Kwa nini raia wa Nigeria wanaandamana?

 Maandamano ya kupinga bei ya vyakula Ibadan
Maelezo ya picha, Wiki iliyopita, Ofisi ya Kitaifa ya Takwimu ya Nigeria iliripoti kwamba mfumuko wa bei ulikuwa wa juu zaidi katika miongo mitatu, ukichangiwa na mfumuko wa bei ya chakula.
    • Author, Na Nkechi Ogbonna
    • Nafasi, BBC News, Lagos

Vyakula vya kimsingi vimekuwa ghali sana kwa Wanigeria wengi kumudu. Katika baadhi ya maeneo ya nchi, watu wanaingia barabarani kupinga kupanda kwa bei ya vyakula katika taifa lenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika.

Kupanda kwa gharama ya maisha na shinikizo la mfumuko wa bei kumeonekana duniani kote lakini nchini Nigeria, hii imekuwa mbaya zaidi kutokana na serikali kuondoa ruzuku ya mafuta na kuendelea kudhoofika kwa sarafu ya Naira, dhidi ya sarafu kuu za kigeni.

Kwa nini Wanigeria hawana furaha?

Njaa ndio sababu kuu ya Wanigeria kutokuwa na furaha na kuandamana. Hivi majuzi, maelfu waliingia mitaani katika majimbo ya kaskazini ya Niger, Kano na Kogi na Ibadan magharibi mwa Nigeria, kudai uingiliaji wa haraka ambao utashughulikia kupanda kwa gharama ya maisha.

Katika jimbo la Kano, ambapo gharama ya vyakula vikuu ikiwa ni pamoja na mchele, mtama na mahindi imepanda, karibu watu milioni 10 wanaishi katika hali ya umaskini, ambao ndio wa juu zaidi nchini.

Wiki iliyopita, Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya Nigeria (NBS) iliripoti mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 29.9, kiwango cha juu zaidi katika takriban miongo mitatu, ukichangiwa na mfumuko wa bei wa vyakula ambao umepanda hadi asilimia 35.4.

Maandamano ya kupinga bei ya vyakula Ibadan

Je, chakula kimekuwa ghali kiasi gani nchini Nigeria?

Bei ya mkate, chakula kikuu cha kifungua kinywa katika nyumba nyingi nchini kote, imepanda kutoka Naira 500 ($0.33) hadi zaidi ya 1,500 ($0.87) ndani ya mwaka mmoja. Bidhaa nyingine za vyakula kama vile mayai, samaki, nyama, mchele na mafuta ya kupika vyote vimeshuhudia ongezeko kubwa la bei. Mfuko wa kilo 50 za mchele, chakula maarufu zaidi, sasa unagharimu Naira 75,000, kutoka Naira 35,000 katika mwaka mmoja uliopita.

Bunge la Nigeria, NLC, limeipa serikali makataa ya siku 14 kutatua mzozo wa kiuchumi, na kutishia mgomo wa nchi nzima mnamo tarehe 27 na 28 Februari. Muungano huo unasema hali ni mbaya zaidi kwa wafanyakazi wa Nigeria ambao wanapata kima cha chini cha Naira 30,000 (dola 20) kwa mwezi.

Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeonya kuwa Nigeria, Ethiopia, Angola na Kenya ziko kwenye hatari ya machafuko kwa sababu ya kupanda kwa bei ya mafuta na bidhaa za chakula.

''

Watu wanageukia nini?

Katika baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa nchi, wakaazi wameanza kukusanya mabaki kutoka kwa wasagaji wa mpunga ili kuyatumia kama chakula. Mabaki hayo yalikuwa kiungo katika uzalishaji wa chakula cha samaki, lakini sasa ndicho ambacho baadhi ya Wanigeria wanaweza kumudu kuzuia njaa.

Video za mitandao ya kijamii pia zimekuwa zikisambazwa zikionyesha familia kadhaa za Nigeria zikigawa chakula.

Video moja inaonyesha mwanamke akikata samaki mmoja katika vipande tisa badala ya wastani wa vipande vinne hadi vitano. Anasema ndiyo njia pekee ya kuhakikisha familia yake inaweza kula samaki mara mbili kwa siku.

tt
Maelezo ya picha, Vyama vya wafanyikazi mara nyingi vimekosoa mfumo wa serikali ya usambazaji wa chakula

Serikali inafanya nini?

Makamu wa Rais wa Nigeria Kashim Shettima ametangaza kuanzishwa kwa bodi ya kudhibiti bei za vyakula. Serikali pia imeamuru hifadhi ya kitaifa ya nafaka kusambaza tani 42,000 za nafaka, ikiwa ni pamoja na mahindi na mtama.

Hii si mara ya kwanza kwa serikali kusema kuwa inasambaza misaada kwa Wanigeria maskini na wasiojiweza. Mbinu yao ya usambazaji wa chakula hata hivyo, mara nyingi imekuwa ikikosolewa na vyama vya wafanyakazi ambao wanasema sehemu kubwa haifikii familia maskini zaidi zinazohitaji.

Nani mwingine anatoa suluhisho?

Baadhi ya waajiri wamejibu mgogoro wa kiuchumi kwa kupunguza idadi ya siku katika wiki ambazo wafanyakazi wanatarajiwa kujitokeza kazini, ili kuokoa gharama za usafiri. Kampuni zingine pia zimelazimika kuongeza mishahara ya wafanyikazi kwa zaidi ya asilimia 50 ili kufikia gharama ya mfumuko wa bei.

Baadhi ya wazalishaji wakubwa wa vyakula vya mifugo wamesema wanasitisha ununuzi wa malighafi yakiwemo mahindi na mtama ili kuongeza upatikanaji wa nafaka sokoni kwa matumizi ya binadamu. Uamuzi huu una athari kwa sekta ya mifugo, sehemu muhimu ya mzunguko wa chakula nchini Nigeria.

Imetafsiriwa na Jaison Nyakundi