Uchaguzi Urusi: Kwa nini haikuwa vigumu kwa Putin kushinda urais?

Chanzo cha picha, MIKHAIL KLIMENTYEV/Sputnik/AFP
- Author, Laura Gozzi na Francis Scarr
- Nafasi, BBC
Kremlin ilihakikisha Vladimir Putin hakuwa na mpinzani wa uhakika na hivyo kuwa rahisi kushinda muhula wa tano kwa kishindo.
Katika sherehe kubwa ya tuzo za kijeshi mwezi Desemba mwaka jana - ndipo Vladimir Putin, 71, aliuambia umma wa Urusi kwamba atagombea tena urais.
"Sasa ni wakati wa kufanya maamuzi. Nitagombea urais wa Shirikisho la Urusi," alitangaza katika hafla hiyo.
Tayari amekuwa madarakani nchini Urusi kwa muda mrefu kuliko mtawala yeyote tangu dikteta wa Sovieti Joseph Stalin.
Amekuwa rais tangu 2000, mbali na miaka minne kama waziri mkuu kwa sababu ya ukomo wa mihula miwili iliyowekwa na katiba ya Urusi.
Tangu wakati huo amebadilisha sheria ili kujipa nafasi ya kugombea tena 2024. Hiyo ina maana kwamba anaweza pia kugombea muhula mwingine wa miaka sita 2030, atakapofikisha miaka 78.
Wakati wa utawala wake, Vladimir Putin ameimarisha nguvu zake kwa utaratibu ambao hakuna tishio kwa utawala wake. Wakosoaji wake wakubwa ama wamekufa, wako jela au uhamishoni.

Chanzo cha picha, REUTERS/Yulia Morozova
Mwaka huu, upigaji kura ulikuwa rahisi zaidi kuliko hapo awali, ulimalizika siku ya Jumapili, na idadi ya waliojitokeza inakisiwa kuwa ni zaidi ya 74%.
Katika maeneo ya Ukraine inayokaliwa kwa mabavu ambayo Urusi inayaita "maeneo mapya," upigaji kura uilifunguliwa siku 10 kabla ya siku ya uchaguzi, na mitandao ya kijamii ilikuwa imejaa matangazo ya kuwataka watu kwenda kupiga kura.
Putin hakuwa na mpinzani

Chanzo cha picha, Kremlin Press Office
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Aliyejiunga na kiongozi wa Urusi kwenye kura alikuwa Nikolai Kharitonov, akiwakilisha Chama cha Kikomunisti, ambacho kinasalia kuwa chama cha pili maarufu zaidi cha Urusi.
Wagombea wengine wawili walikuwa Leonid Slutsky wa LDPR na Vladislav Davankov wa New People, chama cha kiliberali, kinachounga mkono biashara.
Licha ya misimamo yao tofauti ya kisiasa, wote watatu waliunga mkono kwa mapana sera za Kremlin - na hakuna aliyekuwa na nafasi ya kushinda dhidi ya aliye madarakani.
Mwingine ni - diwani wa eneo la Moscow Boris Nadezhdin - alitangaza kugombea mwaka jana, na kuleta matumaini kwa wapiga kura wenye nia ya upinzani.
Alikuwa mgeni mara kwa mara kwenye vipindi vya mazungumzo kwenye runinga na amekuwa akikosoa vita vya Moscow nchini Ukraine.
Lakini katika nchi ambayo wengi wamefungwa kwa kukosoa vita, hakuweza kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwa mgombea.
Maelfu wakiwa kwenye foleni ili kumpa saini za kumuunga mkono, wasimamizi wa uchaguzi nchini Urusi walikataa ombi lake, wakidai zaidi ya 15% ya sahihi alizokusanya zilikuwa na dosari.
Kutengwa kwa Nadezhdin kwenye kinyang'anyiro hicho kulimaliza uwezekano wowote wa Putin kushindwa.
Mijadala ya televisheni ilifanyika katika maandalizi ya upigaji kura, bila Vladimir Putin kushiriki. Badala yake, matangazo ya televisheni ya mikutano yake na wafanyakazi, askari na wanafunzi ilionekana.

Chanzo cha picha, Russian Communist Party
Kwa mtu ambaye ametumia miaka 20 kama rais, Vladimir Putin amethibitisha kutoweza kutatua mengi ya matatizo ya ndani.
Badala yake, zaidi ya 40% ya bajeti ya Urusi mwaka 2024 inatumika kwa jeshi na usalama wa taifa. Na Urusi ina tatizo kubwa la rushwa - ina maana fedha mara nyingi hazifikii kwa walengwa.
Lakini hayo hayakuwa katika mijadala katika uchaguzi ambao waangalizi wengi wa kimataifa wanaamini haukuwa huru na wa haki.

Chanzo cha picha, REUTERS/Maxim Shemetov
Kumekuwa na vitendo vya kupinga uchaguzi, haswa siku ya kwanza ya kupiga kura, rangi ilimiminwa kwenye masanduku ya kura na kumekuwa na visa vya uchomaji moto pia.
Lakini upinzani mkuu ni maandamano, ambapo wapinzani wa kiongozi huyo wa muda mrefu walihimizwa kwenda kwenye vituo vya kupigia kura nchini Urusi na balozi zake nje ya nchi siku ya Jumapili na kumpigia kura yeyote isipokuwa wasimpigie Putin.
Hatua hiyo iliasisiwa na Alexei Navalny, ambaye alikufa gerezani mwezi uliopita, na kukaziwa na mjane wake Yulia Navalnaya, ambaye anasema mume wake aliuawa na Vladimir Putin .

Chanzo cha picha, LDPR/YouTube
Bi Navalnaya alisema madhumuni ya kampeni hiyo ilikuwa ni kuruhusu wafuasi kutambuana kimyakimya katika vituo vya kupigia kura.
Machi 18, Warusi wataamka na kukuta Rais Putin amechaguliwa tena.
Atakapotokea kwenye mkutano wa ushindi huko Moscow, anaweza hata kumwaga machozi - kama alivyofanya baada ya uchaguzi wa rais wa 2012 - na kuwashukuru sana wapiga kura kwa imani waliyoweka kwake.
Kwa miaka sita ijayo, demokrasia ya maji taka itaendelea.
Imetafsiriwa na Rashid Abdalla














