Je, Urusi na China zinanufaika na juhudi za Trump kutwaa Greenland?

Chanzo cha picha, Gettyimages/BBC
- Author, Paula Adamo Iduetta
- Akiripoti kutoka, BBC World Service
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa Marekani inapaswa kuichukua Greenland ili kuzuia Urusi na China kuchukua udhibiti wa eneo hilo la Denmark lenye mamlaka ya kujitawala kwa kiasi.
"Lazima tuilinde Greenland. Tusipofanya hivyo, China au Urusi watachukua nafasi," Trump aliwaambia waandishi wa habari mapema mwezi huu.
Aliongeza kwa msisitizo: "Sitaki China na Urusi wawe majirani zangu huko Greenland. Hilo halitatokea."
Wachambuzi wengi wa siasa za kimataifa wanaamini kuwa azma ya Trump ya kuichukua Greenland, pamoja na vitisho vya matumizi ya nguvu na vikwazo vya kiuchumi ili kufanikisha lengo hilo, huenda ikapokelewa vyema na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, na Rais wa China, Xi Jinping.
"Nadhani Urusi na China hawaamini bahati waliyoipata," anasema Maria Marticiot, mchambuzi katika Kituo cha Sera za Ulaya.
"Ni kwa manufaa yao kuona Ulaya, pamoja na NATO kama muungano, vikigawanyika, huku mshirika wao mwenye nguvu zaidi akitishiwa," anaongeza, akirejelea Taiwan kisiwa ambacho Beijing inakiona kama jimbo lililojitenga na inaamini hatimaye kitarudi chini ya udhibiti wake.
"Hali hii inawanufaisha kikamilifu Urusi na China, kwa kuwa inaweza kuhalalisha hatua za Urusi nchini Ukraine na matarajio ya China kuhusu Taiwan."
Kwa mtazamo huo huo, mkuu wa sera za mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, aliandika katika mtandao wa kijamii wa X:
"Urusi na China zina kila sababu ya kufurahi. Ndizo zinazofaidika na mgawanyiko kati ya washirika."
Hata hivyo, hali halisi huenda isiwe rahisi kama inavyoonekana.
Wachambuzi wa BBC, akiwemo Tony Han, wamechunguza kwa kina mtazamo wa kweli wa Urusi na China kuhusu mvutano kati ya Trump na Ulaya kuhusiana na Greenland.
Majibu ya Urusi yamekuwaje?

Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kauli za hivi karibuni za Rais Trump kuhusu nia ya kuipata Greenland zimechukuliwa na wengi kama ishara ya kurejea kwa lugha na fikra za upanuzi wa mamlaka ya nchi, zinazofanana kwa kiasi kikubwa na hoja alizowahi kutumia Rais wa Urusi, Vladimir Putin, kuhalalisha kunyakua Crimea.
Trump amewasilisha Greenland kama zawadi ambayo Marekani iliipa Denmark zamani, simulizi linalofanana na hoja za enzi za Umoja wa Kisovieti zilizoeleza Crimea kama "zawadi" kwa Ukraine.
Kauli yake kuwa Marekani itachukua Greenland "kwa njia yoyote ile" inakumbusha msimamo mkali wa Putin dhidi ya Kyiv.
Hata hivyo, Moscow imejibu kwa tahadhari kubwa.
Putin alitania kuwa Trump ana fedha za kutosha kuinunua Greenland, akifananisha suala hilo na mchezo wa ubao, lakini akasisitiza kuwa "halihusiani na Urusi."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, alilinganisha kwa uangalifu, akisema Greenland ni muhimu kwa usalama wa Marekani kama Crimea ilivyo kwa Urusi, lakini aliepuka kuunga mkono wazi madai ya Trump.
Kwa hakika, Kremlin haijatoa uungwaji mkono wa moja kwa moja, na ukimya huo una maana kubwa. Ikizingatiwa tabia ya Trump ya kupenda sifa, uungwaji mkono wa Moscow ungeweza kuwa na manufaa kwa Urusi.
Swali linabaki: kwa nini Kremlin inajibu kwa tahadhari, ilhali mvutano kati ya washirika wa Magharibi ungeweza kuipendelea Urusi kwa kuondoa umakini kwenye vita vya Ukraine?
Kwa mujibu wa mchambuzi Alexander Baunov wa Kituo cha Carnegie Eurasia, kutotabirika kwa Trump kunatia wasiwasi zaidi kuliko faraja kwa Moscow. Urusi ina hofu kuhusu kile anachokiita "nguvu ya uharibifu isiyo na mipaka" ya rais huyo wa Marekani.
Trump, kama Putin, anachangia kudhoofisha mfumo wa sasa wa utawala wa dunia mfumo ambao Urusi haijaridhika nao.
Lakini iwapo mfumo huo utaporomoka kabisa, Urusi itapinga nini, na itahalalisha vipi matarajio yake ya baadaye?
Kwa sasa, Kremlin inaendelea kuchunguza na kufuatilia hali hiyo kwa tahadhari.
China imechukulia vipi agizo la Trump kuidhibiti Greenland?

