Mvutano wa Dangote na mafia wa mafuta Nigeria: Nani atashinda?

cx

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Aliko Dangote alitengeneza utajiri wake kupitia sukari na simenti
    • Author, Will Ross
    • Nafasi, BBC Africa
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Uzalishaji wa petroli katika kiwanda cha mafuta cha mfanyabiashara tajiri, Aliko Dangote chenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 20, huenda ikawa ni habari njema kwa Nigeria.

Kwa muda mrefu tangu mafuta yalipogunduliwa kwa mara ya kwanza nchini Nigeria mwaka 1956, sekta hiyo ya mafuta ghafi yanayosafishwa kuwa petroli na bidhaa nyinginezo, imekuwa ni eneo la mikataba mibaya na kila serikali.

Mkuu wa taasisi ya fikra huria ya Eurasia, Amaka Anku, anakisifu kiwanda cha kusafisha mafuta cha Dangote, ni "wakati muhimu sana" kwa taifa hilo la Afrika Magharibi.

"Kilichokuwepo katika sekta hiyo ni ukiritimba usio na tija na ufisadi," anasema.

Mapato ya mafuta yanachangia karibu 90% ya mapato ya uuzaji nje ya Nigeria, lakini idadi ndogo ya wafanyabiashara na wanasiasa wamejilimbikizia utajiri wa mafuta.

Suala la mtindo wa biashara hiyo limekuwa la kutatanisha, ikiwa ni pamoja na viwanda vinne vya kusafisha mafuta vilivyokuwepo hapo awali. Vilijengwa katika miaka ya 1960, 70 na 80, vimeporomoka katika hali mbaya.

Mwaka jana bunge la Nigeria liliripoti kuwa katika muongo mmoja uliopita nchi hiyo lilitumia kiasi cha dola bilioni 25 kujaribu na kushindwa kurekebisha viwada hivyo.

Nchi hiyo mzalishaji mkubwa wa mafuta barani Afrika imekuwa ikisafirisha mafuta ghafi ambayo husafishwa nje ya nchi, jambo ambalo linawanufaisha baadhi ya wafanyabiashara wenye mtandao mkubwa.

Pia unaweza kusoma

Nani anayefaidika?

erdf

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Nigeria mara nyingi inakabiliwa na uhaba wa mafuta, na kusababisha foleni ndefu katika vituo vya kujaza mafuta
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Nigerian National Petroleum Company (NNPC) hubadilisha mafuta ghafi ya Nigeria kwa bidhaa nyingine, ikiwa ni pamoja na petroli safi, ambayo husafirishwa kurudi nyumbani.

Kiasi gani cha pesa hupatikana na ni nani anayefaidika na "mabadilishano haya ya mafuta" ni moja tu ya mambo yasiyojulikana katika mikataba hii.

"Hakuna mtu ambaye ameweza kufafanua ni nani hasa anayefaidika," anasema Toyin Akinosho kutoka Africa Oil+Gas Report.

Mtaalamu wa mafuta wa Nigeria, Kelvin Emmanuel anasema mwaka 2019 matumizi rasmi ya petroli nchini humo "yaliongezeka kwa 284% hadi lita milioni 70 kwa siku, bila ushahidi ili kuhalalisha ongezeko hilo kubwa la mahitaji."

Bunge limeripoti hapo awali kwamba - kwenye karatasi - waagizaji walikuwa wakilipwa kuleta petroli nyingi zaidi kuliko zinazotumiwa na nchi.

NNPC ilipata mabilioni ya dola kwa mwaka kutokana na uzalishaji wa mafuta ghafi. Lakini kwa miaka mingi, chini ya serikali zilizopita, baadhi ya faida zake hazikuwahi kufikia hazina ya taifa.

Huenda mafuta ndiyo chanzo kikuu cha mapato kwa serikali lakini kwa miongo kadhaa, hadi 2020, NNPC haikuweka wazi hesabu zake. Taarifa yake kwa vyombo vya habari kuanzia Machi mwaka huu iliahidi uwazi zaidi na uwajibikaji.

Bei ya juu ya mafuta, uhaba wa mafuta na sarafu kushuka thamani. Wakati Rais Bola Tinubu anachukua nchi mwezi Machi 2023, dola 1 ya Marekani ilikuwa ni naira 460 na sasa dola 1 ni kwa naira 1600. Mambo hayo yamekuwa pigo kubwa, na wengi wa watu wanalazimika kuendesha jenereta ili kuwasha taa na kuchati simu.

Katika jiji kuu la Lagos mafuta yamepanda kutoka naira 858 ($0.52) hadi naira 1,025 kwa lita.

Moja ya sababu kuu ya mgogoro wa kiuchumi wa Nigeria ni ugavi mdogo wa fedha za kigeni. Nchi hiyo haiuzi nje bidhaa za kutosha na kutoa huduma ili kuleta dola.

Habari njema na mbaya

er

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kiwanda cha kusafisha mafuta kinachomilikiwa na Dangote kina ukubwa wa takriban viwanja 4,000 vya soka

Habari njema ni kwamba kiwanda cha Dangote kitanunua mafuta ghafi na kuuza mafuta yaliyosafishwa nchini Nigeria kwa fedha za ndani, na hilo litaifanya dola iwepo kwa wingi.

Habari mbaya bei ambayo Dangote atalipa kwa pipa la mafuta ghafi ya ndani, bado itakuwa naira sawa na gharama ya kimataifa ya dola.

Kwa hivyo ikiwa bei ya ghafi itapanda katika soko la dunia, Wanigeria watalazimika kulipa naira zaidi. Kusafisha ndani ya nchi kutamaanisha gharama ndogo za usafirishaji lakini ni pesa kidogo zitakazookolewa.

Inatarajiwa kuwa kiwanda cha kusafisha mafuta cha Dangote kutasaidia kuleta uwazi katika sekta hiyo.

Anajua kuwa aliwakasirisha baadhi ya wale wanaonufaika na mikataba ya kutatanisha, wakati mradi wa dola bilioni 20 ulipoanza. Lakini, anasema, alidharau changamoto hiyo.

Mafia wa mafuta

d

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Baadhi ya mafuta ghafi ya Nigeria huishia kwenye vinu haramu kama hiki

"Nilijua kungekuwa na vita. Lakini sikujua kwamba mafia katika mafuta, wana nguvu kuliko mafia katika dawa za kulevya," alisema Dangote katika mkutano wa uwekezaji mwezi Juni.

"Hawataki ufisadi ukome. Dangote anakuja na atawavuruga kabisa biashara yao. Biashara yao iko hatarini," anasema Emmanuel, mtaalamu wa mafuta.

Kiwanda cha kusafisha mafuta cha Dangote karibu na Lagos kina uwezo wa kushughulikia mapipa 650,000 ya mafuta ghafi kwa siku.

Ungefikiri kuwa ingekuwa rahisi kupata mafuta ghafi kwa ajili ya kiwanda hicho. Lakini baadaye kukaibuka kichwa cha habari: "Dangote wa Nigeria anunua mafuta ghafi kutoka Brazili."

Kukatokea mvutano juu ya usambazaji na bei. Mamlaka ya udhibiti ikalalamika kuhusu mbinu za mapatano za Dangote.

Mengine yaliyozuka ni; mafuta ghafi ya Nigeria yana salfa kidogo, na ni mafuta ghali zaidi duniani. Yana bei ya juu kuliko washindani wake wengi.

Mzozo kati ya mdhibiti na Dangote kuhusu kiwanda na bei – umeleta mzozo mwingine na wafanyabiashara wa mafuta - ambao wanakataa kununua kutoka katika kiwanda hicho.

Wakati majadiliano kuhusu bei yalipoanza, Farouk Ahmed, mtendaji mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mafuta chini ya Nigeria (NMDPRA), alimshutumu Dangote kwa "kutaka Lamborghini kwa bei ya Toyota."

Dangote amelalamika kwamba hapewi mafuta ghafi ya kutosha kama ilivyokubaliwa awali, lakini hata suala la bei litakapotatuliwa, bado atahitaji kuagiza mafuta ghafi kutoka nje.

"NNPC haina mafuta ghafi ya kutosha kwa Dangote. NNPC haiwezi kuipa Dangote zaidi ya mapipa 300,000 kwa siku," anasema Akinosho wa Africa Oil+Gas.

Anasema hilo ni kwa sababu NNPC imeuza mamilioni ya mapipa ya mafuta kwa ajili ya mikopo. Mwezi Agosti 2023 ilipata mkopo wa dola bilioni 3 kutoka kwa taasisi ya kifedha ya Afreximbank. Kwa malipo ya kusambaza mapipa milioni 164 ya ghafi.

Septemba NNPC ilikubali kuwa ina deni kubwa. Iliripotiwa kuwa inadaiwa na wasambazaji wake karibu dola bilioni 6 kwa mafuta yaliyoingizwa Nigeria.

Uzalishaji wa mafuta nchini Nigeria umeshuka katika miaka ya hivi karibuni kutoka mapipa milioni 2.1 kwa siku mwaka 2018 hadi mapipa milioni 1.3 kwa siku mwaka 2023.

NNPC inasema wizi wa mafuta ndio sababu kuu kushuka kwa uzalishaji.

Inasema katika wiki moja tu - kutoka 28 Septemba hadi 4 Oktoba - kulikuwa na matukio 161 ya wizi wa mafuta na mitambo haramu 45 ya kusafisha "iligunduliwa.”

Sababu nyingine zinazochangia kushuka kwa uzalishaji, ni pamoja na makampuni ya kimataifa ya mafuta kuuza maeneo yao ya ufukweni ya mafuta - ambayo baadhi hayafai tena baada ya kuchimbwa mafuta kwa miaka 60.

Dangote mwenye umri wa miaka 66, ambaye ameorodheshwa na Bloomberg Billionaires Index kama mtu wa pili kwa utajiri barani Afrika, alipata utajiri wake katika saruji na sukari.

Mabishano kati ya maafisa katika kiwanda cha kusafisha mafuta cha Dangote, wauzaji mafuta na wadhibiti hutokea mara kwa mara kwenye vyombo vya habari.

Pande zote zinashutumiwa kwa kuficha ukweli na takwimu, na huwaacha watu wakishuku juu ya kinachoendelea ndani ya sekta hii ambayo bado haijaeleweka.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdalla na kuhaririwa na Seif Abdalla