Waandamanaji Iran: 'Walisema tusiponyamaza watatubaka'

Chanzo cha picha, Reuters
"Waliniweka chini, na afisa mmoja akaniwekea buti lake mgongoni. Alinipiga teke tumboni, akanifunga mikono, kisha akanisukuma ndani ya gari."
Hivi ndivyo Maryam mwenye umri wa miaka 51, muandamanaji aliyekamatwa wiki iliyopita katikati ya Tehran, akielezea wakati ambapo vikosi vya usalama vya Iran vilivyomuweka kizuizini.
Maandamano yameenea kote nchini Iran tangu kifo cha Mahsa Amini mnamo Septemba 16, mwanamke mwenye umri wa miaka 22 ambaye aliwekwa kizuizini na polisi wa maadili katika mji mkuu siku tatu zilizopita kwa madai ya kuvunja sheria kali za hijabu.
Polisi wanashikilia kuwa alianguka katika kituo kimoja baada ya kupata mshtuko wa moyo, lakini familia yake inadai kuwa maafisa walimpiga kichwani kwa fimbo na kugonga kichwa chake kwenye moja ya magari yao.
Maandamano yaliyochochewa na kifo chake, yakiongozwa hasa na wanawake, yalianza na matakwa ya kukomesha sheria za lazima za hijabu.
Lakini sasa yamegeuka kuwa maandamano ya nchi nzima dhidi ya viongozi wa Iran.
Makamanda 'wasio na huruma'
Licha ya kuzuiwa kwa mtandao, video za waandamanaji wakikamatwa na vikosi vya usalama vya Iran zimeendelea kuchapishwa kwenye mitandao ya kijamii.
"Ni mbaya zaidi kuliko unavyoona kwenye video hizi," Maryam, ambalo si jina lake halisi.
"Nilimsikia mmoja wa makamanda wao akiwaamuru askari wao wasiwe na huruma. Maafisa wa kike [ni] wa kutisha vile vile. Mmoja wao alinipiga kofi na kuniita jasusi wa Israel na kahaba."
BBC imeona video ambazo makamanda wanaonekana wakiwaamuru maafisa wa polisi wa kutuliza ghasia "kutowahurumia waandamanaji na kuwapiga risasi".
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe, 1
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Video nyingine zilizothibitishwa na BBC zinaonesha vikosi vya usalama vikiwafyatulia risasi waandamanaji na kuwashikilia wale walioweza kuwakamata.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali, zaidi ya watu 40 wameuawa wakati wa machafuko hayo. Mashirika ya haki za binadamu yameripoti idadi kubwa ya vifo.
Idadi ya jumla ya watu waliokamatwa haijaelezwa na mamlaka. Hata hivyo, mwendesha mashtaka mkuu wa Mazandaran, jimbo la kaskazini mwa Tehran, alisema waandamanaji wasiopungua 450 wamezuiliwa huko tu. Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema maelfu ya waandamanaji wanashikiliwa.
"Nilimsukuma afisa wa usalama nyuma na kujaribu kukimbia, lakini punde si punde, mtu wa pili na wa tatu walifika," alisema Sam, muandamanaji kijana kutoka jiji kuu. "Baada ya sekunde chache, zaidi ya 15 walikuwa wakinipiga bila huruma."
Aliongeza: “Nilihisi ladha ya damu mdomoni mwangu na mipigo ya bunduki ya umeme mwilini mwangu. Waliniweka chini, wakanifunga mikono nyuma ya mgongo wangu na kunifunga miguuni kwa kamba za viatu.
"Mmoja wa askari alinipiga teke la jicho la kushoto wakati akinipeleka [mahali] walipowaweka wafungwa wengine."
Wasichana wadogo 'wasio na woga'
Rais Ebrahim Raisi ameahidi "kushughulikia kikamilifu" maandamano hayo, ambayo sasa yameenea katika majimbo mengi 31 ya Iran.
Kwa Wairani wengi, Bw Raisi anahusishwa na mauaji makubwa ya maelfu ya wafungwa wa kisiasa katika miaka ya 1980, alipokuwa mmoja wa majaji wanne waliohusika kwenye mahakama za siri zilizowahukumu kifo.
"Waliniweka mimi na wafungwa wengine kwenye sakafu ya basi juu ya kila mmoja kwa saa moja na nusu," Sam alisema.
"Nilikuwa nikifikiria kuhusu jukumu la Raisi katika kuwanyonga wafungwa wa kisiasa, na kwa muda nilifikiri kwamba wanaweza kuninyonga."
Bw Raisi amesisitiza kuwa walionyongwa miaka ya 1980 walitiwa hatiani kwa mujibu wa sheria za Iran.
Licha ya kuwa rais ndiye anayesimamia polisi wa kutuliza ghasia na vikosi vingine vya kutekeleza sheria, hakuna ushahidi kwamba amewaamuru kuua watu waliohusika katika maandamano ya mwezi huu.

