Hata uwe tajiri vipi,usiwahi kuonyesha hilo nchini China -Lakini kwanini?

China

Chanzo cha picha, Getty Images

Je yuan 650 sawa na dola 101 za Marekani zinatosha kununua chakula cha siku moja?

Hapana, sio kweli kulingana na Su Mang, aliyekuwa mhariri mkuu wa kampuni ya Harper Bazaar China, ambaye maoni yake katika kipindi cha televisheni cha moja kwa moja yalisababisha hasira miongoni mwa watumiaji wa mitandao ya kijamii.

"Lazima tule vizuri, siwezi kula vyakula vivi hivi tu," aliongeza wakati anazungumza katika kipindi hicho chenye watu maaarufu 15 wanaoishi pamoja kwa siku 21.

Wakiwa wamekasirishwa na maoni yake, wananchi walisema kuwa pesa za chakula chao cha mchana kawaida ni chini ya yuan 30.

Ingawa Bi. Su, ameelezea kwamba watu walikosa "kumuelewa" - yuan 650 ilikuwa ni za muda wote watakaokuwa kwenye kipindi, - lakini bado umma haukuridhika na jibu lake.

"Alijaribu kuelezea, lakini ukweli ni kwamba watu mashuhuri huwa wanajionea fahari bila wao kujua," mtu mmoja aliandika kwenye jukwaa la mtandao wa Weibo.

Kisa chake ndio cha hivi karibuni zaidi kusababisha hasira miongoni mwa umma kwasababu tu wanajiona ni matajiri.

Su Mang is the former editor of high-end magazine Harper's Bazaar China

Chanzo cha picha, Getty Images

Mapema mwaka huu, Annabel Yao, msichana mdogo wa Huawei mwanzilishi wa Ren Zhengfei, alisababisha hasira kwenye intaneti aliposema kwamba ameishi maisha magumu sana.

"Sijawahi kujitunza kama yule anayeitwa 'princess'... Nafikiri mimi ni kama wengine wengi tu wa umri wangu, nililazimika kufanyakazi kwa bidii hasa, kusoma kwa bidii kabla ya kujiunga na shule nzuri," alisema hivyo katika video iliyorekodiwa dakika 17 akitangaza taaluma yake ya kuimba.

Lakini alipoweka video hiyo katika akaunti yake ya Weibo na kushirikisha wengine, ambaye baba yake inasemekana kwamba utajiri wake unakadiriwa kuwa dola bilioni 1.4, alisema kuwa kufikia makubaliano na kampuni ya muziki ilikuwa ni "zawadi ya kipekee siku yake ya kuzaliwa" aliyojitunuku.

'Hastahili'

Kwa miaka mingi, matajiri nchini China wamekuwa wakifahamika kwa kujifaharisha. Wakionesha magari yao ya kifahari na mikoba yao kwenye mitandao.

Lakini taratibu, tabia ya kuonesha mali au utajiri - ama kwa kukusudia au vyinginevyo - huwa ni kujitengenezea uhasama na kudharauliwa.

Watu kama Bi. Su na Bi. Yao wanalengwa kwasababu wengi wanaamini kuwa watu mashuhuri na kizazi cha pili ambacho ni matajiri yaani watoto - hawastahili kupata mapato ya juu.

"Ukilinganisha kuwa wao ni nyota na kuonekana kuwa rahisi kwao kupata 'kazi', watu watalalamika kuhusu vile wanavyofanya kazi kwa kutumia nguvu nyingi na kwa bidi hasa na mapato ya chini wanayopata," amesema Dkt. Jian Xu wa chuo kikuu cha Deakin, mtafiti wa utamaduni wa vyombo vya habari China.

Dkt. Haiqing Yu, profesa wa Chuo kikuu cha RMIT huko Melbourne, aliongeza kuwa "matamashi ya Su Mang kuhusu chakula chake yalisababisha hasira miongoni wa watu kwasababu yanaonesha kile ambacho China inajaribu kuficha" - kwamba baadhi ya watu ni matajiri sana, huku wengine wakiwa hawana kitu.

China, pengo kati ya matajiri na maskini ni kubwa mno

Wakati kipato cha wastani kwa mwaka nchini humo ni yuan 32,189 au dola 5,030 au sawa na yuan 2,682 kwa mwezi, kulingana na Takwimu za Taifa, pia Beijing imekuwa kitovu cha mabilionea wengi kuliko mji mwingine wowote ule duniani.

Kulingana na ripoti ya Hurun inayofuatilia utajiri wa watu, wanaorodheshwa kuwa matajiri China, rekodi yao ya mapato ilifikia dola trilioni 1.5 mwaka 2020, kiwango ambacho ni takriba nusu ya pato la taifa la Uingereza.

Na kwa mtajiri kuonesha waziwazi mali zao inaonekana kama hatua isiyokubalika katika jamii.

