Kwa nini Putin amekwenda Azerbaijan licha ya kuwa nyumbani kuna 'moto'?

Chanzo cha picha, EPA
Rais wa Urusi Vladimir Putin akiwa Azerbaijan, kwa mujibu wa taarifa rasmi, ziara yake itachukua siku mbili, Agosti 18 na 19. Putin anawasili Baku wakati ambapo mapigano dhidi ya jeshi la Ukraine yanafanyika katika eneo la Urusi, katika eneo la Kursk.
Ikulu ya Kremlin imesema ziara hiyo italenga katika kuendeleza uhusiano wa washirika na wa kimkakati kati ya Azerbaijan na Urusi. Putin pia anatarajiwa kujadili mchakato wa amani kati ya Azerbaijan na Armenia na Rais Ilham Aliyev.
Kwa nini Putin anakuja sasa? Uchambuzi
Kenul Khalilova, Mhariri wa idhaa ya BBC ya BBC Azerbaijan
Hii ni ziara ya kwanza ya Vladimir Putin nchini Azerbaijan tangu aanzishe vita dhidi ya Ukraine miaka miwili iliyopita.
Ziara hiyo pia inakuja wakati Ukraine imevamia ardhi ya Urusi na mapigano yanafanyika nchini Urusi kwenyewe.
Baada ya nchi za Magharibi kumtenga Putin kwa ajili ya kunyakua ardhi ya Ukraine, anatafuta kuimarisha uhusiano wake na washirika na kutafuta mpya.
Alitia saini makubaliano ya muungano na Azerbaijan katika siku ambazo jeshi lake lilivamia eneo la Ukraine.
Ingawa serikali ya Azerbaijan inadumisha uhusiano mzuri na Ukraine na Magharibi, haijawahi kumpa kisogo Putin. Ziara ya sasa ya serikali pia ni fursa kwa kiongozi wa Urusi kuonesha ulimwengu kuwa anaungwa mkono.
Ni vyema kutambua kwamba kabla ya ziara yake nchini Azerbaijan, Putin alifanya ziara za kiserikali nchini Korea Kaskazini na Vietnam.
Suala la gesi
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Baada ya Urusi kuivamia Ukraine na kuweka vikwazo vya Magharibi, Moscow iliacha kusafirisha gesi katika nchi za Ulaya.
Kwa upande wake, Azerbaijan ilitia saini makubaliano na Umoja wa Ulaya na kukubali kuongeza mauzo ya gesi ili kusambaza nchi za Ulaya ambazo hazikuwa na gesi ya Urusi.
Mchambuzi wa kisiasa Fuad Shahbazov anaamini kwamba malengo makuu ya ziara ya sasa ya Vladimir Putin nchini Azerbaijan yanahusiana na masuala ya kiuchumi na, kwanza kabisa, ya nishati.
Kwa maoni yake, hati mpya juu ya usafirishaji wa gesi kati ya Azerbaijan na Urusi inaweza kusainiwa wakati wa ziara hiyo.
"Hati ya ugavi wa gesi ya Kirusi kwa Azerbaijan badala ya kuongeza kiasi cha mauzo ya gesi ya Kiazabajani kwenda Ulaya inaweza kusainiwa. Hiyo ni, gesi ya Kirusi inaweza kutumika kwenye soko la ndani. Aidha, hati kuhusu ushirikiano katika uchumi inaweza kutiwa saini," Fuad Shahbazov anaamini.
Kulingana na Shahbazov, lengo jingine la ziara hii linaweza kuwa kuimarisha msimamo wa Urusi katika mchakato wa amani kati ya Armenia na Azerbaijan.
Anaamini kwamba hivi karibuni taasisi za Magharibi zimejitolea zaidi katika kutatua mzozo kati ya nchi hizo mbili, na Urusi ina nia ya kurejesha ushawishi wake katika eneo la Caucasus Kusini.
"Ziara hii inalenga kuthibitisha nia ya Urusi katika eneo hilo," Shakhbazov alibainisha.
Kuunga mkono makubaliano ya amani
"Upande wa Urusi bado uko tayari kufanya kila kitu katika uwezo wake ili kurejesha uhusiano kati ya Azerbaijan na Armenia," RIA Novosti anaandika, akinukuu Kremlin.
Katika miezi ya hivi karibuni, Azerbaijan na Armenia zimekuwa na mazungumzo ya moja kwa moja juu ya kuweka mipaka na kuhitimisha mkataba wa amani, wakielezea utayari wao wa kutia saini makubaliano ya amani.
Mnamo Agosti, Baku na Yerevan walitupilia mbali kifungu kuhusu njia ya usafiri inayounganisha Azerbaijan na jina lake la Nakhchivan, au "Ukanda wa Zangezur" kama unavyojulikana huko Baku, kutoka kwenye rasimu ya makubaliano ya amani.
Suala hilo liliahirishwa kujadiliwa katika hatua inayofuata ya mazungumzo.
Baku na Moscow walitaka barabara kati ya Azerbaijan na Nakhichevan idhibitiwe na Urusi, lakini Armenia ilipinga hili.
Kutoelewana kati ya Armenia na Urusi kuliibuka baada ya Vita vya Pili vya Karabakh. Rasmi Yerevan hana furaha kwamba Urusi na CSTO hawakutoa msaada wakati wa vita.
Ombi la Armenia kwa nchi za Magharibi kupata silaha na mafunzo ya kijeshi pia lilisababisha kutoridhika nchini Urusi. Rasmi Moscow haikaribishi uwepo wa nchi wanachama wa NATO nchini Armenia.
Mambo haya (pamoja na uadui wa kibinafsi kati ya Putin na Waziri Mkuu wa Armenia Nikol Pashinyan) yamesababisha Urusi na Armenia kutofautiana zaidi katika miaka ya hivi karibuni.
Licha ya ukweli kwamba Urusi na Armenia ni washirika, Vladimir Putin hakwenda huko, kwani Armenia ni mwanachama wa makubaliano ya utekelezaji wa maamuzi ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).
Mnamo Machi 17, 2023, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ilitoa kibali cha kukamatwa kwa Rais wa Urusi Vladimir Putin.
Je, kuna uhusiano kati ya ziara hiyo na Iran?
Muda mfupi kabla ya ziara ya leo ya Rais Vladimir Putin wa Urusi, tarehe 6 Agosti, Katibu wa Baraza la Usalama la Urusi Sergei Shoigu alitembelea Azerbaijan na kukutana na Rais Ilham Aliyev. Njia yake ya kwenda Baku ilipitia Iran.
Sergei Shoigu alitembelea Iran wiki moja baada ya mauaji ya kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh mjini Tehran na kufanya mkutano mjini Baku kabla ya kurejea nyumbani. Katika ziara hiyo, Shoigu alizungumza kuhusu masuala kama vile amani na usalama katika Caucasus Kusini, lakini alitembelea Azerbaijan pekee kutoka eneo hilo.
Weledi wa mambo wanaamini kuwa ziara ya afisa wa ngazi ya juu wa Urusi kwanza mjini Tehran na kisha Baku huenda inahusishwa na mzozo kati ya Iran na Israel.
Kulingana na mchambuzi Fuad Shahbazov, Urusi ina wasiwasi kuhusu uwezekano wa uungwaji mkono wa siri kwa Israel kutoka Azerbaijan katika tukio la mzozo kati ya Iran na Israel.
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga na kuhaririwa na Seif Abdalla












