Ulimwengu uliofichwa wa biashara ya ngono Somalia

.

Chanzo cha picha, LEYLA JEYTE

Maelezo ya picha, Ufukwe wa Lido wa Mogadishu ni sehemu inayostawi ya maisha ya mji mkuu, lakini karibu yake kuna upande wa maisha uliofichwa

Wanawake wawili katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, wamekuwa wakizungumza na BBC kuhusu jinsi walivyovutiwa na ulimwengu wa siri wa biashara ya ngono katika jiji linaloishi chini ya tishio la ghasia kufuatia miaka ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Tumebadilisha majina yao ili kulinda utambulisho wao.

Ufukwe wa Lido uliochangamka na wenye shughuli nyingi wa Mogadishu unatoa taswira ya jinsi jiji linavyoweza kuwa, linapojaribu kusahau masuala ya mizozo, ghasia na vita.

Maeneo ya mapumziko ya bahari, mikahawa ya ngazi ya juu, hoteli na vyakula vipya ni vivutio vikubwa.

Lakini kukaa karibu na eneo hilo utakutana na mengine mengi – watu kufanya karamu, utumiaji wa dawa za kulevya na ghasia zinazochochewa na ngono.

Wanawake walionaswa katika upande huu uliofichika wa jiji ni vijana, masikini na mara nyingi walio katika hatari kwenye taifa hili lenye Waislamu wengi.

Fardousa, 22, ambaye amekuwa mfanyabiashara ya ngono kwa miaka mitatu, amekaa katika chumba cheusi kilichofunikwa na mapazia mekundu katika jengo la ghorofa lililojaa matundu ya risasi katika wilaya ya Wardhigley ya Mogadishu.

Juu ya kelele za jiko, msichana mwembamba mwenye sauti nyororo anaelezea kile kilichompata.

Fardousa anaelezea kwamba aliondoka nyumbani akiwa na umri wa miaka 19, jambo ambalo ni nadra sana katika jamii ya Kisomali ambapo wasichana kwa ujumla hawaachi familia kabla ya kuolewa.

Hata hivyo, dhuluma nyumbani au tofauti zisizoweza kusuluhishwa na wanafamilia wengine zinaweza kuwasukuma kwenda mbali na hili linaonekana kuwa jambo linaloendelea kuongezeka.

"Mwanzoni sikuona kama kutoroka lakini sikuweza kuvumilia kuishi na mama yangu wa kambo tena," Fardousa anasema.

"Alikua mke wa pili wa baba yangu baada ya mama yangu kuaga dunia nikiwa mdogo. Alikuwa mnyanyasaji sana kwa miaka mingi na licha ya hayo, baba yangu alikubali alichosema yeye na kumpendelea kila mara."

.

Chanzo cha picha, LEYLA JEYTE

Maelezo ya picha, Wafanyabiashara ya ngono Mogadishu wanaishi kwenye vivuli na ni nadra sana sauti zao kusikiki

Baada ya kuondoka nyumbani, Fardousa alianza kuhama kutoka sehemu moja hadi nyingine kutafuta marafiki wapya, ambao alifikiri wangejali maslahi yake:

"Nilifikiri walinijali. Nikiangalia nyuma sasa, najua hawakuwa marafiki wa kweli."

Hatimaye akawa mraibu wa opioidi au afyuni kama vile mofini, tramadol na petidini yaani pethidine, na akajiunga na matukio yanayofanywa kisiri kama karamu za usiku katika Ufuo wa Lido, ambapo alitambulishwa kwa kazi ya ngono.

Fardousa hivi karibuni alijikuta amenaswa katika dunia ya Mogadishu ambako anaenda kutoka hotelini moja hadi nyingine kwenye nyumba za wageni katika maeneo yaliyojitenga.

Lakini sasa anajua wateja wa kutosha ambao anaweza kuwategemea wanaowasiliana naye kwa simu.

"Nasubiri simu yangu iite kisha nitoke na wanaume kufanya ngono.

Wakati mwingine, marafiki zangu wa kike hunipigia simu wakiwa na wateja tayari."

'Nilihitaji pesa kwa ajili ya uraibu wangu'

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Anajihusisha na wateja kutoka matabaka mbalimbali ya maisha.

"Wanaume hawa mwanzoni walikuwa marafiki wa kiume wa marafiki zangu wa kike, kisha ikabadilika na kuanza kufanya mapenzi na wanaume tofauti ambao sikuwafahamu.

Nilikuwa katika mazingira magumu na nilihitaji pesa kwa ajili ya uraibu wangu, sawa tu na wasichana wengine wengi katika jiji hili. "anasema Fardousa.

Kwa sababu ya asili yake, hakuna data rasmi juu ya kiwango cha kazi ya ngono lakini ushuhuda kutoka kwa Fardousa na wengine unatoa taswira ya mazingira hatari ambayo wasichana wengi kama hawa wanajikuta wametumbukia.

Hodan amekuwa mfanyabiashara ya ngono kwa miaka miwili na nusu.

Kama Fardousa, kijana mwenye umri wa miaka 23 alitoroka nyumbani na kujikuta amezama katika maisha ya chinichini ya Mogadishu yanayojumuisha vijana wenzake waliotoroka makwao ambao hawana msaada wa kifedha.

Anazungumza juu ya sauti ya watoto wanaocheza mpira nje kwa sauti ya utulivu kabisa.

"Mimi hutumia usiku mwingi nikiwa katika mahoteli. Vivyo hivyo kwa wengi wa wasichana hawa. Unakutana na wanaume wa kila aina huko lakini mambo yanaweza kuwa mabaya zaidi unapotoka na baadhi ya wanaume hawa," Hodan anasema.

