Aiden Aslin: Muingereza wa Ukraine aambiwa kuwa hukumu ya kunyongwa itatekelezwa

Chanzo cha picha, Aiden Aslin
Mwanamume wa Uingereza aliyehukumiwa kifo na mahakama ya uwakilishi ya Urusi kwa kupigana nchini Ukraine ameambiwa kuwa hukumu ya kifo itatekelezwa, familia yake imesema.
Aiden Aslin na Shaun Pinner walihukumiwa na mahakama ambayo haitambuliki kimataifa katika kile kinachoitwa Jamhuri ya Watu wa Donetsk (DPR).
Aslin aliambia familia yake, waliomteka walisema hakukuwa na jaribio lolote la maafisa wa Uingereza kufanya mazungumzo kwa niaba yake.
Waziri wa mambo ya nje alijadili kesi yake na Ukraine mapema mwezi Juni.
Liz Truss alisema yeye na mwenzake wa Ukraine Dmytro Kuleba wamezungumza kuhusu "juhudi za kuhakikisha kuachiliwa kwa wafungwa wa kivita wanaoshikiliwa na washirika wa Urusi" na ametaja hukumu za kifo kuwa "hukumu ya udanganyifu isiyo na uhalali kabisa".
Ofisi ya Mambo ya Nje inajulikana kuwa inachunguza kikamilifu kesi za raia wa Uingereza ambao wamezuiliwa nchini Ukraine na inatoa usaidizi kwa familia za Aslin na Bw Pinner.
Familia ya Aslin ilisema kuwa ilizungumza naye kwa njia ya simu ambapo alisema aliambiwa "muda unazidi kwenda" na watekaji wake.
"Hakuna maneno, hakuna maneno tu, itakuwa habari mbaya zaidi kwa kila mtu, kuwa na mtu wa familia yako kutishiwa kwa njia hii", bibi yake Aslin, Pamela Hall aliambia BBC.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Aiden alikasirika sana alipompigia simu mama yake asubuhi ya leo. Jambo la msingi ni kwamba Aiden amesema DPR imemwambia hakuna mtu kutoka Uingereza ambaye amewasiliana kutoa majibu na kwamba atanyongwa."
"Lazima niamini kile ambacho Aiden ametuambia, kwamba ikiwa DPR haitapata majibu basi watamnyonga. Ni wazi natumai hiyo si kweli."
Aslin na Pinner walihamia Ukraine mwaka wa 2018 na walikuwa wamehudumu kama sehemu ya wanajeshi wa Ukraine kwa miaka kadhaa kabla ya uvamizi wa Urusi.
Wote walikuwa na wenza wa Ukraine na walikuwa wameifanya nchi hiyo kuwa makazi yao. Walitekwa baada ya kukaa wiki wakilinda jiji lililozingirwa la Mariupol.
Lakini mahakama ya wakala wa Urusi iliwaita "mamluki", ikiwashutumu kwa kutumwa kupigana katika mzozo wa kigeni kwa sababu ya pesa.
Walishtakiwa kwa uhalifu ikiwa ni pamoja na kuchukua mamlaka kwa nguvu na kupata mafunzo ya kutekeleza shughuli za kigaidi kulingana na vyombo vya habari vya Urusi RIA Novosti.
Mapema mwezi huu Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky aliwaambia wanafunzi wa Uingereza kwamba kile ambacho Urusi ilikuwa ikiwafanyia wawili hao wa Uingereza ni "kitendo cha kusikitisha" na kusema "hakuwezi kuwa na uhalali wowote wa vitendo hivyo".
Alisema ni "ishara yenye nguvu sana na ya hatari" kwa nchi nyingine kwamba Urusi "inatenda hivi kwa raia wa nchi yoyote".
Serikali ya Uingereza imesema wanapaswa kutendewa kama wafungwa wa kivita chini ya sheria zilizowekwa katika Mikataba ya Geneva.
"Nimelia sana kwa hili, lakini kulia haisaidii, nataka kufanya hivyo lakini sijui nifanye nini.
Bi Hall alisema: "Baada ya simu ya Aiden leo asubuhi ninapaswa kufikiria nini? Sitaki kukata tamaa lakini ni ngumu sana."
"Siwezi kujizuia kufikiria kwamba mawasiliano yanapaswa kufanywa kati ya Uingereza na Urusi."
Lakini vyanzo vya serikali ya Uingereza vinaonyesha kuwa mawaziri kwa sasa hawataki kujadiliana na Urusi moja kwa moja kwa sababu inaweza kuhatarisha kuchochea maelezo ya uwongo ya Urusi kwamba watu hao ni mamluki.
Aslin alikuwa amekaribia kufunga ndoa na mchumba wake raia wa Ukraine ambaye ameenda Uingereza tangu alipokamatwa.
"Angekuwa ameolewa kufikia sasa ni jambo ambalo ningelipenda sana. Nataka aolewe na awe na maisha aliyoyataka," bibi yake alisema.
"Ninajua kwamba Boris Johnson amekuwa Kyiv na alizungumza tena na Rais Zelensky na ninatumai walizungumza juu ya watu hawa."
Katika wiki za hivi karibuni Aslin na Pinner walikejeliwa na watangazaji katika vipindi vya televisheni inayounga mkono Kremlin nchini Urusi, ambavyo vimekuwa vikionyesha video za wanaume hao waliofungwa.

