Je nini kinachofuata baada ya kifo cha Malkia?

Chanzo cha picha, Getty Images
Watu kote nchini Uingereza na ulimwengu wameguswa na kifo cha Malkia Elizabeth II.
Ingawa ratiba iliyopangwa kwa umakini ya matukio rasmi itawekwa tofauti, kifo cha Malkia kitakuwa na athari kubwa kwa maisha ya kila siku nchini Uingereza. Maelezo mengi yanapaswa kuthibitishwa, lakini kuna kipi cha kutarajia.
Je kutakuwa na mapumziko ya kitaifa?
Mazishi hayo yanatarajiwa kufanyika huko Westminster Abbey katika muda wa siku 10 au 11 na tarehe hiyo itathibitishwa na Buckingham Palace. Kuna uwezekano wa kutangazwa kuwa likizo ya benki (mapumziko ya kitaifa), lakini hii itathibitishwa na ikulu na serikali.
Ikiwa likizo ya benki itatangazwa, shule zitafungwa.
Bado haijabainika ikiwa watafunga kabisa kabla ya wakati huo. Idara ya Elimu na mamlaka zilizokabidhiwa madaraka zinatarajiwa kutoa ushauri.
Je, matukio yataghairishwa?
Ratiba ya michezo iliyopangwa Ijumaa imeghairishwa kwa kiasi kikubwa, ikijumuisha mechi za kandanda katika Ligi ya Soka ya Uingereza na Ligi ya Soka ya Ireland Kaskazini.
Mashindano ya mbio zote yameahirishwa na Mamlaka inayosimamia Mbio za Farasi ya Uingereza na kwenye gofu hakutakuwa na mchezo kwenye mashindano ya BMW PGA siku ya Ijumaa.
Hatua ya sita ya mbio za baiskeli za Tour of Britain, zilizopangwa kufanyika Ijumaa, hazitaendelea. Na siku ya pili ya mechi ya kriketi ya majaribio kati ya Uingereza na Afrika Kusini siku ya Ijumaa imeahirishwa, na hakuna uthibitisho wa ikiwa mchezo uliosalia wa siku ya tano utafanyika.
Matangazo ya BBC ya Alhamisi na Ijumaa yamesitishwa, pamoja na tamasha la Last Night of the Proms siku ya Jumamosi.
Maonyesho katika ukumbi wa michezo kote Uingereza yanatarajiwa kuendelea, lakini watatekeleza ukimya wa dakika moja. Sherehe ya tuzo ya Muziki ya Mercury imeahirishwa Alhamisi jioni baada ya habari hiyo kutangazwa.
Je, mgomo wa reli na posta utaendelea?
Muungano wa Mashirika ya Reli, Majini na Uchukuzi (RMT) umetangaza kuwa mgomo uliopangwa tarehe 15 na 17 Septemba utasimamishwa kama ishara ya heshima. Chama cha Wafanyikazi pia kimesitisha mgomo uliopangwa kufanyika Septemba.
Migomo ya posta siku ya Ijumaa pia umefutiliwa mbali na Chama cha Wafanyakazi wa Mawasiliano (CWU).
Je, kutakuwa na ibada nyingine zozote za ukumbusho kabla ya mazishi?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kutakuwa na ibada ya ukumbusho katika Kanisa Kuu la St Paul siku ya Ijumaa, itakayohudhuriwa na waziri mkuu na mawaziri wengine wakuu.
Kwa sababu Malkia alifariki huko Scotland, jeneza lake litalala katika Kanisa kuu la St Giles huko Edinburgh. Wananchi wataruhusiwa kutoa heshima zao za mwisho kwa siku chache.
Jeneza litasafirishwa kwa ndege hadi London, ambapo mamia ya maelfu ya watu wataruhusiwa kupita na kutoa heshima zao za mwisho kwa muda wa siku nne katika jimbo la Westminster Hall.
Bendera ya muungano itapeperushwa nusu mlingoti kwenye majengo ya serikali hadi asubuhi baada ya mazishi. Bendera zitarudi kwenye mlingoti kamili kwa kipindi cha saa 24 kuanzia saa 13:00 BST siku ya Jumamosi ili kuashiria kutangazwa kwa Charles kama Mfalme, kisha zitarejea nusu mlingoti.
Siku ya Ijumaa, kengele zitalia kwa heshima kwa Malkia huko Westminster Abbey, Kanisa Kuu la St Paul na Windsor Castle. Heshima ya bunduki zitafyatuliwa mara 96 kuashiria kila mwaka wa maisha yake katika Hyde Park na kwingineko.















