Kwanini wanandoa wa asili tofauti ni maarufu China?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Sylvia Chang
- Nafasi, BBC Hong Kong
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Mwanablogu wa Kichina Laura Deng alishangazwa na jinsi picha za sherehe yake ya kwanza ya Krismasi huko London akiwa na mpenzi wake Muingereza zilivyopokelewa mtandaoni. Hakutarajia alipoamua kuzishiriki kwenye Xiaohongshu, mtandao wa kijamii wa Kichina ambao ni sawa na Instagram, miaka mitatu iliyopita.
Mbali na selfie ya wanandoa, chapisho hilo lilijumuisha picha za zawadi, mti wa Krismasi, na meza ya sherehe iliyofunikwa kwa zawadi za Krismasi. Chapisho hilo liliwavutia watu wengi kuliko machapisho yake ya kawaida ya mitindo na urembo, na kumletea mamia ya wafuasi wapya.
Tangu wakati huo, Deng mwenye umri wa miaka 29 amebadilisha mkakati wake wa mitandao ya kijamii na kuanza kushiriki maudhui kuhusu uhusiano wake, akiangazia tofauti za kitamaduni kati yake na mpenzi wake.
Wafuasi wake wameongezeka kutoka 1,000 hadi zaidi ya 80,000, katika hatua iliyomuwezesha kutia saini kandarasi za utangazaji zinazompatia mapato ya ziada ya kila mwezi ya yuan 3,000 hadi 70,000 swawa na dola 400 hadi 9,800 za Kimarekani.
Baada ya zaidi ya watu 10,000 kuanza kumfuatilia mtandaoni, mashirika ya ushawishi yalianza kumtafuta. Sasa ana timu ya watu wanne wanaoshughulikia mambo tofauti, kama vile kuhariri video, kudhibiti utangazaji wa kibiashara, na kuandaa mikakati ya kukuza hadhira yake.
Laura Deng na Charles Thomas ni miongoni mwa mamia, kama si maelfu, ya wanandoa wenye asili tofauti wanaopata umaarufu mtandaoni nchini China. Mara nyingi, mshirika wa kigeni ni mzungu, na watu wanaofuata akaunti hizi ni wanawake vijana wanaoishi katika sehemu tajiri zaidi za China.
Ndivyo ilivyo kwa TJandClaire, akaunti inayoendeshwa na mwanamke wa Shanghai na mumewe Mmarekani, ambayo imepata wafuasi zaidi ya milioni 3.8 kwenye Douyin, toleo la Kichina la TikTok. Asilimia 60 kati yao ni wanawake wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi 30, kulingana na kampuni ya uchanganuzi wa data ya Chan Mama.
Ndoto na kutoridhika

Chanzo cha picha, Getty Images
Deng alitangaza kuchumbiana na Charles Thomas mnamo Mei, na mashabiki wengi walimpongeza na kumtakia kila la heri. "Nimekuwa nikifuatilia hadithi yako kwa muda mrefu, hatimaye tutaiona siku yako kuu!" mmoja aliandika.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Kwa baadhi wa wasichana, kuona uhusiano wa kimapenzi kati ya watu wa wenye asili tofauti katika mitandao ya kijamii ni kama kusoma riwaya ya mapenzi ya kidijitali. Inatimiza mawazo yao kuhusu ndoa, lakini pia inaonyesha kwamba hawajaridhishwa na ukweli," anasema Li Chen, msomi wa vyombo vya habari katika Chuo kikuu cha Texas A&M.
China bado ni jamii ya kitamaduni. Wanawake wanatarajiwa kufanya kazi za nyumbani na malezi ya watoto; ubaguzi wa mahali pa kazi ni jambo la kawaida, na hakujakuwa na mabadiliko ya sheria katika miaka ya hivi karibuni.
Wanawake wengi hususan vijana wa China wanakataa majukumu ya kitamaduni ya kijinsia, licha ya shinikizo la serikali kwao kuolewa na kupata watoto kutokana na kushuka kwa viwango vya uzazi. Mnamo 2023, idadi ya watu wa China ilipungua kwa mwaka wa pili mfululizo, hadi bilioni 1.409, kutoka milioni 2.08 mwaka uliopita.
Wafuasi wengi wa akaunti hizi wanadhani kuwa mahusiano katika mahusiano au na wanandoa wa mataifa ya Magharibi ni ya usawa zaidi, mtazamo ambao huenda isiwe hivyo . "Wanaume wa Magharibi huwa na mwelekeo wa familia zaidi kuliko wanaume Wachina," alisema mtu mmoja aliyefuatilia akaunti ya Laura Deng.
Qian Huang, profesa msaidizi wa masomo ya vyombo vya habari katika Chuo Kikuu cha Groningen nchini Uholanzi, anakubali kwamba mwelekeo huo unaweza kuonyesha kuongezeka kwa ufeministi nchini China, hasa miongoni mwa makundi ya watu wenye kipato cha kati na cha juu.
Anabainisha kuwa washawishi wanaokuza useja pia wanazidi kuwa maarufu.
Fahari ya Uchina