Chanzo cha picha, Alex Tobiassen
Alex Tobiassen, ambaye pia alijiunga na kikosi cha wanamaji wa Ukraine akiwa na Aslin na Pinner, alisema watu hao sasa wanajulikana kama "mashujaa" miongoni mwa wanajeshi wengi wa Ukraine wanaoendelea kupigana.
Alisema hukumu yao ya kifo imewatia nguvu wanajeshi wa Ukraine zaidi.
"Kwa kweli inakusanya watu zaidi nyuma yao," alisema, akizungumza na BBC kutoka Ukraine
"Tuna uhusiano wa kifamilia hapa. Ninapigania marafiki zangu, familia yangu, nyumba yangu na hivi ndivyo Aiden alivyoona.
“Aiden Aslin na Shaun Pinner walikuja hapa kabla ya uvamizi huu kuanza, walijitengenezea maisha katika nchi hii, wakatulia.
"Walijiandikisha jeshini kama askari wa baharini aliye na kandarasi, kama mtu yeyote anayejiandikisha jeshini iwe Uingereza au Marekani.
“Hawa jamaa waliingia ofisini, wakapitia taratibu zao za matibabu, wakapitia mchakato wa kuchunguzwa maisha yao ya nyuma, wakajiandikisha na kula kiapo cha kujitoa, hawa wanaume si mamluki, iko wazi.
"Lakini, kama tunavyoona, Warusi wamepuuza kabisa hilo."

Chanzo cha picha, INSTAGRAM
Kuhusu tishio la hukumu ya kifo kutekelezwa, Tobiassen alisema: "Ni mbaya kabisa, kwa wakati huu ninaimani sana kwamba serikali ya Uingereza pamoja na serikali ya Ukraine itapiga hatua na kutafuta njia fulani ya kujadili kuachiliwa kwao.
"Hiyo ndiyo imani yangu na hicho ndicho ninachoomba."
Maandamano yanapangwa kumuunga mkono Aslin na jumuiya ya Ukraine huko Nottingham mwishoni mwa juma hii.
"Kuna watu wengi huko nje wanaomuunga mkono Aiden na vijana wengine ambao wanazuiliwa," bibi yake alisema
"Ningemwambia Aiden sote tunatuma slamu za upendo na msaada wetu, na kwamba kuna maelfu ya watu ambao wanamuunga mkono yeye na watu wengine.
"Watu wa Newark wamekuwa na msaada mkubwa."