Kwa vile biashara ya ngono ni kinyume cha sheria nchini Somalia, wengi wa wanawake hao vijana wanajikuta katika mazingira hatarishi bila kukimbilia usalama wao kwa mamlaka.

BBC iliomba maoni kutoka kwa maafisa wa polisi na wizara ya maendeleo ya wanawake na haki za binadamu kuhusu hili na masuala mengine yaliyotolewa katika makala hiyo, lakini haikupata jibu.

.

Chanzo cha picha, Leyla Jeyte

Maelezo ya picha, Baadhi ya wafanyabiashara ya ngono, kama Fardousa, sasa wanatumia simu zao kuwasiliana na wateja badala ya kuhatarisha kuwasiliana mahali hatari.

"Mara nyingi wasichana wanarudi wakiwa wamenyanyaswa wakiwa na alama kwenye miili yao, huku wafanyabiashara wengine wadogo wa ngono wakitumiwa vibaya na watu wanaofikiri wanaweza kuwaamini," kulingana na Hodan.

Kwa Fardousa, hii inasababisha vurugu.

"Awali, nilikuwa nikienda na wanaume sehemu walizochagua wao kufanya mapenzi lakini siku moja usiku nilipigwa na kupata michubuko usoni na kuachwa nikimwagika damu, yote yalianza kwa sababu hatukukubaliana juu ya bei," anasema.

"Tangu wakati huo siendi sehemu za siri na mwanaume yeyote bila kujali wanatoa kiasi gani, ni hatari sana, napendelea hoteli nikijua hutadhurika na ikiwa hivyo basi kilio chako kitasikikana kupata msaada.

"Wanawake wengine wengi wanaojihusisha na biashara ya ngono hawana bahati sana. Wafanyabiashara ya ngono wanaokwenda na wanaume hawa majumbani mwao na maeneo ya faragha wananyanyaswa na hata kubakwa, wakati mwingine na zaidi ya mwanaume mmoja."

Anasema pia kwamba mashambulizi hayo wakati mwingine hurekodiwa na wanawake hao hulaghaiwa.

"Wanaogopa aibu watakapojulikana wanachofanya"

'Ni vigumu kuwakabili wapendwa'

Hodan anasema kuchukuliwa video inaweza kutokea kwa wafanyabiashara ya ngono baada ya kulewa na kutumia madawa ya kulevya, huku wahalifu wakiwashurutisha kugawanya faida zao.

"Ikiwa watakataa, basi wanapigwa na kudhulumiwa kimwili na wanaume huku video ikitumika kama chombo dhidi yao. Katika baadhi ya matukio, wanajulikana hata kushirikisha video hiyo ili kuwatesa wasichana zaidi. Ni aina ya ulaghai wa kidijitali."

Ripoti ya hivi majuzi ya mtandao wa TV wa Uingereza Channel 4 iliandika aina hizi za udhalilishaji zinazotokea miongoni mwa wanawake wa Somalia kwa ujumla, nje ya mipaka ya kazi ya ngono.

"Imetokea kwa wasichana wengi ninaowajua. Wengi wanaona aibu kukubali lakini sote tunajua kinachoendelea. Tumekaa katika mtindo huu wa maisha kwa muda mrefu," Hodan anasema.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa iligundua kuwa kulikuwa na ongezeko kubwa la unyanyasaji wa kijinsia kutoka 2019 hadi 2020, ikisema kuwa unyanyasaji mara nyingi huongezeka katika maeneo yenye migogoro.

Pia ilibainisha kuwa "sheria dhaifu huruhusu wahalifu kutembea huru, na walionusurika hupokea usaidizi mdogo au kutopata kabisa".

Wanawake wanaojihusisha na biashara ya ngono ni miongoni mwa walio hatarini zaidi katika jamii ya Kisomali, kwani wanaepukwa kutokana na maisha yao ambayo ni mwiko, kimsingi yanawafanya kuwa watu waliotengwa.

"Nchini Somalia, wanawake kama sisi hawana mfumo wa usaidizi na hakuna mtu unayeweza kumgeukia. Shinikizo la kijamii linafanya kila kitu kuwa mbaya zaidi, ndiyo maana wengi wa wanawake hawa walio katika mazingira magumu wanasitasita kupata msaada, hasa kama wanakabiliwa na matatizo ya uraibu," Fardousa anaongeza.

Kuna mashirika kadhaa ya wanawake nchini Somalia lakini walipowasiliana na BBC hawakutaka kutoa maoni yao kutokana na unyeti wa somo hilo.

Hodan na Fardousa wanasisitiza kuwa wanawake wengi hawataingia katika kazi hiyo hatari ikiwa mifumo na mashirika yangewasaidia, ambayo mara nyingi yanawapelekea kunaswa katika maisha ya ukatili na unyanyasaji.

"Wasichana wengi wadogo wanapambana na uraibu ambao unawaacha katika hatari zaidi. Wengi wao hawana hata mahali pa kulala usiku," anasema Fardousa.

"Wanakimbilia kulala kwenye mitaa inayozunguka eneo la Lido Beach na maeneo mengine ya jiji, huku wengine wakienda na wanaume kutafuta mahali pa kulala. Kisha wananyanyaswa zaidi kwa ajili ya ngono."

Fardousa anatazama juu na akiwa ameketi nyuma yake ni mwanamke kijana ambaye ameshika mtoto mchanga. Yeye ni mfanyakazi wa ngono wa zamani, Amina, ambaye aliacha baada ya kupata ujauzito.

"Amina huwa ananiambia niache maisha haya [na nirudi nyumbani], lakini si rahisi hivyo. Ni vigumu kuwakabili wapendwa wako. Sijaona familia yangu kwa miaka mitatu."