Steve Rosenberg: Uvamizi wa Ukraine dhidi ya Urusi unatia doa sifa ya Putin kama 'Bw Usalama'

Chanzo cha picha, EPA
- Author, Steve Rosenberg
- Nafasi, Mhariri BBC Russia
- Akiripoti kutoka, Moscow
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Kursk.
Ni moja ya maneno ya kwanza niliyoandika na kuzungumza kama mwandishi wa BBC.
Mnamo 2000, niliripoti juu ya kuzama kwa nyambizi ya Kursk kwenye maji ya barafu ya Bahari ya Barents. Maafisa 118 wanliokuwa wakihidumu katika chombo hicho walifariki.
Vladimir Putin wakati huo alikuwa rais kwa chini ya nusu mwaka. Bado ninakumbuka vituo vya televisheni vya Urusi vikimkosoa kuhusu jinsi alivyoshughulikia maafa.
Wiki hii iliadhimisha miaka 24 tangu K-141 Kursk kuzama. Na, kwa mara nyingine tena, neno Kursk limejaa katika taarifa yangu kutoka Urusi. Wakati huu Mkoa wa Kursk, ambapo wanajeshi wa Ukraine walianzisha uvamizi wao wa kushtukiza na ambapo wamekuwa wakiteka eneo hilo kwa siku tisa sasa.
Neno sawa.
Lakini Urusi ya 2024 ni tofauti sana na Urusi ya mwaka 2000.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mara hii katika televisheni ya Urusi hakuna dokezo la ukosoaji wa Rais Putin; hakuna kutilia shaka maamuzi yake; hakuna kiashiria kwamba ni uvamizi wake wa Ukraine ambao umesababisha matukio haya ya kushangaza. Pia ni vyema kuzingatiwa kuwa, Kremlin imekuwa na robo ya karne ya kudhibiti vikali vyombo vya habari vya Urusi na kutoa ujumbe.
Lakini je, matukio haya yataathiri sifa ya Vladimir Putin?
Ni swali ambalo nimeulizwa mara nyingi zaidi ya miaka miwili na nusu iliyopita:
- Mnamo 2022 wakati Ukraine ilipozamisha meli ya kivita ya Moskva, Meli kubwa ya Urusi katika Bahari Nyeusi
- miezi michache baadaye wanajeshi wa Urusi walipoondoka kaskazini-mashariki mwa Ukraine
- na mnamo 2023 Wagner walipofanya uasi, wakati mamluki wenye silaha walipoandamana kuelekea Moscow - changamoto ya moja kwa moja dhidi ya mamlaka ya Vladimir Putin.
Rais Putin alipitia yote hayo, bila kudhurika. Mara hii huenda pia ana hakika kwamba anaweza kushinda changamoto hii ya hivi punde.
Lakini ikumbukwe kwamba. Maasi ya Wagner yalikwisha ndani ya siku moja.
Mashambulizi ya Ukraine ndani ya Urusi yamekuwa yakiendelea kwa zaidi ya wiki moja. Kadiri yanavyoendelea, ndivyo shinikizo litakavyokuwa kwa uongozi wa Urusi na, ikiwezekana, uharibifu mkubwa kwa mamlaka ya Rais Putin.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Katika miongo miwili na nusu aliyokuwa madarakani, Bw Putin amekuza sifa ya "Bw Usalama", mtu pekee katika nchi hii kubwa mwenye uwezo wa kuwahakikishia Warusi usalama.
Kinachojulikana kama "operesheni maalum ya kijeshi" (uvamizi kamili wa Ukraine) iliwasilishwa kwa watu wa Urusi kama njia ya kuimarisha usalama wa kitaifa wa Urusi.
Miaka miwili na nusu ya vita hivi hakuna na hakuna ishara ya kudumisha "usalama".
Kuna vikosi zaidi vya Nato kwenye mipaka ya Urusi, na Uswidi na Finland zimejiunga na Muungano wa Nato; Miji ya Urusi inakabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya ndege zisizo na rubani za Ukraine; sasa wanajeshi wa Ukraine wanateka eneo la Urusi.
Vladimir Putin anatumia lugha ya busara kujaribu kuonyesha umma wa Urusi kwamba hakuna haja ya kuogopa.
Akizungumzia uvamizi wa Ukraine ameepuka kutumia neno "uvamizi". Badala yake, amezungumzia "hali katika eneo la mpaka" au "matukio yanayofanyika". Kiongozi huyo wa Kremlin pia ameyaita mashambulizi ya Ukraine "uchokozi".
Rais wa Urusi atafanya nini baadaye?
Usitarajia atachukua simu na kupigia Kyiv. Maafisa wa Urusi wameweka wazi kwamba, kufuatia shambulio la Ukraine, wanasitisha wazo la mazungumzo ya amani.
Sio kwamba mazungumzo yoyote makubwa yalikuwa yamepangwa kufanyika.
Wiki hii Vladimir Putin alitangaza nia yake ni nini hasa: "... kumuondoa adui katika ardhi ya Urusi."
Kusema ni jambo moja. Kutenda ni jambo lingine. Licha ya kuimarisha uwepo wake katika eneo la Kursk, jeshi la Urusi bado halijafanikiwa kupata tena udhibiti katika sehemu hii ya Urusi.

Chanzo cha picha, Reuters
Nilipokuwa nikitembea karibu na Kremlin Alhamisi asubuhi, nilisimama na kujionea mwenyewe.
Wafanyikazi walipokuwa wakipanga viti na skrini tayari kwa tukio la moja kwa moja, wimbo wa Edith Piaf Non, je ne regrette rien (Hapana, sijutii lolote) ulikuwa ukicheza kwenye skrini kubwa ya video... kwa sauti kubwa katika Red Square.
Ilikuwa ni wakati kustaajabisha sana.
Vladimir Putin hajaonyesha dalili ya kujutia kuanzisha uvamizi kamili wa Ukraine.
Hajaonesha kujutia uamuzi aliyochukua tangu wakati huo.
Ikiwa matamshi yake ya umma yanaashiria hali yake ya sasa ya akili, bado anaamini kuwa matokeo ya vita hivi ni moja tu: ushindi wa Urusi.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi












