Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, makazi ya Israel yanaweza kuhimili mashambulizi ya makombora?
Katika hatua za nyuma, maswali kadhaa yalijiri akilini miongoni mwa Waisraeli kuhusu uwezo wa kiulinzi wa Israeli na nafasi ya kunusurika kutokana na mashambulio ya makombora yanayoweza kutokea na kuongezeka kwa mvutano upande wa kaskazini na Lebanon.
Ijapokuwa kuna mifumo ya ulinzi ya anga ambayo Israel inaitegemea yanapotokea mashambulizi dhidi yake, yawe ya makombora au ndege zisizo na rubani, miundombinu imeandaliwa kulinda raia kupitia makazi yao.
Makazi nchini Israeli yamegawanywa katika miundo mitatu: "mamad", ambacho ni chumba kilichoimarishwa ndani ya kila ghorofa, "mamak", ambacho ni chumba kilichoimarishwa ndani ya jengo la makazi, na "mekelat", ambacho ni chumba kilichowekwa ngome katika mitaa na barabara.
Makao mengi yanajumuisha vyumba vilivyojengwa kwa saruji na milango ya chuma.
Je, makazi haya yana uwezo gani wa kujikinga dhidi ya makombora?
Jeshi la Israel limeiambia BBC kuwa makao hayo yameundwa kukabiliana na vitisho mbalimbali ikiwemo makombora ya masafa marefu.
Hatahivyo msemaji wa Kamandi ya Makazi hayo hakuwa na uhakika kwamba makazi yanalinda dhidi ya makombora ya balestiki, wakati wa majadiliano kwenye kipindi cha Channel 13 ya Israeli kuhusu uwezo wa makazi kuwalinda Waisraeli dhidi ya mashambulio ya moja kwa moja.
Je, majengo yote ya Israeli yana ngome ya ulinzi?
Baadhi ya takwimu zilizochapishwa na vyombo vya habari vya Israel zinasema kuwa zaidi ya asilimia 62 ya nyumba za Waisraeli hazina vyumba vya kujilinda na mashambulizi.
Hii ni kwa sababu nyumba za zamani zilizojengwa kabla ya 1991 hazina vyumba vya kujilinda dhidi ya mashambulizi ya makombora.
Baada ya kuanza kwa Vita vya Ghuba, mkandarasi wa ujenzi wa Israeli alitakiwa kujenga chumba cha kujilinda dhidi ya mashambulizi kama sehemu ya vibali vya ujenzi vilivyohitajika.
Yeyote ambaye yuko ndani ya nyumba yake angeelekea moja kwa moja kwenye chumba chake cha kujihifadhi, na ikiwa ving'ora vingesikika mitaani, Waisraeli wangeelekea kwenye makazi ya umma yaliojengwa kuhimili makombora mitaani.
Na ikiwa hakuna makazi katika eneo hilo, lazima watoke nje ya magari yao na kulala chini hadi ving'ora visimame.
Afisi simamizi ya Israel Home Front iliiambia BBC kwamba inafanya utafiti unaoendelea kuchunguza uwezo wa makazi kustahimili vitisho vyovyote.
Imetafsiriwa na Seif Abdalla