Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwa nini Uswizi ina makaazi mengi ya kujikinga na shambulio la nyuklia ulimwenguni?
"Ikiwa unataka amani, jitayarishe kwa vita."Na ndivyo ilivyokuwa, angalau huko Uswizi.
Katika kina kirefu cha mwamba mgumu wa milima ya Alps nchini Uswizi kuna mtandao wa mahandaki au makaazi ya kiraia na ya kijeshi yaliozingirwa na kinga ya zege ilioundwa kulinda raia dhidi ya shambulio lolote la nyuklia.
Milango yao imefichwa chini ya vilima, nyuma ya milango midogo msituni, au hata chini ya majengo ambayo yanajifanya kuwa nyumba, lakini kwa kweli yana kuta za zege zenye urefu wa mita mbili na madirisha yenye mashimo yanayotumika kuweka bunduki tayari kukabiliana na adui.
Uswizi iliyo na raia milioni 8.8, ina makaazi mengi mengi zaidi ya kujilinda dhidi ya shambulio la kinyuklia kwa kila mtu duniani: ikiwa ni zaidi ya 370,000. Takwimu za hivi punde zinaonyesha.
Sheria ya 1963 inahakikisha kwamba raia wote, ikiwa ni pamoja na wageni na wakimbizi, wana uhakika wa kumiliki makaazi ya kujilinda dhidi ya tukio la vita vya silaha au maafa ya nyuklia katika nchi yao au nchi jirani.
Nafasi ya kila mtu lazima iwe angalau mita moja ya mraba. Zaidi ya hayo, ni lazima ziwe ziko umbali usiozidi dakika 30 kutoka nyumbani, au dakika 60 katika maeneo ya milimani.
Umbali wa rahisi, si tu kutokana na ukubwa wa nchi, lakini pia kwa sababu wamiliki wa vitalu vya ghorofa wanatakiwa kujenga na kuandaa makao katika nyumba zao zote.
"Wengi wa wakazi wanaishi katika majengo ambayo yanajumuisha nyumba hizo . Ikiwa hakuna makazi hayo katika jengo linalokaliwa, kuna makaazi kama hayo yaliotengewa ," inaelezea Ofisi ya Shirikisho ya Ulinzi wa Kiraia.
Makazi yameundwa kwa ajili ya matumizi ya vita na lazima yaweze kulinda raia dhidi ya athari za silaha za kisasa. Ni lazima watoe ulinzi dhidi ya vitu hatari kama vile silaha za nyuklia, kibayolojia na kemikali, pamoja na silaha za kawaida.
Ni utamaduni wa ulinzi wa kiraia na raia, badala ya kijeshi.
"Ganda gumu la nje la makaazi linaweza kustahimili angalau tani 10 za shinikizo kwa kila mita ya mraba (yaani, paa 1), ambayo ina maana kwamba linaweza kustahimili kuporomoka kwa jengo juu yake," unaelezea ulinzi wa raia.
Baada ya tetemeko la ardhi, kwa mfano, makao yanaweza kutoa malazi ya dharura, na aina ya chujio lililowekwa linaweza kulinda dhidi ya silaha za kibiolojia na kemikali, kwani husafisha hewa ya nje iliyochafuliwa.
'Ni vizuri kujiandaa'
"Inanifanya nijisikie salama zaidi nikijua kwamba kuna mahali pa kujikinga kwa kila mtu iwapo kutatokea shambulio la nyuklia au maafa. Sidhani kama vita nchini Uswizi au mojawapo ya nchi jirani ni hali inayowezekana. Hata hivyo, nadhani ni vyema kuwa tumejitayarisha," Nicolas Städler anaiambia BBC Mundo kutoka mji wa Basel, kwenye mpaka wa Ujerumani na Ufaransa.
Lakini anakiri kwamba hivi sasa, ikiwa kuna jambo lingetokea, hajui mahali ambapo angelazimika kwenda.
Kwa Daniel Jordi, naibu mkurugenzi wa Ofisi ya Shirikisho ya Ulinzi wa Raia, kujua mahali pa kujificha ni muhimu ..
"Makaazi ya kujikinga unayopaswa kwenda yanahusishwa na anwani yako. Lakini ni kawaida kwa familia kubadilisha nyumba au kuhama. Kujua mahala palipo makazi yao kunaweza kusababisha kuchanganyikiwa. Je, ni ya zamani? Je, ni mapya? Pendekezo letu ni kuzungumzia kuhusu hilo wakati unaohitajika ," Jordi anasema.
Kuwepo kwa mtandao huu kulianza tangu Vita vya Pili vya Dunia, wakati nchi hiyo ilipojipata katikati ya Ujerumani ya Nazi ya Hitler, Italia ya Kifashisti ya Benito Mussolini, na nia yake yenyewe ya kutoegemea upande wowote. Uswizi imejiepusha na vita vya kigeni tangu 1815.
Kipindi cha Vita Baridi kilichochea zaidi ujenzi wa makaazi haya na sasa yote lazima yakaguliwe kila baada ya miaka 10 na kupata cheti.
Kwa sasa baadhi ya makaazi haya yamekuwa , vyumba vya kuhifadhia vilivyojaa watu, au pishi za divai, kutaja chache. Baadhi ni makumbusho, hoteli, au mikahawa.
