Kupanda kwa bei ya mafuta ghafi kuna athari Afrika?

Mapipa ya mafuta

Chanzo cha picha, AFP

Bei ya mafuta ya petroli barani Afrika inatazamiwa kupanda katika wiki za usoni kutokana na matokeo yaliyosababisha na kuongezeka ama kupanda kwa bei ya mafuta duniani, kwa mujibu wa wachambuzi.

Siku ya Jumanne bei ya mafuta ghafi, ilipanda bei mpaka zaidi ya dola $80 kwa pipa moja ikiwa ni kwa mara ya kwanza kwa zaidi ya miaka mitatu.

Kimetokea nini?

Kulegezwa kwa masharti ya janga la Covid-19, upatikanani wa chanjo, kuanza ena kwa safari za ndege za kimataifa na kurejea kwa shughuli za kiuchumi wakati dunia ikirejea katika hali yake ya kawaida baada ya janga, imefanya mahitaji ya mafuta kuogezeka, na kusababisha bei kupata.

Mtaalamu wa masuala ya mafuta, Patrick Obath, anasema "Usambazaji wa mafuta ni mdogo kulinganisha na mahitaji. Tunatarajia bei itaendeea kupanda katika miezi michache ijayo na huenda kukatoka na jambo la lingine la kushangaza kwa sababu ya mahitaji kuongezeka wakati wa majira ya baridi Ulaya na Marekani."

Kwa nini wazalishaji wa mafuta Afrika hawawezi kulikwepa hili ?

Nchi nyingi Afrika zinatarajiwa kuathirika kwa kuwa zinategemea mafuta ghafi kwa ajili ya mahitaji yake ya nishati.

Diran Fawibe, mchumi kutoka International Energy Services, anasema "Barani Afrika, ingawa kuna nchi chache zinazozalisha mafuta kama Nigeria na Angola, baadhi ya nchi abazo hazizalishi mafuta zitaongeza bei kwa ababu watapaswa kuagiza kutoka nje kwa bei ya juu kuliko ilivyokuwa awali, na baadhi ya nchi hizo tayari zimeanza kukumbana na tatizo hilo la kuweka uwiano sawa wa bajeti zao."

Hii maana yake ni habari mbaya kwa nchi kama Kenya inayoshuhudia kupanda kwa kasi kwa bei ya mafuta katika miezi michache iliyopita. Mwezi Septemba mamlaka nchini humo ziliongeza bei ya mafuta ya petrol mpaka dola $1.22 kwa lita, katika jiji la Nairobi, ongezeko la asilimia 6 kutoka mwezi uliopita, ikiwa ni ongezeko kubwa, katika muongo uliopita.

Jumatatu wiki hii, Mahakama ilizuia mpango wa Mamlaka ya mapato nchini humo (KRA) wa kuongeza ushuru kwenye mafuta. Katika uamuzi, Jaji James Makau alisema kuwa uamuzi wa kuruhusu ushuru huo ungekuwa na hatari kwa Wakenya kutokana na ongezeko zaidi la bei ya mafuta.

Bei za mafuta mara nyingi zinaonekana kama kipimo cha shughuli za uchumi. Gharama za mafuta ni kiungo muhimu kwenye gharama za maisha kwa nchi nyingi, ikiwa na athari za moja kwa moja kwenye gharama uzalishaji, bei ya umeme na bei ya bidhaa za kawaida.

Ken Gichinga, mchumi kutoka Mentoria Consulting anasema, "Rekodi ya kuongezeka kwa bei ya mafuta kutasababisha kupanda kwa gaharama za kufanya biashara."

Kwa namna gani wazalishaji wa mafuta kama Nigeria, Angola wanaathirika?

Kama bei inapanda pengine lingekuwa kama jambo zuri kwa wazalishaji hawa wakubwa wa mafuta Afrika, lakini haifahamiki kama wataweza kunufaika na hilo.

Nigeria na Angola na wao wanaguswa angalau kwa muda mfupi kutokana uwekezaji duni, maana yake hazizalishi kwenye ubora na viwango vinavyotakiwa.

"Kama Nigeria ingekuwa na uwezo wa kuzalisha, ingeweza kutumia fursa hii ya kupanda kwa bei, lakini haiku hivyo kwa sasa kwa sababu Nigeria inazalisha kiduchu," anasema mchumi Diran Fawibe.

Kupanda kwa bei ya mafuta duniani inaweza kuongeza mapato kwa muda mfupi , lakini thamani halisi itaonekana wakati wazalishaji wa mafuta watakavyoweza kuzalisha na kukidhi mahitaji ya usambazaji..

Bismark Rewane, mchumi kutoka Nigeria anasema "Kwa sababu Nigeria kwa sasa inaagiza bidhaa za mafuta kutoka nje, utaona bei ya mafuta kwenye pampu inakwenda sawa na senti 17 kwa lita. Kama gharam hizo zitafikia karibu na dola 1, kuna uwezekano serikali ikaendelea kutoa ruzuku kufidia bei hiyo ya mafuta au kama wataamua kurekebisha italeta athari katika jamii."

Nchi nyingi Afrika zinatarajiwa kuathirika kwa kuwa zinategemea mafuta ghafi kwa ajili ya mahitaji yake ya nishati

Chanzo cha picha, Getty Images

Nini cha kufanya?

Nchi zinazozalisha na kuuza mafuta duniani kupitia muungano wao wa (OPEC) zinanatarajiwa kukutana Oktoba 4. Baadhi ya wachambuzi wana matumaini kwamba pengine nchi hizo zinaweza kuongeza usambazaji wa mafuta. Hatua hiyo itasaidia nchi kama kuogeza uzalishaji wake na kuneemeka na kupanda huko kwa bei ya mafuta.

Michael Famoroti, mchumi mwandamizi kutoka Stears, anasema "Hatma ya usambazaji wa mafuta unabaki mikononi mwa OPEC na namna gani itaruhusu wanachama wake kuogeza uchimbaji. Inaonekana OPEC watajaribu kuleta unafuu wa bei ili kuvutia uwekezaji zaidi katika sekta ya mafuta, ambao umeporomoko kwa kiwango kikubwa katika kipindi cha miezi 18 iliyopita.

Natarajia hatua madhubuti zitachukuliwa na OPEC kabla ya mwisho wa mwaka, lakini sitarajii wanaweza kufanyika kwa mabadiliko makubw akatika mkutano wa wiki ijayo."