Chanzo cha picha, Getty Images
Ni jambo la kawaida kwa akaunti zinazotolewa kwa wanandoa wa rangi tofauti kuonyesha mtu wa Magharibi akifurahia chakula cha Kichina, kuimba Mandarin, kutembelea vivutio vya utalii nchini China, au kuchunguza teknolojia ya hali ya juu ya Kichina.
Video ya Charles Thomas akiwa amevalia mavazi ya kitamaduni ya Kichina na akipita Leicester Square huko London ilikuwa mojawapo ya maudhui yaliyowavutia wafausi wengi kwenye mtandao wa Xiaohongshu wa Laura Deng.
Aina hii ya maudhui hutofautiana na video zilizochapishwa na wageni wanaoiunga mkono serikali ya China, ambao mara nyingi huagazia maisha yao ya kila siku nchini China na kueleza kuunga mkono msimamo wa Beijing kuhusu masuala yenye utata, kama vile mzozo na jamii ya wachache ya Uighur katika eneo la Sinkiang. Washawishi waliojitolea kwa wanandoa wa rangi tofauti mara chache hushughulikia masuala ya kisiasa.
Bi Deng, ambaye ameishi nchini Uingereza kwa miaka 10, anasema ni kawaida kuonyesha utamaduni wake kwa mpenzi wake na familia. "Ninatarajia kuwaonyesha ubora wa China," anasema, akiongeza kuwa mitazamo ya mataifa ya Magharibi kuhusu nchi yake inachangiwa na utangazaji mbaya wa vyombo vya habari.
Anakumbuka wazazi wa mpenzi wake walivutiwa walizuru China kwa mara ya kwanza, akisema: "Mambo mengi hapa ni bora zaidi kuliko Uingereza."

Chanzo cha picha, Getty Images
Mtandao umedhibitiwa sana nchini China, ikimaanisha kuwa washawishi wanaozungumza kuhusu wanandoa wa rangi tofauti "wanalingana na ajenda ya serikali," anasema Dk. Chen. "Huenda wasichochewe na utaifa, lakini wanaweza kuchuma mapato," anasema.
Hata hivyo, utaifa unaweza kuwa msumeno unaokata mbele na nyuma.
Wendy, ambaye hakutaka kutaja jina lake la ukoo, anaishi Ulaya na mchumba wake Mfaransa. Ana karibu wafuasi 20,000 kwenye Xiaohongshu, ingawa yeye huepuka kutumia lebo kama vile "wanandoa wa rangi tofauti" au "wapenzi wa kitamaduni." Machapisho yanayoangazia mchumba wake huvutia watu wengi zaidi kuliko mengine.
Lakini pia anapokea maoni kadhaa ya chuki na ubaguzi wa rangi. Katika matukio kadhaa, ameshutumiwa kuwa “kibaraka wa mataifa ya Magharibi” au hata mpelelezi. Mashambulizi haya yamesababisha akaunti zake kufungwa kwa mara tatu.
Msichana huyo mwenye umri wa miaka 28 pia amepokea ofa za kushirikiana na chapa mbalimbali, lakini alihisi kutoridhika na mitazamo isiyo ya kweli ya maudhui yaliyofadhiliwa yanayotolewa. "Wanataka uifanye iwe ya kimapenzi iwezekanavyo," anasema.
Anaeleza kuwa hayakuwa aina ya maudhui ambayo alitaka kushiriki mwanzoni na kwamba yaliishia kuharibu uhusiano wake na mchumba wake. Mwaka huu, alikataa kila mpango wa udhamini aliopewa.
"Nataka tu kuwa mwaminifu kwangu na kuangazia nyakati za furaha.
Laura Deng ameshutumiwa kwa kutumia hisia za utaifa kujitangaza. Lakini anasisitiza kuwa haelewi lolote kuhusu siasa na kwamba maudhui yake yanatokana na hisia na uzoefu wake binafsi.
"Watu wanapenda kuona jinsi sisi Wachina tunavyoonyesha fahari utamaduni wetu kwa wengine," anasema. "Sijali wanachosema kuhusu mwangwi wa sera za serikali. Ikinivutia nitachapisha, nitaendelea kufanya hivyo,” anamalizia.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi












