Shindano la urembo katika sehemu hatari zaidi kuwa mwanamke

Chanzo cha picha, Shukri Mohamed Abdi
- Author, Kiin Hassan Fakat & Mary Harper
- Nafasi, Mogadishu
Wakati watu wengi nchini Somalia wakijibana kwenye mikahawa na majumbani Jumapili usiku kutazama fainali ya michuano ya Euro 2024, upande mwingine mamia ya wakazi wa Mogadishu walikusanyika katika Hoteli ya kifahari kwa shindano lingine: Miss Somalia.
Tukio la gari kulipuka umbali wa kilomita moja kutoka kwa mkahawa wa Top Coffee uliokuwa umejaa mashabiki wa soka linakupa taswira ya mazingira na hali ya maisha ya kila siku nchini Somalia.
Wakati washiriki wa shindano la urembo walipokuwa wakitembea jukwaani kuonyesha mitindo yao katika hoteli hiyo, takriban watu watano waliuawa na wengine 20 kujeruhiwa katika mlipuko.
Wanamgambo wa kundi la al-Shabab, ambalo limedhibiti sehemu kubwa ya Somalia kwa zaidi ya miaka 15, lilidai kufanya shambulio hilo.
Hani Abdi Gas alianzisha shindano la Miss Somalia mnamo 2021, jambo la kijasiri kufanya katika nchi ya kihafidhina, kitamaduni inayokabiliwa na wanamgambo wa kijihadi. Somalia imekuwa ikiongoza mara kwa mara katika orodha ya maeneo hatari zaidi duniani kuwa mwanamke.
Bi Gas alikulia katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab nchini Kenya, pamoja na mamia ya maelfu ya Wasomali wengine waliokimbia vita na ukame. Alirudi katika nchi yake mnamo 2020.
Ingawa shindano hilo linahusu urembo, Bi Gas anasema lengo kuu la shindano hilo ni kupaza sauti za wanawake dhidi ya unyanyasaji.
"Inakuza umoja na uwezeshaji," alisema.
Bi Gas anaamini kuwa ni wakati wa Somalia kujiunga na mataifa mengine duniani linapokuja suala la mashindano ya urembo. "Nataka kusherehekea matarajio ya wanawake kutoka asili mbalimbali, kujenga imani yao na kuwapa nafasi ya kuonyesha utamaduni wa Kisomali duniani kote."
Mashindano ya mwaka huu yalijumuisha wanawake kutoka nyanja tofauti za maisha. Mmoja wa washiriki alikuwa polisi mwanamke.

Chanzo cha picha, Shukri Mohamed Abdi
Shindano la urembo linachukuliwa kuwa wazo la kutisha nchini Somalia.
Baadhi wanaziona kama dharau kwa Uislamu na utamaduni wa Kisomali. Wengine wanasema ni aina nyingine ya unyanyasaji wa kijinsia, unaowadhalilisha haswa wanawake.
"Nimechukizwa na wazo la wasichana wetu kushiriki katika shindano hili baya," kiongozi wa ukoo Ahmed Abdi Halane alisema.
“Mambo kama haya ni kinyume na utamaduni wetu na dini yetu. Ikiwa msichana atavaa nguo za kubana na kuonekana jukwaani, ataleta aibu kwa familia yake na ukoo wake. Wanawake wanapaswa kukaa nyumbani na kuvaa mavazi ya heshima."
Wanawake wengine pia wanapinga mashindano ya urembo.
"Ni vizuri kuunga mkono vijana wa Kisomali lakini si kwa njia zinazokinzana na dini yetu," alisema mwanafunzi Sabrina, ambaye hakutaka kufichua jina lake la ukoo.
"Si sahihi kwa mwanamke kujitokeza hadharani bila kujitanda na ndivyo washiriki wa Miss Somalia walifanya."
Tofauti na majoho ya rangi moja na stara zinazovaliwa na wanawake wengi wa Kisomali, washiriki wa Miss Somalia walivaa gauni za kuvutia na za kupendeza.
Akiwa amevalia gauni refu la dhahabu huku mikono ikitiririka hadi sakafuni, Aisha Ikow mwenye umri wa miaka 24 alitawazwa mshindi wa Miss Somalia na kujinyakulia zawadi ya pesa taslimu dola 1,000 za Kimarekani .