Wakati tabia hii ni maarufu sana kwa mataifa mengi yenye tatizo la ukosefu wa usawa wa mapato, China inaonekana kuchukua mkondo mwingine, wataalamu wanasema

Kwa kipindi kirefu, watu walikuwa wakifikiria kuwa wanaweza kufikia kiwango cha "ustawi kwa kila mmoja" - hatua ambayo aliyekuwa kiongozi maarufu Deng Xiaoping alisema hilo ndilo litakuwa lengo hata kama itamaanisha baadhi ya watu na dini kuanza wao kuwa matajiri.

"Lakini baada ya miaka 40 tangu nchi hiyo kuanza kufungua milango yake, watu matajiri wameendelea kuwa matajiri, huku wengine wakisazwa nyuma, na kuongeza pengo kati yao na maskini huku wengine wakiwa wanahisi kukata tamaa na kutokuwa na nguvu," Dkt. Xu amesema.

Wakati mwingine hasira huongezeka zaidi kwasababu ya kile alichokiita "matarajio kuwa watu mashuhuri wanastahili kuchangia zaidi (katika jamii) kwasababu wanajulikana na umma na pia wanaonekana kama nembo inayoashiria nguvu".

Kwa mfano mwezi uliopita, kulikuwa na hasira baada ya kubainika kwamba mwigizaji wa kike Zheng Shuang analipwa karibu yuan milioni 2 kwa siku kwa kipindi chake kwenye televisheni, ikiwa ni jumla ya yuan milioni 160 kwa mradi wote.

"Mtu kulipwa yuan milioni 160 ina maanisha nini? Mfanyakazi wa kawaida anayelipwa yuan 6,000 kwa mwezi anahitajika kufanyakazi kwa miaka 2,222 mfululizo…," tu mmoja aliandika katika mtandao wa Weibo.

Actress Zheng Shuang was criticised for her high wage

Chanzo cha picha, Getty Images

Lakini raia walikuwa na hasira hata zaidi kwasababu Bi. Zheng alikuwa katikati ya suala lililozua utata. Mapema mwaka huu, alijipata katika gumzo tata lililohusu kubeba mimba kwa ajili ya kumzalia mwanamke mwengine ambalo chini China ni kinyume cha sheria - baada ya kudaiwa kuwa ametelekeza watoto wake wawili waliozaliwa kwa njia hiyo nje ya nchi hiyo.

Kwa mtu kupokea kiasi hicho cha pesa na hachukuliwi kuwa mfano mzuri katika jamii bila shaka kwa raia ni tatizo kubwa.

Hii ndio sababu mwaka 2018, pia watu hawakuwa na huruma na mwigizaji wa kike maarufu anayejulikana kwa jina Fan Bingbing alipowekewa kifungo cha nyumbani kwa kukwepa kulipa kodi, hata ingawa alikuwa nyota nchini humo.

Kujifaharisha lakini ukajifanya kuwa mnyenyekevu

Kutojihusisha na kujifaharisha pia kunahusishwa na dhana kuwa ni ishara ya ukosefu wa utamaduni, wataalamu wanasema.

Kwa kuwa tabaka la wastani la China limeongezeka, wasomi wa mijini wanafasiri kujishauwa kwa utajiri "kama ukosefu wa usasa yaani 'ushamba' au kuwa na asili ya 'tabaka la chini," Dkt. John Osburg, mwandishi mmoja wa vitabu amezungumza na BBC.

Hata hivyo, licha ya hayo yote bado hamu ya kuwa na vitu vya kifahari haitoondoka hivi karibuni.

Kulingana na utafiti uliofanywa kimataifa, China imeipiku Japan kama nchi yenye soko la vitu binafsi vya kifahari eneo la Asia Pasifik na inatarajiwa kuwa na mauzo ya juu baada ya janga la corona kufikia mwishoni mwa wiki.

China has surpassed Japan as Asia Pacific's leading personal luxury market

Chanzo cha picha, Google

Cha msingi, ni kwa matajiri kuwa na uwezo wa kuonesha kwamba hawajishauwi - yaani waonesho mafanikio yao lakini kwa njia ambayo sio kuonesha fahari kwa wengine.

Dr Yu alielezea vile kwa baadhi wameamua kubadilisha namna ya kuonesha utajiri wao. "Baadhi ya matajiri sasa wanajaribu kuonesha walicho nacho kwa kujificha au njia ya ustaarabu wala sio kuweka picha za mali yao mitandaoni," alisema.

Kwa mfano, mshawishi mmoja, MengQiqi77 - aliyetambulika kwa kujifaharisha kwa maisha yake ya kifahari - kuna wakati "alilalamika" katika mtandao wa Weibo kwamba hakuna vituo vya kutosha vya magari yanayotumia umeme katika eneo jirani. "Kwahiyo, hatukuwa na namna zaidi ya kuhamia nyumba kubwa yenye gereji ya kibinafsi kwa ajili ya gari la mume wangu aina ya Tesla," aliandika.

Ingawa pia, haikuchukua muda mrefu kabla ya ujumbe kama huo anaoweka mitandaoni pia nao kuanza kukera watu na kuzua gumzo huku wakosoaji wake wakikejeli ujumbe anaoweka na hata kumpachika jina.