"Wazo lilikuwa kutumia makaazi haya bila kurekebisha muundo wake. Tunatarajia kwamba, wakati unakuja, wananchi watakuwa na siku mbili za kurejesha sehemu hiyo ya basement kwa matumizi yake ya awali: Mahandaki ya kujilinda ," anasema naibu mkurugenzi wa Ofisi ya Shirikisho ya Ulinzi wa Raia.
Makao yaliyojengwa yapata miaka 50 au 60 iliyopita
Baadhi ya makaazi hayo yako katika hali mbaya kutokana na kutotumika kwa miaka mingi, lakini zote lazima zikaguliwe kila baada ya miaka 10 na kupokea cheti kwamba kila kitu kiko sawa au kulipia ili kirekebishwe.
"Sijisikii kulindwa zaidi. Mageuzi ya silaha za vita yamefikia hatua ambapo mashambulizi dhidi ya raia nchini Uswisi yanaweza kusababisha vifo vingi," anaeleza Eugenio Garrido, wakili kutoka Jamhuri ya Dominika ambaye ameishi Zurich kwa miaka mingi.
"Sina uhakika kama makazi yaliyojengwa miaka 50 au 60 iliyopita yangekomesha mashambulizi kama hayo," anaongeza.
Na, "kutokana na kubadilika kwa hali ya usalama duniani," serikali ya Uswizi inataka kuboresha mtandao huo wa makaazi na inapanga kuwekeza dola za Marekani milioni 250 ili kuufanya kuwa wa kisasa, kuhakikisha kwamba vyumba hivyo vinafanya kazi na tayari kutumika katika tukio la dharura.
Mamlaka zilisisitiza kuwa uboreshaji wa makazi sio maandalizi ya vita, lakini ni uwekezaji katika usalama wa umma.
Isabel anaishi Zurich. Pia hana uhakika ni wapi makaazi yake ya kujificha yapo iwapo kutotokea dharura , lakini anaiambia BBC Mundo kwamba kujua kuna mahali pa kujifichia kunampa "amani ya akili."
"Nadhani ni hatua kubwa ya kulinda idadi ya watu dhidi ya maafa au migogoro yoyote ya nyuklia; inanipa amani ya akili kujua kwamba mimi na familia yangu tuna mahali pa kujilinda."
"Jinsi ulimwengu unavyoenda, hakuna jambo linaloweza kuzuiwa, lakini ninatumaini kwamba Uswisi itadumisha kutoegemea upande wowote na kuendelea kuwa mahali salama kwa wakazi wake na kuwapa hifadhi watu wenye uhitaji," asema, akirejelea roho ya jadi ya Uswizi ya kukaribisha na kutounga mkono upande wowote.
Sio kitambo sana , Uswisi ilikaribisha maelfu ya Wayahudi waliokimbia Ujerumani ya Nazi ya Hitler.
Lakini uamuzi wa serikali ya Uswizi kupitisha vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Urusi uliashiria mabadiliko makubwa kutoka kwa msimamo wa muda mrefu wa nchi hiyo usiofungamana na upande wowote na mtazamo wa umma.
'Kuongezeka kwa mahitaji'
Kulingana na vyombo vya habari vya ndani, makampuni ya Uswizi yaliyobobea katika ujenzi wa vyumba hivyo yameripoti ongezeko kubwa la maswali na maombi tangu kuanza kwa vita. Kwa mfano, Oppidum Bunkers, wajenzi wa makazi ya kifahari, waliripoti "ongezeko la mara kwa mara" katika maswali kuhusu bidhaa zake katika miezi ya hivi karibuni.
Na makampuni kama vile Mengeu AG na Lunor yamepata "mlipuko wa maombi" ya kurekebisha au kuthibitisha utendakazi wa vyumba vilivyopo, ambavyo vingi ni vya miaka ya 1960 na 1980 na vinahitaji marekebisho ya haraka.
Daniel Jordi, kutoka Ulinzi wa Kiraia, anathibitisha: "Ndiyo, tangu vita vya Ukraine, tumepokea maswali mengi zaidi, kutoka kwa raia na kutoka kwa majimbo, ambayo yana jukumu la kuhakikisha kuwa makazi yapo tayari na kwamba watu wanayafikia."
Wimbi la maswali mara nyingi hujumuisha, "Bunker yangu iko wapi?" "Je! ninayo?" "Je, bado ni nzima?" "Nawezaje kurekebisha yangu?"
Eneo lililojipata kati ya migogoro ya kigeni
"Kwa muda mrefu, Uswizi ilikuwa eneo lililojipata kati ya nchi zinazopingana au kambi. Hali hiyo ilidumu kwa karne nyingi, ikijumuisha nyakati za vita na migogoro kati ya Ufaransa, Urusi, na baadaye Ujerumani.
Tangu mwisho wa Vita Baridi, Uswizi ilionekana kuwa kisiwa ndani ya bara la Ukraine, lakini hali ya amani na utulivu imathiriwa na matokeo ya vita vya Ukraine.
Na kwa kuwa matokeo ya vita huko Ukraine hayajulikani, nchi nyingine zimeitikia kwa njia sawa, kama vile majimbo ya Baltic, Finland, Norway, na Sweden.
Wakati ambapo mataifa yenye nguvu ya Ulaya yameamua kuongeza matumizi katika ulinzi na silaha, Uswizi imeanzisha tena mfumo wa zamani wa ulinzi ambao uliiruhusu kusalia nje ya migogoro ya silaha katika karne iliyopita.
Imetafsiriwa na Seif Abdalla