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa upande wa China, maafisa wake wameitaka Marekani kuheshimu misingi ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa, ikiwemo kuheshimu mipaka ya nchi na uhuru wao wa kisiasa.
Vyombo vya habari vya serikali ya China vimekuwa wazi zaidi.
Mtandao wa CGTN umeeleza vitisho vya Marekani vya kuichukua Greenland kama "usaliti mkubwa" kwa mwanachama mwenzake wa NATO na ishara ya "karibu kusambaratika" kwa muungano huo.
"Kudhoofika au kugawanyika kwa muungano wa Atlantiki ni habari njema kwa China," alisema José Ignacio Torblanca, mtafiti katika Baraza la Ulaya la Mahusiano ya Kimataifa aliambia BBC's China World Service.
"Wazungu wanavyokabiliana na Marekani, ndivyo itakuwa rahisi kwa Vladimir Putin, mshirika wa kimkakati wa Uchina, kustawi," anaendelea. "Na kulazimika kujilinda dhidi ya Urusi huku pia wakisimama dhidi ya Marekani kutaondoa motisha yoyote ya kuwa upande wa Marekani katika Pasifiki."
Wataalam wa China pia wamekosoa vikali jitihada za Marekani kuwasilisha shughuli zake katika eneo la Aktiki kama tishio.
Kupitia mpango wa kimkakati wa China wa kuendeleza njia za meli na miundombinu katika Aktiki almaarufu "Polar Silk Road", China inalenga fursa za kisayansi, kiuchumi na kimkakati katika eneo hilo, hasa kutokana na kuyeyuka kwa barafu kunakofungua njia mpya za usafiri wa baharini.
Mnamo Oktoba 2025, meli ya kwanza kusafiri kwa njia mpya ya Aktiki kutoka China hadi Ulaya ilifika kwenye bandari ya Felixstowe nchini Uingereza.
Greenland imekuwa kivutio kwa kampuni za China, hususan katika miradi ya miundombinu na rasilimali madini, ingawa juhudi nyingi zimekwama kutokana na vikwazo vya kisiasa.
Mnamo mwaka wa 2018, kampuni kubwa ya ujenzi inayomilikiwa na serikali ya China ilikuwa ikishindania kandarasi ya kukuza miundombinu ya uwanja wa ndege wa Greenland. Lakini baada ya Marekani kuibua wasiwasi, serikali ya Denmark iliingia na kufadhili mradi huo, na hatimaye kampuni ya China ilijiondoa kwenye shindano hilo.
Rasilimali muhimu zaidi za kimkakati za Greenland ni madini adimu, Mataifa yanakodolea macho hasa maeneo mawili ya Quanfield na Tenbrys, ambayo yana madini hayo muhimu.
Madini hayo yanayotumika katika utengenezaji wa teknolojia za kisasa kama simu janja, magari ya umeme na vifaa vya anga.
Kampuni za China tayari zinatawala soko la dunia la madini hayo, na upatikanaji wa Greenland ungeimarisha zaidi nafasi hiyo, jambo linaloibua hofu kwa Marekani na washirika wake.
Makampuni ya China yamejaribu kupata maslahi katika hifadhi ya madini ya Greenland lakini, kama ilivyo kwa miradi ya viwanja vya ndege, yamekabiliwa na vikwazo vya kisiasa.
Kampuni ya Shenghe Resources ya China ilipata hisa ya pili kwa ukubwa katika mradi wa Quanfield, lakini ilisimamisha uzalishaji baada ya Greenland kupitisha sheria ya kupiga marufuku uchimbaji wa urani.
Wakati huo huo, mradi wa Tenbreeze umeripotiwa kuchukuliwa na kampuni ya Critical Metals Corp. yenye makao yake makuu mjini New York baada ya maafisa wa Marekani kumtaka mmiliki wa awali kutoiuza kwa kampuni ya China.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid












