Shell yapuuzilia mbali onyo kuhusu udanganyifu katika usafishaji wa mafuta, chanzo chaiambia BBC

..

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 8

Uchunguzi wa BBC umebaini madai kwamba kampuni kubwa ya mafuta Shell imepuuza onyo la mara kwa mara kuhusu operesheni ya kusafisha maeneo ya mafuta ya kusini mwa Nigeria, ambayo inashutumiwa, imekuwa na matatizo na rushwa.

Kampuni hiyo ya kimataifa yenye makao yake London, pamoja na serikali ya Nigeria, mara kwa mara imesema kwamba kazi ya kusafisha maeneo yaliyoathiriwa na mafuta ya Ogoniland, ambayo ilianza takriban miaka nane iliyopita, inaendelea vizuri.

Lakini BBC imegundua ushahidi kwamba walionywa mara kwa mara kwa miaka kadhaa kwamba mpango huo, ulioanzishwa na serikali na kufadhiliwa na makampuni mbalimbali ya mafuta kwa kiasi cha $1bn (£805m), umekumbwa na matatizo kadhaa.

Mtaalamu mmoja aliye karibu na wachunguzi ameelezea mradi huo wa kusafisha kama "udanganyifu" na "hila" ambayo imetumia fedha bure na kuacha watu wa Ogoniland katika eneo la Niger Delta wakiishi na athari mbaya za uchafu wa mafuta - miaka 13 baada ya ripoti ya kihistoria ya Umoja wa Mataifa kufichua hali mbaya ya eneo hilo.

Shell iliiambia BBC: "Mazingira ya kufanya kazi katika eneo la Niger Delta bado ni changamoto kutokana na kiwango kikubwa cha shughuli haramu kama wizi wa mafuta."

"Matukio ya kuvuja yanapotokea kwenye miundombinu yetu, tunasafisha na kurekebisha, bila kujali chanzo. Ikiwa ni kuvuja kwa sababu ya shughuli za uendeshaji, pia tunalipa fidia kwa watu na jamii."

"Madai ya Shell yanakuja wakati ambapo kesi ya kiraia inatarajiwa kuanza Alhamisi katika Mahakama Kuu ya London, ambapo mawakili wanaowakilisha jamii mbili za Ogoniland zenye wakazi takriban 50,000 watasema kwamba Shell lazima iwajibike kwa uchafuzi wa mafuta uliofanyika kati ya 1989 na 2020, kwa madai kwamba ulitokana na miundombinu yake.

Jamii hizo zinasema kwamba uvujaji huo umeharibu vyanzo vya maji safi, hawana uwezo wa kulima na kuvua, na kuleta hatari kubwa kwa afya ya umma.

Shell, ambayo imekuwa ikipambana kuuza mali zake katika taifa hilo la Afrika magharibi ili kujikita katika uchimbaji mafuta baharini na gesi ya ardhini, imeonyesha kuwa itajitetea dhidi ya madai hayo.

Inakanusha madai hayo na inasema kwamba uvujaji katika eneo hilo umesababishwa na uharibifu, wizi na usafishaji haramu wa mafuta ambapo kampuni hiyo inasema haihusiki.

BBC imeitembelea maeneo yaliyoathiriwa katika jimbo la Niger Delta, ambapo Shell, kampuni kubwa ya mafuta na gesi binafsi nchini humo, iligundua kuwepo kwa mafuta ghafi miaka 68 iliyopita.

UN inasema kwamba angalau mapipa milioni 13 ya mafuta ghafi - au tani milioni 1.5 - yamevuja tangu 1958 katika matukio zaidi ya 7,000 katika eneo la Delta ya Niger.

Uvujaji huo umehatarisha afya na maisha ya familia nyingi.

Unaweza pia kusoma
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Grace Audi, 37, anaishi na mpenzi wake na mtoto wao wa miaka miwili huko Ogale, ambapo kumekuwa na angalau matukio 40 ya uvujaji wa mafuta kutokana na miundombinu ya Shell, kulingana na Leigh Day, kampuni ya sheria ya Uingereza inayowakilisha jamii katika kesi hii.

Familia yake na majirani zake wanapata maji ya visima yaliyo na uchafu, na kulazimika kununua maji safi kwa matumizi ya kunywa, kupika, kufanya usafi, na mara moja kwa siku kwa ajili ya shughuli nyingine, kwa gharama ya Naira 4,500 za Nigeria ($3, £2.40) - katika eneo ambako mshahara wa wastani wa kila siku ni chini ya $8.

Hii ni simulizi inayojulikana kwa wengi huko Ogoniland.

Paulina Agbekpekpe aliiambia BBC kuwa kijani kibichi kilikuwa kimezunguka mikoko katika maeneo ya wakazi wa Bodo - ambao sio miongoni mwa wale wanaokwenda mahakamani Alhamisi.

Alisema mito na mabwawa yalikuwa na wingi wa wanyama na samaki.

"Mahali palikuwa na kijani kibichi, sio mikoko pekee, bali kila mahali kwenye pwani - kulikuwa na miti ya mipapai, michikichi na zaidi. Lakini wakati wa uvujaji wa mafuta, uharibifu umekuwa kila mahali," alisema mama huyu wa watoto sita mwenye umri wa miaka 50.

Familia yake imejishughulisha na uvuvi kwa vizazi, hadi uvujaji mbaya wa mafuta ulipotokea miaka kumi iliyopita.

"Wengi wa watoto - kutokana na maji hayo ya kunywa - wamepata magonjwa. Wengi wamekufa. Nimepoteza watoto wanane. Mume wangu ni mgonjwa.

"Kwa sababu ya kupoteza vipato vyetu, watu wa Bodo wanateseka na njaa."

Mnamo 2011, Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa (UNEP) ulifanya utafiti mkubwa kuhusu athari za uchafu katika eneo hilo lenye mafuta.

Iligundua kuwa wanajamii wa moja ya jamii huko Ogoniland walikuwa wanakunywa maji yaliyochafuliwa na kemikali inayojulikana kusababisha satarani kwa viwango zaidi ya mara 900 juu ya mwongozo wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO). Kemikali hiyo hiyo, benzini, iligundulika katika sampuli zote za hewa.

Iligundua pia kwamba maeneo ambayo tawi la Shell la Nigeria, Shell Petroleum Development Company of Nigeria (SPDC), lilidai kuwa yamerejeshwa, bado yalikuwa yamechafuliwa na mbinu walizotumia hazikufikia viwango vya udhibiti.

Ripoti hiyo ilihitimisha kuwa usafishaji kamili wa eneo hilo ungechukua miaka 25-30 - na ilisababisha kuundwa kwa Mradi wa Usafishaji wa Hidrokarboni (Hyprep).

Huu ulianzishwa awali na serikali ya Nigeria mwaka 2012, lakini hakuna usafishaji ulioanza - hadi ulipoanzishwa tena na serikali mpya mnamo Desemba 2016.

Hyprep ilifadhiliwa na sehemu ya makampuni ya mafuta ikiwemo kampuni ya serikali ya Nigeria National Petroleum Company (NNPC) na Shell, ambayo ilitoa $350m.

...
Maelezo ya picha, Wavuvi walionesha BBC kuwa mafuta yapo katika vyanzo vya maji vya Ogoniland

Hata hivyo, BBC imeona nyaraka za ndani zinazodai kwamba wawakilishi wa Shell na serikali ya Nigeria waliondolewa mara nyingi kuhusu madai ya udanganyifu yanayohusiana na miradi ya shirika hilo.

Mtu mmoja aliyetambua kuhusu mradi huo alizungumza na BBC kuhusu wasiwasi wao - na alitaka kutotajwa jina kwa kuhofia usalama wake.

"Inajulikana kwamba kile tunachofanya kwa kweli ni udanganyifu. Sehemu kubwa yake ni kuwadanganya watu wa Ogoni," alisema mtoa siri huyo.

"Ni udanganyifu unaoendelea ili pesa zaidi ziingizwe kwenye mfuko na kuishia mikononi mwa wanasiasa na watu wengine wenye nguvu."

Madai kuhusu kushindwa kwa Hyprep ni pamoja na:

  • Mikataba ikitolewa kwa kampuni ambazo hazikuwa na uzoefu unaofaa
  • Matokeo ya kimaabara yameghushiwa - wakati mwingine kutaja udongo na maji yaliyochafuliwa kuwa safi
  • Gharama za mradi zikiongezwa
  • Wakaguzi wa nje wakati fulani wakizuiwa kukagua usafishaji kwenye tovuti ulifanyika ipasavyo.

Katika kumbukumbu za kikao kilichofanyika mwaka 2023, kilichohudhuriwa na wawakilishi kutoka tawi la Shell la Nigeria, UNEP na Hyprep, ilibainika kwamba "wataalamu wasio na uwezo" walikuwa "wanahusika tena" na walionyeshwa kuwa hawapaswi "kuruhusiwa kuendelea kuharibu mazingira".

Katika ripoti nyingine iliyovuja na kuonwa na BBC mwaka huo huo, ilibainika kwamba matokeo ya maabara "yaliripotiwa mara kwa mara na kutofautiana".

Mnamo 2022, Umoja wa Mataifa uliandika barua kwa wizara ya mazingira ya Nigeria, ukionya kuwa kama hakuna mabadiliko, "viwango vibaya sana" vya usafishaji vitaendelea.

BBC imewaomba Hyprep na serikali ya Nigeria kutoa maoni kuhusu madai hayo lakini haijapata jibu.

Lakini uchunguzi wetu umebaini ushahidi kwamba Shell ilikuwa inafahamu kuhusu matatizo hayo.

Katika kikao na kamishna mkuu wa Uingereza nchini Nigeria Januari mwaka jana, kumbukumbu za kikao hicho zilizopatikana chini ya Sheria ya Uhuru wa Habari, wawakilishi wa Shell walikiri "changamoto za kitaasisi" katika shirika la usafishaji na kuna uwezekano wa kunyimwa ufadhili baadaye".

Shell iliiambia BBC: "Hyprep ni shirika lililoanzishwa na linaangaliwa na serikali kuu ya Nigeria, na baraza lake la uongozi linajumuisha wakuu wa wizara na maafisa wa serikali, pamoja na wawakilishi watano wa jamii na mashirika yasiyo ya kiserikali, na mwakilishi mmoja wa Shell."

..

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, UN ilionya mnamo 2011 inaweza kuchukua hadi miaka 30 kusafisha uchafu wa mafuta huko Ogoniland.

Huu siyo mradi pekee wa urejeshaji katika eneo la Ogoniland ambao unadaiwa kuwa umeharibiwa.

Mnamo 2015, Shell iliingia makubaliano ya £55m kwa ajili ya usafishaji baada kutokea mara mbili uvujaji mkubwa za mafuta mwaka 2008 katika miundombinu yake katika eneo la Bodo.

Kampuni ilisema kuwa usafishaji huo, uliofanywa na Bodo Mediation Initiative (BMI), ambayo inakusudia kuwa mpatanishi kati ya makampuni ya mafuta, ikiwemo Shell, na jamii ya Bodo (na ambayo inafadhiliwa kwa sehemu na kampuni ya mafuta na wadhibiti wa Nigeria), imeidhinishwa kama asilimia 98% imekamilika.

Hata hivyo, BBC ilitembelea maeneo ndani ya eneo hilo na kugundua mafuta ghafi yanatoka kwenye ardhi na kujaa juu ya maji.

Shell na BMI wanasisitiza kuwa matukio yoyote ya uvujaji wa mafuta katika eneo hilo ni kwa sababu ya wizi - unaojulikana katika sekta hii kama "wizi wa mafuta".

"Kuna mpango wa kuwaita wataalamu kurudi kusafisha maeneo hayo kwa mujibu wa vigezo, kwa kiwango kinachohitajika," Boniface Dumpe, mkurugenzi katika BMI, aliambia BBC.

"Ni jukumu la wahusika wote,ikiwemo Shell, kuhakikisha kwamba miundombinu yao inatunzwa, na kuhakikisha kuwa uvujaji wa mafuta haujirudii kwenye miundombinu yao.

"Lakini kwa maeneo ambayo tayari yamesafishwa. Ningefikiri kwamba pia kuna jukumu kwa jamii kuhakikisha kwamba shughuli haramu hazisababishi tena uchafuzi."

Shell ilisema inachukua hatua madhubuti ili kuzuia uvujaji wa mafuta unaosababishwa na wizi wa mafuta.

Kampuni hiyo ilisema: "Tunachukua hatua madhubuti ili kuzuia shughuli hii na uvujaji unaosababishwa nayo, ikiwa ni pamoja na uangalizi wa anga, kuondoa uungaji haramu wa vifaa kwenye mabomba, na kujenga kizuizi cha chuma kulinda mifuniko ya visima."

Madai ya kushindwa kwa usafishaji wa mafuta yanakuja wakati Shell inajiandaa kuuza tawi lake la Nigeria, SPDC, kwa Renaissance Africa, shirikisho la makampuni ya ndani na ya kimataifa.

..
Maelezo ya picha, Subira Ogboe anasema alipanda zao hili la mahindi miezi minne iliyopita lakini halistawi ipasavyo

Baadhi ya wakazi wa Ogoniland wameshutumu kampuni hiyo ya mafuta kwa "kukimbia" jukumu hilo la kusafisha ardhi na maji kwa usahihi ambayo yanadaiwa kuchafuliwa.

Wanahofu pia kuwa Shell huenda bado itafaidika na eneo hilo kwa kuuza mafuta yatakayochimbwa kutoka katika eneo hilo baadaye.

"Shughuli zozote zinazohusu mafuta katika mabomba husika zitakuwa na athari kubwa kwa maisha yao ya kila siku," Joe Snape, wakili kutoka Leigh Day, aliambia BBC.

"Kuna maelezo kidogo sana kuhusu matokeo ya mikataba hii.

"Hakujulikani jinsi shirikisho la Renaissance [Africa] itakavyofanya kazi. Angalau kwa kampuni ya Shell tunayo namna ya kuwawajibisha."

Bidhaa za uchimbaji, kama vile mafuta ya petroli na gesi,ni 90% ya bidhaa zinazosafirishwa nje ya Nigeria, nyingi zikitokea katika eneo la Niger Delta.

Wakazi, ambao chanzo chao kikuu cha kipato kilikuwa kilimo na uvuvi, waliiambia BBC kuwa tangu kugunduliwa kwa mafuta, au kile ambacho wengine wanakiita "dhahabu myeusi", nyumbani kwao kumekuwa kukichimbwa kwa kuwanufaisha makampuni makubwa ya mafuta, wezi wa mafuta na wanasiasa mafisadi.

Wanasema hawajapata faida yoyote, bali mateso - kama vile Patience Ogboe ambaye anashutumu uvujaji wa mafuta wa hivi karibuni uliharibu mazao yake.

"Hapo kabla, nilipovuna, nilikuwa naweza kula baadhi na familia yangu na hata kuuza baadhi… lakini kwa miaka michache iliyopita sikupata kitu chochote. Ni mbaya sana," aliiambia BBC mkazi huyo mwenye umri wa miaka 42.

...