ya Urusi. Hata ingawa ni Urusi iliyoivamia Ukraine.
Lakini kutokana na sauti ya matamshi ya hivi punde zaidi ya Rais Putin, ni wazi kwamba anazingatia kwamba kulengwa kwa eneo la Urusi linalotambulika kimataifa na mifumo ya makombora ya Magharibi kungeufanya mzozo kuchukua mwelekeo tofauti.
Ambacho hakuweka wazi hapo jana ni jinsi Moscow ingejibu.
"Tutachukua maamuzi kulingana na vitisho ambavyo tutawekewa ," Vladimir Putin alisema.
Siku ya Ijumaa, Urusi ilifuta vibali vya wanadiplomasia sita wa Uingereza, ikiwatuhumu kwa "shughuli za uasi" na kutishia usalama wa Urusi.
Lakini majibu ya Putin ni mapana zaidi. Alitoa vidokezo kadhaa mapema mwezi Juni.
Katika mkutano na wakuu wa mashirika ya habari ya kimataifa, aliulizwa: Je, Urusi itachukua hatua gani ikiwa Ukraine ingepewa fursa ya kushambulia maeneo ya Urusi kwa silaha zinazotolewa na Ulaya?
"Kwanza, bila shaka, tutaboresha mifumo yetu ya ulinzi wa anga. Tutakuwa tunaharibu makombora yao,” Rais Putin alijibu.
"Pili, tunaamini kwamba ikiwa mtu anafikiria kuwa inawezekana kusambaza silaha kama hizo kwenye eneo la vita ili kupiga eneo letu na kuleta matatizo kwa ajili yetu, kwa nini hatuwezi kusambaza silaha zetu kwenye maeneo hayo duniani kote? watalenga vituo nyeti vya nchi zinazofanya hivi kwa Urusi?"
Kwa maneno mengine, kuwapa silaha maadui wa Magharibi kushambulia Magharibi nje ya nchi ni jambo ambalo Moscow imekuwa ikizingatia.
Mapema mwezi huu, naibu waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Sergei Ryabkov, alitangaza kwamba Urusi inatazamiwa kurekebisha sera yake ya nyuklia: hati ambayo inaweka wazi chini ya hali gani Moscow inaweza kufikiria kutumia silaha za nyuklia.
Alipendekeza kwamba uamuzi wa kurekebisha sera hiyo "ulisababishwa na mwenendo wa maadui [wa Urusi] wa Magharibi".
Wakati huo huo, Sir Keir Starmer yuko Washington kwa mazungumzo na Rais Biden.
Miongoni mwa masuala ambayo viongozi hao wawili wanatarajiwa kujadili ni suala la Ukraine na makombora ya masafa marefu.
"Urusi ilianzisha mzozo huu. Urusi iliivamia Ukraine kinyume cha sheria,” Sir Keir alisema alipokuwa akielekea Washington. "Urusi inaweza kumaliza mzozo huu mara moja."
Viongozi wa Magharibi watahitaji kuamua ni lipi wanaloliona kuwa kubwa zaidi: hatari ya kuongezeka kwa mzozo huu, au hitaji la kuondoa vikwazo kwa matumizi ya Ukraine ya makombora ya magharibi.
Imetafsiriwa na na kuchapishwa na Seif Abdalla