Khaled bin Zayed: Je, tunajua nini kuhusu Mwana Mfalme mpya wa Abu Dhabi?

.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Sheikh Khaled alihitimu kutoka Chuo cha Kijeshi cha Sandhurst nchini Uingereza

Siku ya Jumatano, Rais wa UAE, Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan, alimteua mtoto wake wa kiume, Sheikh Khalid bin Mohamed bin Zayed, kuwa Mrithi wa Kifalme wa Imarati ya Abu Dhabi, na pia aliwateua ndugu zake katika nyadhifa nyingine za juu.

Na Shirika la Habari la Emirates lilitangaza uteuzi huo, ambao ni maarufu zaidi katika enzi ya Rais wa Nchi hiyo tangu ashike madaraka Mei 2022, kufuatia kifo cha kaka yake, Sheikh Khalifa bin Zayed Al Nahyan.

Ilijumuisha uteuzi wa Naibu Waziri Mkuu Mansour bin Zayed kuwa Makamu wa Rais wa Nchi, pamoja na Makamu wa Rais wa sasa na Mtawala wa Dubai, Mohammed bin Rashid Al Maktoum, na kuwateua Sheikh Tahnoon na Sheikh Hazza kuwa naibu watawala wa emirate.

Mwanamfalme mpya wa Abu Dhabi ni nani?

Sheikh Khalid bin Mohammed bin Zayed Al Nahyan alizaliwa Januari 8, 1982. Yeye ni mtoto wa kwanza wa Sheikh Mohammed bin Zayed, na mama yake ni Sheikha Salama binti Hamdan Al Nahyan.

Alihitimu kutoka Chuo cha Kijeshi cha Sandhurst nchini Uingereza, na alihudumu katika Huduma ya Usalama ya Serikali.

Aliteuliwa kuwa mkuu wa Vyombo vya Usalama vya nchi, akiwa na cheo cha waziri, kwa amri ya shirikisho mnamo Februari 15, 2016, na kuendelea na wadhifa wake hadi Januari 17, 2017, alipoteuliwa kuwa Naibu Mshauri wa Usalama wa Kitaifa, akiwa na cheo cha waziri.

Sheikh Khaled alikua mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Imarati ya Abu Dhabi, kwa mujibu wa amri ya Emiri iliyotolewa Januari 21, 2019.

Baada ya takriban miezi 9, Sheikh Khaled aliteuliwa kuwa mkuu wa Ofisi ya Mtendaji wa Abu Dhabi, na akawajibikia masuala yote yanayohusu Halmashauri Kuu, ikiwa ni pamoja na masuala yaliyoibuliwa, mipango, maombi, au mipangilio.

Sheikh Khaled pia ni mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Uwekezaji ya Abu Dhabi na Kampuni ya Mafuta ya Emirates (ADNOC).

"Utawala uliotarajiwa"

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Tangu kuanzishwa kwa taifa hilo, ni watawala pekee kutoka Imarati ya Abu Dhabi wameiongoza Emirates, wakati makamu wa rais wamekuwa watawala wa Imarati ya Dubai.

Kwa hiyo, katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, kulikuwa na uvumi mwingi kuhusu uwezekano wa kumteua Sheikh Khaled kama Mwana Mfalme wa Abu Dhabi, hasa kutokana na kuonekana kwake mashuhuri katika mikutano mingi ya kisiasa.

Sheikh Khaled alishiriki katika hafla kadhaa muhimu, alipoonekana na Waziri Mkuu wa Japani Fumio Kishida, mnamo Septemba 26, 2022, wakati akisaini naye makubaliano ya kina ya ushirikiano wa kimkakati kati ya nchi hizo mbili, pembezoni mwa ziara yake ya Tokyo.

Pia aliongoza ujumbe wa UAE ulioshiriki katika sherehe za mazishi ya Waziri Mkuu wa zamani wa Japan, Shinzo Abe, katika mji mkuu, Tokyo, mbele ya viongozi kadhaa wa dunia.

Kuhudhuria kwake kwenye mazishi hayo kulikuwa kustaajabisha, hasa kwa vile nchi za Ghuba zilituma viongozi wao au mawaziri mashuhuri kushiriki katika hafla hiyo.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kuna dhana kwamba Sheikh Khaled atateuliwa kuwa mwana mfalme wa Abu Dhabi, haswa kwa kuzingatia sura yake maarufu katika mikutano mingi ya kisiasa

Mnamo Februari 2023, Sheikh Khaled alisimamia operesheni ya "Gentle Knight" iliyoanzishwa na UAE ili kutoa misaada kwa walioathiriwa na tetemeko la ardhi nchini Uturuki na Syria, kwa kuendesha daraja la kwenye anga la kusafirisha timu za utafutaji na uokoaji, vifaa vya matibabu na misaada muhimu.

Shughuli za Sheikh Khaled zinaonyesha kuwa anajali sana vijana, na pia nyanja za kiuchumi. Hata hivyo, habari kuhusu maisha ya kibinafsi ya Sheikh Khaled, iwe mke wake au watoto, yamesalia kuwa mbali na vyombo vya habari.

Je, ni mamlaka gani ya makamu wa rais wa UAE?

