Israel na Hezbollah zachezea moto lakini hakuna kati yao anayetaka vita vingine

Uhasama wa kisiasa usio wa kawaida uliongezeka kati ya Israel na Hezbollah wiki hii, hata kama mashamulizi ya makombora yalipungua.

Mabadilishano makali ya hivi majuzi ya silaha wakati wa sikukuu ya Waislamu ya Eid al-Adha na vitisho vikali, ikawa ni mtindo uliozoeleka wa kujizuia kutokea kwa vita.

Kiongozi wa Hezbollah, Hassan Nasrallah, Jumatano alitishia kuvamia kaskazini mwa Israel ikiwa vita kamili na Israel vitazuka.

Pia alisema Hezbollah walikuwa na "silaha mpya" ambazo zingeonekana kwenye uwanja wa vita.

Lakini, aliongeza kuwa kundi hilo halikutaka vita na Israel - na kuchukulia kuhusika kwake kama msaada kwa mshirika wake Hamas huko Gaza.

Siku ya Jumanne, Hezbollah ilitoa picha za ndege zisizo na rubani katika mji wa kaskazini mwa Israel wa Haifa, na maeneo muhimu ya kijeshi na ya kiraia yakiwa yanaonekana kwenye video hiyo.

Ilionekana kote kama tishio lisilo la moja kwa moja kwa Israel kutozidisha mzozo huo - shamulizi baya kwa mji wa Haifa kungeweza kusababisha vita vya pande zote.

Bw Nasrallah alisema ni sehemu ya "vita vya kisaikolojia" vya Hezbollah dhidi ya adui yake.

Saa chache baada ya video hiyo kutolewa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Israel Katz, alisema nchi hiyo "iko karibu sana na wakati wa uamuzi wa kubadilisha sheria dhidi ya Hezbollah na Lebanon".

Katika vita vya pande zote, alisema, "Hezbollah itaangamizwa na Lebanon itashambuliwa vibaya".

Jeshi la Israel lilisema kuwa mipango ya operesheni ya mashambulizi nchini Lebanon "imeidhinishwa na kuthibitishwa".

Kuna maoni yanayoshikiliwa na watu wengi kwamba si Israel wala Hezbollah wanaotaka kuanzisha vita hivi sasa. Vita hivyo - kati ya maadui wawili waliojihami vizuri - vinaweza kuhatarisha uharibifu kwa mamilioni ya watu wa pande zote za mpaka, na pia kuna hatari ya kuvuta wasaidizi wa Hezbollah, Iran, na Marekani, mshirika mkuu wa Israel.

Lakini mpaka kati ya kujizuia na hamu ya vita unazidi kuwa mgumu kuonekana.

Soma zaidi:

Baadhi katika serikali ya Israel wanaamini kwamba mashambulizi ya Hamas tarehe 7 Oktoba yalibadilisha suala zima la usalama, na kwamba wakaazi wa maeneo ya kaskazini hawataweza kurejea makwao isipokuwa ikiwa Hezbollah itashindwa vitani.

Wakazi wengi wa kaskazini wanakubaliana na hilo.

Zaidi ya watu 60,000 wamekuwa wakiishi katika makaazi ya muda mbali na mpaka tangu Hezbollah ilipoanza kurusha roketi na makombora kaskazini mwa Israel kumuunga mkono mshirika wake wa Palestina, Hamas.

Zaidi ya Walebanon 90,000 pia wameyakimbia makazi yao huku wanajeshi wa Israel wakijibu mashambulizi ya angani na mizinga.

Kura ya maoni ya Waisrael 800 wiki hii na Taasisi ya Sera ya Watu wa Kiyahudi iligundua kuwa zaidi ya 60% walitaka kushambulia Hezbollah "kwa nguvu yote".

Zaidi ya theluthi moja (36%) walisema walitaka kufanya hivyo "haraka iwezekanavyo" - hata kabla ya Israel kumaliza kupigana na Hamas huko Gaza. Idadi hiyo imeongezeka tangu kura kama hiyo kufanyika miezi mitatu iliyopita.

Vita huko Gaza ni sababu nyingine kwa nini serikali ya Israel inaweza kuwa na wasiwasi wa kuanzisha vita vya pili, vikali zaidi na Hezbollah kwa wakati mmoja.

Lakini mwezi huu iliongeza idadi ya mwanajeshi wa akiba ambayo inaweza kuwaita, kutoka 300,000 hadi 350,000, na kuchochea uvumi kwamba vita upande wa kaskazini havijaondolewa.

Serikali pia inajaribu kuongeza muda wa kuhudumu kwa wanajeshi wa akiba, ikiongeza mwaka mmoja ambao wanajeshi wanaweza kuitwa kuhudumu.

Na malengo ya pande zote mbili yameendelea kuongezeka katika kipindi cha miezi minane iliyopita, huku mashamulizi ya kuvuka mpaka yakiongezeka.

Siku chache kabla ya Eid, ndege zisizo na rubani na roketi zilisikika kutoka Lebanon, baada ya Israel kumuua kamanda mkuu wa Hezbollah, Taleb Abdallah.

Hiyo ilifuatia mwezi mmoja wa mashambulizi ya Hezbollah, na ongezeko la makombora ya vifaru na ndege zisizo na rubani zilizotumwa kuvuka mpaka.

Mzozo unaokua wa kulipiza kisasi unahatarisha kuzitumbukiza pande hizo mbili kwenye vita, ikiwa lengo linaonekana kuwa nyeti sana.

Kufikia sasa, Umoja wa Mataifa unasema zaidi ya watu 400 wameuawa nchini Lebanon, wakiwemo raia.

Takriban watu 25 - wanajeshi na raia - wameuawa nchini Israel.

Marekani ilituma mjumbe wake katika pande zote mbili za mpaka wiki hii kujaribu kutatua mzozo huo, lakini Hezbollah imekuwa wazi kwamba inafanya kazi kwa mshikamano na mshirika wake wa Hamas, na makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza yanaonekana sana kama njia pekee inayowezekana kuwa suluhisho la kidiplomasia upande wa kaskazini.

Kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anayekabiliana na vita na shinikizo la kurejesha utulivu, kuna manufaa ya kuendeleza migogoro yote miwili.

Itakuwa vigumu kwake kudai ushindi huko Gaza bila kuua, kukamata au kuondoa uongozi wa Hamas, wakati kundi hilo bado vikosi vyake viko sawa.

Na kila wiki ambapo vita dhidi ya Hamas vinaendelea, vikosi vyake vinalenga makamanda zaidi wa Hezbollah, na nafasi zaidi za Hezbollah kwenye mpaka wa kaskazini - ambayo inaweza kumsaidia kurai wakazi kurejea, wakati migogoro yote miwili itakapoisha.

Kucheza kwa muda ni utaalamu wa Bw Netanyahu.

Kwa upande wa kaskazini, pande zote mbili zinakabiliana kwa silaha.

Pia unaweza kusoma:

Imetafsiriwa na Asha Juma na kuhaririwa na Yusuf Jumah