Kwanini uchumi wa Nigeria upo kwenye hali mbaya

Chanzo cha picha, AFP
Na Nkechi Ogbonna
BBC News, Lagos
Kwa sasa Nigeria inakabiliwa na mgogoro mbaya zaidi wa kiuchumi katika kizazi, na kusababisha ugumu wa maisha na hasira kuenea.
Kundi mwavuli la vyama vya wafanyakazi, Nigeria Labour Congress (NLC), limeandaa maandamano ya nchi nzima siku ya Jumanne, likitaka hatua zaidi kutoka kwa serikali.
Lita moja ya petroli inagharimu zaidi ya mara tatu ikilinganishwa na miezi tisa iliyopita, wakati bei ya chakula muhimu , mchele, imepanda zaidi ya mara mbili katika mwaka uliopita.
Takwimu hizi mbili zinaangazia matatizo ambayo Wanigeria wengi wanakabiliwa nayo kwani mishahara haijaendana na kupanda kwa gharama ya maisha.
Kama mataifa mengi, Nigeria imekumbwa na misukosuko ya kiuchumi kutoka nje ya mwambao wake katika miaka ya hivi karibuni, lakini pia kuna masuala mahususi kwa nchi hiyo, kwa kiasi fulani yakichochewa na mageuzi yaliyoletwa na Rais Bola Tinubu alipoingia madarakani Mei mwaka jana.
Uchumi ni mbaya kiasi gani?
Kwa ujumla, mfumuko wa bei wa kila mwaka, ambao ni kiwango cha wastani ambacho bei hupanda, sasa unakaribia 30% - kiwango cha juu zaidi katika karibu miongo mitatu. Gharama ya chakula imeongezeka zaidi - kwa 35%.
Hata hivyo, kima cha chini cha kila mwezi cha mshahara, kilichowekwa na serikali na ambacho waajiri wote wanapaswa kuzingatia, hakijabadilika tangu 2019, wakati kiliwekwa naira 30,000 - hii ni ya thamani ya $ 19 (£ 15) tu kwa viwango vya sasa vya kubadilisha fedha.
Wengi wanalala njaa, wakipunguza chakula wanachokula au kutafuta njia mbadala za bei nafuu.
Kaskazini, baadhi ya watu sasa wanakula mchele ambao hutupwa kama sehemu ya mchakato wa kusaga. Bidhaa taka kawaida hutumiwa kama chakula cha samaki.
Video zinazoshirikiwa sana za mitandao ya kijamii zinaonyesha jinsi baadhi ya watu walivyopunguza chakula wanachokula sasa.
Klipu moja inaonyesha mwanamke akikata samaki katika vipande tisa badala ya wastani wa vinne hadi tano. Anasikika akisema lengo lake ni kuhakikisha familia yake inaweza kula samaki angalau mara mbili kwa wiki.
Ni nini kinachosababisha mdororo wa kiuchumi wa Nigeria?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mfumuko wa bei umeongezeka katika nchi nyingi, huku gharama za mafuta na nyinginezo zikiongezeka kutokana na vita vya Ukraine.
Lakini juhudi za Rais Tinubu za kurekebisha uchumi pia zimeongeza mzigo.
Siku alipoapishwa miezi tisa iliyopita, rais mpya alitangaza kuwa ruzuku ya mafuta ya muda mrefu itaondolewa.
Hili lilikuwa limeweka bei ya petroli kuwa chini kwa wananchi wa taifa hili linalozalisha mafuta, lakini pia lilikuwa tatizo kubwa la fedha za umma. Katika nusu ya kwanza ya 2023, ilichangia 15% ya bajeti - zaidi ya matumizi ya serikali katika afya au elimu. Bw Tinubu alidai kuwa hii inaweza kutumika vyema mahali pengine.
Walakini, kuongezeka kwa bei ya petroli baadaye kumesababisha bei zingine kupanda huku kampuni zikipitisha gharama za usafirishaji na nishati kwa watumiaji.
Sababu nyingine inayochochea mfumuko wa bei ni suala ambalo Bw Tinubu alirithi kutoka kwa mtangulizi wake, Muhammadu Buhari, kulingana na mchambuzi wa masuala ya fedha Tilewa Adebajo.
Aliambia kipindi cha Newsday cha BBC kwamba serikali iliyopita iliomba benki kuu ya nchi hiyo mikopo ya muda mfupi ili kufidia matumizi ya kiasi cha $19bn.
Benki ilichapisha pesa hizo, ambazo zilisaidia mfumuko wa bei ya mafuta, Bw Adebajo alisema.
Nini kimeifanyikia Naira?
Bw Tinubu pia alikomesha sera ya kuweka bei ya sarafu, naira, kwa dola ya Marekani badala ya kuiachia soko kuamua kwa misingi ya ugavi na mahitaji. Benki kuu ilikuwa ikitumia pesa nyingi kudumisha kiwango hicho.
Lakini kung'oa kigingi kumepelekea thamani ya naira kushuka kwa zaidi ya theluthi mbili, na kushuka kwa muda mfupi wiki iliyopita.
Mei iliyopita, naira 10,000 zingebadilishwa kwa $22, sasa inabadilishwa na takriban $6.40 pekee.
Kwa vile naira ina thamani ndogo, bei ya bidhaa zote zilizoagizwa kutoka nje imepanda.
Mambo yatakuwa mazuri lini?
Wakati rais huenda asibadilishe maamuzi yake kuhusu ruzuku ya mafuta na naira, ambayo anadai kuwa italipa kwa muda mrefu kwa kufanya uchumi wa Nigeria kuwa na nguvu, serikali imeanzisha baadhi ya hatua za kupunguza mateso.
Makamu wa Rais wa Nigeria Kashim Shettima alitangaza kuanzishwa kwa bodi yenye dhamana ya kusimamia na kudhibiti bei za vyakula. Serikali pia iliamuru hifadhi ya kitaifa ya nafaka kusambaza tani 42,000 za nafaka, ikiwa ni pamoja na mahindi na mtama.
Hii si mara ya kwanza kwa serikali kusema kuwa inasambaza misaada kwa Wanigeria maskini na walio katika mazingira magumu, lakini vyama vya wafanyakazi mara nyingi vimekuwa vikikosoa mbinu ya serikali ya usambazaji wa chakula, vikisema wakati mwingi misaada haifikii familia maskini.
Serikali pia imesema inashirikiana na wazalishaji wa mpunga ili kuuingiza sokoni na maafisa wa forodha wameagizwa kuuza kwa bei nafuu magunia ya nafaka ambayo wameyanasa. Katika ishara ya jinsi mambo yalivyo mabaya, siku ya Ijumaa hii ilisababisha mkanyagano katika jiji kubwa zaidi la Lagos, ambapo watu saba , vyombo vya habari vya ndani vinaripoti. Mpango huo sasa umesitishwa .
Mpunga huo ulikamatwa chini ya serikali iliyopita, ambayo ilipiga marufuku uagizaji wa mchele kutoka nje ili kuhamasisha wakulima wa ndani kulima zaidi. Marufuku hiyo iliondolewa mwaka jana kwa kujaribu kupunguza gharama lakini kwa sababu ya kushuka kwa thamani ya naira, hilo halijafanikiwa.
Takriban familia milioni 15 maskini pia zinapokea msaada wa fedha wa naira 25,000 ($16; £13) kwa mwezi, lakini siku hizi hilo halisaidii sana .

Imetafsiriwa na Yusuf Jumah