Chanzo cha picha, SOCIAL MEDIA
Maryam alisema kuwa watu waliozuiliwa kando yake waliendelea kuandamana walipokuwa wakihamishiwa katika kituo kikuu cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).
"Kulikuwa na wasichana wengine pamoja nami kwenye gari, lakini walikuwa wadogo zaidi," alisema. “Nilipowaona na ushujaa wao nilitulia wakaanza kunisaidia.
"Walikuwa wakipiga kelele na kuwakejeli maafisa. Kizazi hiki ni tofauti na kizazi changu. Hawana woga."
Picha na video zilizothibitishwa na BBC zilionyesha ndugu wa waandamanaji waliokamatwa wakipanga foleni mbele ya Gereza maarufu la Evin kaskazini mwa Tehran. Walikuwa wakisubiri kujua taarifa kuhusu wafungwa hao au kuwasilisha stakabadhi za kuwaachilia kwa dhamana.
Mtu mmoja aliambia BBC kwamba mamlaka ilikuwa imewaonya kutotangaza kukamatwa kwa ndugu zao "la sivyo hali yao ingezidi kuwa mbaya".

Lakini sio kila mtu amehamishiwa kwenye vituo vikubwa vya polisi. Wengi wanazuiliwa katika vituo vidogo vya polisi na vituo vya IRGC, ambavyo vingi havijulikani kwa umma.
"Tulihamishwa hadi kituo kidogo cha polisi. Hawakuwa tayari kupokea watu wengi," Maryam aliambia BBC. "Waliweka angalau wanawake 60, ikiwa ni pamoja na mimi, katika chumba kidogo. Tulikuwa tumesimama karibu karibu na hatuwezi kukaa au kusogea.
"Walisema hatuwezi kutumia choo, na kwamba tukipata njaa tunaweza kula kinyesi chetu.
"Baada ya takriban siku nzima tulipopiga kelele na kupinga ndani ya chumba hicho, walianza kututishia kwamba tusiponyamaza watatubaka."
'Kuendelea kuwa na ari ya juu '
Mwanamke mwingine aliyekamatwa katika moja ya miji ya kusini mwa Iran aliambia BBC kwamba maafisa wa usalama wa kike walitoa vitisho vya unyanyasaji wa kingono.
"Afisa ambaye alikuwa akitusajili katika kituo hicho aliuliza jina langu na kuniita kahaba," Fereshteh, ambalo si jina lake halisi, alisema. "Nilipolalamika, alisema kwamba nikiendelea atamwomba mmoja wa ndugu [walinzi wa kiume] aondoke pamoja nami."
Behzad, muandamanaji ambaye alizuiliwa katika kituo kikuu cha polisi huko Tehran, alisema: "Waliwaweka zaidi ya watu 80 kwenye chumba kidogo. Sote tulikuwa na hasira na maumivu."
"Walinyang'anya simu janja zetu na kupekua picha, video na ujumbe wetu kuona kama tulikuwa tumetumiana habari zozote za maandamano. Ikiwa ndivyo, [walisema] walikuwa wakiongeza mashtaka kwenye faili zetu."
"Asubuhi iliyofuata, hakimu alikuja na kukutana nasi. Walitupilia mbali mashtaka na kuwaachilia vijana wengi."
"Lakini kwa watu wazima, hakimu aliuliza maswali mafupi na kuamua hatima yetu kulingana na kikao hicho kifupi cha mahakama."
Behzad alisema takriban 10% ya watu aliozuiliwa pamoja nao waliachiliwa bila kufunguliwa mashtaka, huku wengine wakiachiliwa kwa dhamana.
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe, 2
Muandamanaji mwingine ambaye alizuiliwa kwa siku mbili mjini Tehran aliambia BBC kwamba licha ya "uhasama", vijana wadogo waliokuwa kizuizini walijaribu "kuendelea kuwa na mwamko wa hali ya juu".
"Nilikuwa na waandamanaji ambao walikuwa na umri wa chini ya miaka 25. Wengine walikuwa na damu kwenye nyuso zao, lakini walikuwa wakitabasamu, wakipiga soga, na wakifanya mzaha.
"Mmoja wao aliniuliza nitabasamu na kuongeza: 'Tumeshinda kwa sababu tuko sahihi."














