Ni kawaida kiasi gani kusahau maneno na ni wakati gani utajua limekuwa tatizo?

Chanzo cha picha, getty
Sote tumewahi kupitia hili, wakati wa kuzungumza katikati ya sentensi huwezi kukumbuka neno unalotaka kutumia...
Ni wakati gani ugumu wa kutafuta maneno unaweza kuonyesha kweli kuna tatizo?
Ni kawaida kupata tatizo kama hilo mara kwa mara, lakini ikiwa hutokea mara nyingi mno hasa kusahau majina na nambari, hii inaweza kuwa ishara ya ugonjwa wa neva.
Hatua zinazohitajika kuzungumza
Utamkaji wa neno unahusisha hatua kadhaa na mchakato wake. Hizi ni pamoja na:
- Tambua maana iliyokusudiwa
- Chagua neno sahihi kutoka kwa “leksimu ya kiakili” (kamusi ya kiakili ya msamiati wa mzungumzaji)
- Rejesha muundo wako wa sauti
- Toa matamshi ili kuieleza
Ugumu wa kupata maneno unaweza kutokea katika kila moja ya hatua hizi.
Wakati mzungumzaji mwenye afya hawezi kupata neno akilini mwake, wanasayansi wa lugha huita hali hii "tip-of-the-tongue phenomenon."
Mara nyingi mzungumzaji aliyechanganyikiwa atajaribu kutoa dalili kuhusu maana ya neno analomaanisha... "Unajua, kitu unachotumia kugongea msumari", "kinaanza na N!"
Hili ni jambo la kawaida na ni aina ya hitilafu ya usemi ambayo hutokea hasa wakati wa kurejesha muundo wa sauti.
Ni nini kinachoweza kuathiri utafutaji wa maneno?
Ugumu wa kutafuta maneno hutokea katika umri wote, lakini mara nyingi zaidi tunapozeeka.
Kwa watu wazima, jambo hilo linaweza kusababisha kufadhaika na wasiwasi juu ya uwezekano wa kupata shida ya akili. Lakini sio kwamba ni sababu ya moja kwa moja ya kukutia wasiwasi.

Chanzo cha picha, getty
Njia moja ya kuchunguza tatizo la kutafuta maneno ni kuwataka watu kufuatilia mara kwa mara kusahau kwao na hutokea katika muktadha gani.
Baadhi ya tafiti zimeonyesha kuwa aina ya maneno, kama vile majina ya watu na mahali, nomino hasa (vitu kama vile “mbwa” au “jengo”), na majina ya kujieleza (dhana kama vile “uzuri” au “ukweli”), yana uwezekano mkubwa zaidi kusahaulika ikilinganishwa na vitenzi na vivumishi.
Maneno ambayo hayatumiwi sana pia yana uwezekano mkubwa wa kutokumbukwa.
Hii inadhaniwa kuwa ni kwa sababu yana miunganisho hafifu kati ya maana zao na muundo wa sauti kuliko maneno yanayotumiwa mara kwa mara.
Uchunguzi wa kimaabara pia umeonyesha kuwa kusahau kuna uwezekano mkubwa wa kutokea chini ya hali zenye msongo wa mawazo.
Kwa mfano, wasemaji wanapoambiwa kwamba wanafanyiwa majaribio bila kujali umri wao.
Watu wengi wanaripoti kuwa na matatizo wakati wa mahojiano ya kazi.
Ni kwa kiasi gani inakuwa tatizo?

Chanzo cha picha, getty
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Makosa ya mara kwa mara yanayohusisha maneno, majina, na nambari, yanaweza kuonyesha shida kubwa zaidi.
Hali hii inaitwa "anomia" au "anomic aphasia ," na inaweza kuhusishwa na uharibifu wa ubongo kutokana na viharusi, uvimbe, majeraha ya kichwa, au shida ya akili, kama vile ugonjwa wa Alzeima.
Hivi majuzi, familia ya mwigizaji Bruce Willis ilifichua kwamba aligunduliwa na ugonjwa wa mishipa ya fahamu unaoathiri shughuli nyingi za mwili.
Moja ya dalili za kwanza za hali hii ni ugumu wa kupata maneno badala ya kupoteza kumbukumbu.
Anomic aphasia inaweza kutokana na matatizo ambayo hutokea katika hatua tofauti za utengenezaji wa maneno akilini.
Tathmini ya mwanasaikolojia wa kimatibabu inaweza kusaidia kufafanua ni hatua gani ya uchakataji imeathiriwa na tatizo linaweza kuwa kubwa kiasi gani.
Kwa mfano, ikiwa mtu hawezi kutaja kitu cha kawaida, kama vile nyundo, mwanasaikolojia wa kiafya atamtaka aeleze kitu hicho kinatumika kufanya nini.

Chanzo cha picha, getty
Ikiwa huwezi, utaombwa kuashiria au kuiga jinsi kinavyotumiwa.
Unaweza pia kupewa kidokezo au ujumbe, kama vile herufi ya kwanza (m) au silabi (mar).
Watu wengi wanaoathirika na afasia ya anomic hupata matatizo katika hatua za baadaye za kutoa maneno.
Lakini ikiwa hawawezi kueleza au kuiga matumizi ya kitu na viashiria havisaidii, hii huenda inaonyesha upotevu halisi wa ujuzi au maana ya maneno.
Na kawaida ni ishara ya tatizo kubwa zaidi, kama vile afasia inayoendelea.
Utafiti kwa watu wazima wenye afya njema na watu walio na afasia ya anomia umeonyesha kuwa maeneo mbalimbali ya ubongo yanawajibika kwa matatizo yao ya ugumu wa kutafuta maneno.
Kwa watu wazima wenye afya njema, mapungufu hayo yanahusiana na mabadiliko ya shughuli katika maeneo ya ubongo ambayo hudhibiti hatua ya kutengenezaji na kutoa sauti ya neno, na kupendekeza tatizo la kawaida la kutamka badala ya kupoteza maneno.
Katika ugonjwa wa afasia inayoendelea, maeneo ya ubongo ambayo huchakata maana ya maneno huonyesha upotevu wa seli na miunganisho ya neva.

Chanzo cha picha, getty
Kuna matibabu yanayopatikana kwa ugonjwa wa anomic aphasia.
Wataalamu wa magonjwa ya usemi wanaweza kumfunza mtu huyo kazi za kutaja maneno kwa kutumia aina tofauti za viashiria au vidokezo ili kusaidia kurejesha neno.
Vidokezo vinaweza kuwa na sifa mbalimbali za vitu na mawazo, au sifa za sauti za maneno, au mchanganyiko wa zote mbili.
Programu za simu za smartphone pia huonyesha matumaini zinapotumiwa kusaidia kwenye hatua za matibabu.
Kufanikiwa kwa tiba kunahusishwa na mabadiliko katika shughuli kwenye maeneo ya ubongo yanayofahamika kusaidia utayarishaji wa matamshi.
Kwa bahati mbaya, hakuna matibabu madhubuti kwa aphasia inayoendelea, ingawa tafiti zingine zimependekeza kuwa matibabu ya usemi yanaweza kuleta manufaa ya muda.