Chanzo cha picha, Shukri Mohamed Abdi
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Yeye ni mwanafunzi wa chuo kikuu na msanii wa mapambo, na aliwakilisha jimbo la Kusini-Magharibi. Wengine walioingia fainali walikuwa warembo wa kikanda kutoka Jubaland kusini na Galmudug katikati mwa Somalia.
"Nitatumia hii kama fursa ya kupiga vita ndoa za mapema na kukuza elimu ya wasichana," alisema Bi Ikow.
"Shindano hilo linasherehekea utamaduni na urembo wa Kisomali huku likiunda mustakabali mzuri wa wanawake."
Majaji sita, wanawake watano na mwanamume mmoja, walipata ugumu kuchagua mshindi.
Jopo hilo lilijumuisha mwanzilishi Bi Gas, mwakilishi kutoka wizara ya vijana na Miss Somalia 2022. Waliwahukumu washiriki kulingana na urembo wao wa kimaumbile, jinsi walivyotembea kwenye mwambao, mavazi yao na jinsi walivyozungumza hadharani.
Pia kulikuwa na kura ya mtandaoni iliyowekwa wazi kwa umma.
Iligharimu dla moja kupiga kura, na pesa zilizopatikana zilitumika kufadhili hafla hiyo huko Mogadishu na safari za ng'ambo kushindana katika shindano la Miss Africa, Miss World na Miss Universe.

Chanzo cha picha, Shukri Mohamed Abdi
Shindano la usiku katika hoteli ya kifahari iliyo mbele ya bahari lilikuwa tofauti na maisha ya watu wengi nchini Somalia, haswa wanawake.
Wasomali milioni nne, takriban robo ya wakazi, wanaishi kwingineko nchini humo baada ya kulazimishwa kutoka makwao.
Umoja wa Mataifa unakadiria kati ya 70% na 80% yao ni wanawake.
Mwaka 2024 taarifa za kutosha zilikusanywa kuiwezesha Somalia kujumuishwa katika taarifa za Umoja wa Mataifa za maendeleo ya watu kwa mara kwanza ndani miaka 30. Somalia ilishika nafasi ya mwisho.
Somalia ni ya nne kutoka mwisho kwenye orodha hiyo linapokuja suala la Ukosefu wa Usawa wa Kijinsia. Mashirika ya misaada yanasema asilimia 52 ya wanawake nchini wamepitia ukatili wa kijinsia. Takriban 98% hukeketwa.
Tangu jadi, mwanamume alipombaka mwanamke, "adhabu" yake ilikuwa kwamba alipaswa kumuoa mwanamke aliyemnyanyasa kingono. Mitazamo kuhusu ubakaji na aina nyingine za unyanyasaji dhidi ya wanawake haijabadilika sana kwa miaka mingi.
Mwaka 2013, mwanamke mmoja mjini Mogadishu alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela baada ya kuripoti kwamba alibakwa na askari wa vikosi vya usalama.
Katika eneo la Somaliland lililojitangaza kuwa huru, viongozi wa kidini walifuta sheria ya makosa ya kingono ya 2018 mara tu ilipotiwa saini. Toleo lililosahihishwa haliwalindi wanawake dhidi ya ndoa za utotoni, ndoa za lazima, ubakaji au aina nyinginezo za unyanyasaji wa kijinsia.
Lakini wazo kwamba shindano la Miss Somalia linaweza kufanyika mjini Mogadishu, hata kilomita moja kutoka kwa shambulio la bomu la kujitoa mhanga, inaonyesha kuwa nchi inabadilika katika mtazamo na usalama.
Hakuna mtu angelidhubutu kuandaa mashindano ya urembo miaka michache iliyopita, haswa wakati al-Shabab ilipodhibiti mji mkuu.
Umati wa watu katika Hoteli ya Elite haukuondoka hadi asubuhi. Hawakusikia sauti ya shambulio la jirani kwani lilizamishwa na kelele za mawimbi ya Bahari ya Hindi yaliyokuwa yakipiga ufukweni.
Kiin Hassan Fakat ni mwanahabari wa Bilan Media, chombo cha habari kinachoendeshwa na wanawake nchini Somalia.
Mary Harper ameandika vitabu viwili kuhusu Somalia, ikiwa ni pamoja na Everything You Have Told Me Is True, kinachoangazia maisha chini ya al-Shabab.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi na kuhaririwa na Yusuf Jumah












