Urusi na Ukraine: Kati ya Urusi na Ukraine nani ana jeshi lililo na nguvu zaidi?

Rais wa Urusi Vladimir Putin ameamuru kutuma wanajeshi mashariki mwa Ukraine. Amechukua hatua hii baada ya kutambua maeneo mawili yanayodhibitiwa na waasi nchini Ukraine kuwa ni mataifa huru.

Putin anasema jeshi lake linakwenda huko "kulinda amani" lakini Marekani imeitaja hatua hiyo kama upuuzi.

Baada ya hayo, sasa picha zinakuja kwamba jeshi la Urusi linaelekea maeneo haya mawili ya Ukraine.

Urusi ilikuwa imetuma wanajeshi wapatao laki mbili kwenye mpaka wa Ukraine kwa muda wa miezi kadhaa iliyopita. Kufuatia hili vitengo vya kijeshi sasa vitavuka mpaka wa Ukraine.

Jeshi la Urusi lina mizinga na silaha zingine katika mkusanyiko huu, pia wanapata msaada wa jeshi la anga na la wanamaji.

Wakati huo huo, Rais wa Ukraine amesema kuwa nchi yake haigopi chochote wala mtu yeyote.

Kuna wanajeshi wangapi wa Urusi huko?

Inakadiriwa kuwa idadi ya wanajeshi wa Urusi ndani na karibu na Ukraine inaweza kuwa kati ya 100,000 na 190,000 katika wiki za hivi karibuni.

Ijumaa iliyopita, Marekani ilisema kuwa Urusi imetuma wanajeshi kati ya 169,000 na 190,000 ndani na karibu na Ukraine.

Michael Carpenter, balozi wa Marekani katika Shirika la Usalama na Ushirikiano la Ulaya (OSCE), alisema: "Idadi hii inajumuisha wanajeshi walioko karibu na mpaka na Ukraine, na Belarus, na katika Crimea inayokaliwa.

Wakati huo huo, Waziri wa Ulinzi wa Uingereza Ben Wallace alisema kuwa asilimia 60 ya wanajeshi wa Jeshi la Urusi wako karibu na mpaka wa Urusi na Belarusi.

Kwa upande mwingine, Waziri wa Ulinzi wa Ukraine alikuwa ametoa nambari hii kama 149,000.

Urusi haijasema chochote wazi juu ya haya yote. Naibu Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Dmitry Polansky alisema - "Yote haya ni mawazo ya wenzetu wa Magharibi."

Wiki iliyopita, wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema baadhi ya wanajeshi katika wilaya zake za kusini na magharibi wamemaliza mazoezi yao na wanarejea katika kambi zao za kudumu.

Lakini Jumuiya ya kujihami ya NATO ilisema kwamba haijaona ushahidi wowote wa hii ardhini.

Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg kisha akasema, "Kinyume chake, inaonekana kwamba Urusi inaongeza mipango ya kijeshi."

Maafisa wa nchi za Magharibi walisema kwa sharti la kutotajwa majina kwamba kutokana na taarifa za kijasusi wanazozipata sasa, inaonekana kwamba wanajeshi wa Urusi wamefika eneo ambalo Ukraine inaweza kushambuliwa.

Wanasema kuwa theluthi mbili ya jeshi liko ndani ya kilomita 50 kutoka mpakani.

Picha za satelaiti pia zinaonyesha kuwa baadhi ya wanajeshi wa Urusi wamegawanywa katika vikundi vidogo karibu na mpaka wa Ukraine.

Lakini wataalam wengi wanaamini kwamba Urusi italazimika kukusanya wanajeshi wengi zaidi kuliko ilivyo sasa ili kuishambulia kabisa Ukraine, kuweza kutekan nchi nzima au sehemu yake.

Uwezo wa kijeshi wa Ukraine na msaada wa NATO

Jeshi la Ukraine ni dogo zaidi kuliko lile la Urusi, lakini linapata usaidizi kutoka kwa Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Magharibi NATO.

Marekani haijatuma wanajeshi wowote nchini Ukraine lakini imetuma wanajeshi 3,000 zaidi nchini Poland na Romania ili kuimarisha vikosi vya NATO, na imewaweka wanajeshi wengine 8,500 katika hali ya tahadhari.

Marekani pia imetuma silaha zenye thamani ya dola milioni 200, ikiwa ni pamoja na kombora la kushambulia vifaru la Javelin na kombora la kudungua ndege la Stinger. Pia imeruhusu nchi wanachama wa NATO kukabidhi silaha zilizotengenezwa Marekani kwa Ukraine.

Uingereza imepeleka makombora 2,000 ya kushambulia vifaru ya masafa mafupi nchini Ukraine, imetuma wanajeshi 350 zaidi nchini Poland, na kuongeza mara mbili uwezo wake wa kijeshi kwa kutuma wanajeshi 900 zaidi nchini Estonia.

Uingereza imetuma ndege zaidi za kivita kusini mwa Ulaya na meli ya wanamaji pamoja na wanajeshi wengine wa NATO kupiga doria bahari ya Mediterania.

Pia imewatahadharisha wanajeshi wake 1,000 ili iwapo kutatokea shambulio, wasaidie wakati wa mzozo wa kibinadamu nchini Ukraine.

Denmark, Uhispania, Ufaransa na Uholanzi pia zimetuma wanajeshi na meli zao Ulaya Mashariki na mashariki mwa Mediterania.

Na kwa upande mwingine, Ufaransa pia inapanga kuliongoza jeshi la Nato nchini Romania na kutuma wanajeshi wake huko, lakini Nato inasema kuwa itachukua wiki kadhaa kukamilisha mpango wake wote.

NATO ilifanya nini kwa Ukraine hapo awali?

Mnamo mwaka 2014, watu wa Ukraine walimwondoa rais aliyeunga mkono Urusi, na baada ya hapo Urusi ilikalia jimbo la kusini mwa Ukraine la Crimea.

Aliwasaidia pia waasi wanaounga mkono Urusi kuchukua sehemu kubwa ya Mashariki mwa Ukraine.

NATO haikuingilia kati wakati huo, lakini kwa mara ya kwanza ilikuwa imepeleka vikosi vyake katika nchi nyingi za Ulaya Mashariki ili kukabiliana na hili.

NATO imepeleka vitengo vinne vya kimataifa vya ngazi ya battalion huko Estonia, Latvia, Lithuania na Poland na kikosi kimoja cha kimataifa nchini Romania.

Unaweza pia kusoma:

Pia imeongeza ufuatiliaji wa anga katika nchi za Baltic na Ulaya Mashariki ili ndege yoyote ya Urusi iweze kuzuiawa ikiwa itakiuka anga ya nchi wanachama wa NATO.

Urusi inabaki yenye hasira kufuatia hili na inataka vikosi hivi viondoke.