Naibu Waziri Mkuu Mansour bin Zayed aliteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jimbo hilo, pamoja na Makamu wa Rais wa sasa, Mtawala.

Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu ni nafasi ya pili ya juu zaidi katika UAE, akija moja kwa moja baada ya mkuu wa nchi.

Kwa mujibu wa Kifungu cha 51 cha Katiba ya UAE, Baraza Kuu la Shirikisho huchagua Makamu wa Rais wa Nchi kutoka miongoni mwa wanachama wake.

Makamu wa Rais wa Nchi hutumia mamlaka yote ya Mkuu wa Nchi wakati hayupo, kwa mujibu wa Kifungu cha 52 cha Katiba ya UAE.

Muda wa madaraka wa Makamu wa Rais wa Nchi ni miaka 5 ya Gregorian, chini ya kuteuliwa upya, na ikitokea kwamba nafasi ya Rais wa Nchi itakuwa wazi kwa sababu yoyote ile, Makamu wa Rais atatumia mamlaka ya Rais hadi uchaguzi wa Rais mpya.

Imekuwa ni kawaida katika UAE, tangu kuanzishwa kwake, kwa mtawala wa Dubai kuwa makamu wa rais wa nchi na mtawala wa Abu Dhabi kama mkuu wa nchi.

Pia imekuwa ni desturi katika UAE kwa makamu wa rais kuwa waziri mkuu.

Baraza Kuu la Shirikisho ni nini?

Kwa mujibu wa Ibara ya (46) ya Katiba ya Nchi, Baraza Kuu la Shirikisho ndilo lenye mamlaka kuu katika Serikali, kwani Baraza hilo lina watawala wa falme saba, na kila emirate ina kura moja katika mijadala ya Baraza.

Kwa mujibu wa Ibara ya (49), maamuzi ya Baraza Kuu juu ya mambo muhimu hutolewa na wengi wa wajumbe wake watano, mradi kwamba wingi huu ni pamoja na kura za falme za Abu Dhabi na Dubai, na wachache watazingatia maoni ya walio wengi waliotajwa hapo juu. Kuhusu maamuzi ya Baraza juu ya masuala ya kiutaratibu, yanaamuliwa kwa wingi wa kura.

Ibara ya (53) inafafanua kwamba pale nafasi ya rais au naibu wake itakapokuwa wazi kutokana na kifo, kujiuzulu au kusitishwa kwa utawala wa mmoja wao katika ufalme wake kwa sababu yoyote ile, Baraza Kuu litaitwa ndani ya mwezi mmoja wa tarehe hiyo ya kukutana, kumchagua mrithi kuchukua nafasi iliyoachwa wazi kwa muda uliowekwa.

Je, ni changamoto gani zinazoweza kukumbana na mrithi mpya aliyechaguliwa?

Uteuzi wa Sheikh Khalid kama mwana mfalme unaonyesha mwelekeo katika mataifa mengi ya Ghuba ya kutoa kipaumbele kwa watoto wa kiume juu ya ndugu kuhusiana na suala la urithi, ikiwa ni pamoja na Saudi Arabia.

Abu Dhabi imebakia na wadhifa wa rais tangu kuanzishwa kwa UAE na babake Sheikh Mohammed mwaka 1971.

Sheikh Mohammed alikuwa mtawala mkuu wa Emirates kwa miaka mingi kabla ya kushika madaraka baada ya kifo cha kaka yake Mei mwaka jana, wakati ambapo uhusiano kati ya UAE na Marekani ulidorora kutokana na tabia inayoonekana ya Washington ya kujitenga na eneo hilo.

Sheikh Mohammed aliongoza mchakato wa kupanga upya kadi hizo katika Mashariki ya Kati wakati nchi yake na Bahrain zilipoanzisha uhusiano na Israel mwaka 2020 ili kuunda mhimili mpya dhidi ya Iran katika eneo hilo.

Wakati huo huo, UAE iliendelea kushirikiana na Tehran ili kudhibiti mivutano huku ikizingatia vipaumbele vya kiuchumi.

UAE pia imefanya kazi ya kuimarisha uhusiano na Urusi na Uchina.

Nchi hiyo yenye wakazi wasiopungua milioni kumi, inajivunia utulivu wake wa kisiasa na kiuchumi.

Ina mojawapo ya viwango vya juu zaidi vya mapato ya kila mtu ulimwenguni, na inakaribisha mamilioni ya wafanyikazi kutoka nje ambao ndio sehemu kubwa ya wafanyikazi.

Ni kina nani wakuu wa UAE?

  • Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan: Mwana Mfalme wa Abu Dhabi na Naibu Amiri Jeshi Mkuu wa Jeshi.
  • Sheikh Sultan bin Muhammad Al Qasimi: Mwana Mfalme na Naibu Mtawala wa Sharjah.
  • Sheikh Mohammed bin Saud bin Saqr Al Qasimi: Mwana Mfalme wa Ras Al Khaimah.
  • Sheikh Mohammed bin Hamad Al Sharqi: Mwana Mfalme wa Fujairah.
  • Sheikh Rashid bin Saud Al Mualla: Taji Mwana Mfalme wa Umm Al Quwain.
  • Sheikh Ammar bin Humaid Al Nuaimi: Mwana Mfalme wa Ajman.