Jinsi mwanamke aliyesafirishwa kutoka Nigeria mpaka Denmark kufanya ukahaba alivyotoroka

Chanzo cha picha, GUADALUPE BASAGOITIA
Kila mwaka maelfu ya wanawake husafirishwa kimagendo kwenda miji ya Ulaya na kunyanyaswa kingono.
Jewel, mwanamke mwenye umri mdogo kutoka Nigeria aliyekuwa na matumaini ya kuwa mtunza wazee, hatimaye alifanikiwa kutoroka baada ya kupata fursa mara mbili.
"Niliona mwangaza. Sehemu ninatoka ni kama kuna giza kila wakati sababu hakuna umeme…lakini kila kitu hapa kilikuwa kinang'aa. Ilikuwa inapendeza."
Jewel, sio jina lake halisi, anaelezea kuwasili kwake nchini Denmark kwa njia hiyo.
"Nikamshukuru Mungu kwa fursa niliyopata kuja nchi hii. Nilikuwa nataka sana nianze kufanya kazi."
Jewel alipanda ndege kutoka Nigeria akijua kuwa alikuwa anaenda kuwahudumia wazee.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Watu wanaosafirishwa kwa njia za magendo hupitia Libya na mara nyingi wao hutumia mabasi na mashua. Lakini hii ilikuwa imejengwa vizuri hadi hakukuwa na kitu cha kuweza kuzua shaka," anasema.
Shirika la kimataifa la uhamiaji linakadiria kuwa asilimia 80 ya wanawake nchini Nigeria wanasafiri kupitia ardhini kisha wanavuka bahari ya Mediterranea na kusafirishwa kwa biashara za ukahaba barani Ulaya.
Jewel alijua kuhusu wanawake waliotaabika baada ya kufanya safari hiyo hatari, kwa hivyo wakati alianza safari yake kwenye uwanja wa ndege mjini Lagos, alihisi kuridhika.
Mjini Copenhagen alipokewa na mwanamke Mnigeria, aliyempleka kesho yake eneo la Vesterbro mtaa wa madanguro mjini humo.
"Nilitarajia kuona kitu kama hospitali," anakumbuka Jewel.

Chanzo cha picha, Getty Images
Walitembea mitaani kwa muda, na Jewel akafahamu maeneo hayo jinsi alivyoambiwa afanye. Kisha mwanamke huyo akamwambia jambo lililomshitua.
"Akasema, hapa ndio utafanya kazi. Nikatazama kando kuona kama alikuwa ananionesha jengo fulani ambalo sikuwa nimeliona.
Lakini La, alikuwa anamaanisha mahali tulimokuwa tukitembea. Hapo ndipo akaniambia kuwa nitakuwa kahaba na ndipo nitatafuta wateja, nikahisi Denmark yote ilinigeuka."
Usiku huo Jewel alifanya mkutano ambao hakutarajia ambao baadaye ulikuja kuwa wa maana. Michelle Mildwater kutoka HopeNow, shirika lisilo la serikali linalowasaidia watu wanaosafirishwa kimagendo nchini Denmark, alimuona mwanamke huyo mwenye na kumpa kadi yake iliyokuwa na namba ya simu.
'Bosi' wake Jewel Mnigeria, au "Madam" akamwambia asimuamini mwanamke huyo mzungu aliye na baiskeli.
Kisha mteja wake wa kwanza kwa haraka akampata

Chanzo cha picha, Getty Images
"Mwanaume huyo akampa dola 620 ili aende kwenye nyumba yake kisha 'madam' wake akatoka," anasema Jewel.
Tulikaa kwenye gari kwa muda mrefu. Hakuzungumza lugha wakati huo na sikuwa nafahamu alichokuwa akisema. Tulitumia Google kutafsiri ili tupate kuwasiliana.
Miezi iliyofuata, ngono haikuwa rahisi kwa Jewel.
"Hakuwa mzuri kwa hilo. Alikuwa mwanamke mwenye aibu. Lakini kawaida alikuwa na kazi kwa sababu wateja wa kawaida wanajua wakati mtu mpya anakuja na wanataka kujaribu."
Takwimu za hivi punde zilizotolewa na Muungano wa Ulaya kuhusu usafirishaji watu kimagendo ulionesha kuwa kati ya mwaka 2017 na 2018 kulikuwa na zaidi ya waathiriwa 14,000
Hata hivyo idadi hiyo bado ni ndogo sana kwa sababu kesi ambazo hazitambuliwi hazirekodiwi. Nusu walikuwa ni kutoka nje ya Muungano wa Ulaya, na Nigeria ilikuwa moja ya nchi tano za kwanza wanakotoka.
Unyanyasaji wa kingono unaendelea kuwa sababu kuu ya usafirishaji kimagendo wa watu kwa mujibu wa tume ya Ulaya na inakadiriwa kuwa kwa mwaka mmoja mapatano yatokanayo na uhalifu huu hufika dola bilioni16.
Wanawake wanaopata pesa hizi huambiwa kuwa wana deni kubwa la wasafirishaji la usafiri na makazi.
"Kundi la Wanaigeria ni moja ya yale ya wahamiajia walio kwenye biashara ya ukahaba walio na madeni makubwa yanayoweza kuwa kati ya dola 11,000 na 70,000. Na wakati uko na deni la kiwango kama hicho, unahitaji kutafuta pesa kwa haraka. Kama hauna makaratasi yanayokuruhusu ufanye kazi, njia ya haraka zaidi kutafuta pesa ni kwa njia ya ukahaba."
Wasafirishaji wake Jewel walimwambia kuwa angewalipa dola 49,000 kwa malipo ya pole pole.

Chanzo cha picha, JEWEL
Kufanya aelewe zaidi, aliitwa kwenye mkutano wa kutisha katika eneo la makaburi siku moja kabla ya kusafiri kutoka Nigeria.
"Nililazimishwa kuapa kuwa ningelipa deni na kwamba singefichua ni nani alikuwa ananisafirisha. Iwapo ningefanya hivyo vitu vibaya zaidi vingefanyika kwa familia yangu na pia mimi."
Jewel alipokuwa nchini Denmark wasafirishaji wake waliitishia familia yake nchini Nigeria.
"Walikwenda kwenye nyumba yangu na walimtaka bibi yangu asiwe na wazo lolote la kuwaripoti kwa polisi au kukosa kulipa pesa. Kwa hivyo kila nilipompigia simu alilia kwenye simu na kunikumbusha kuwa nilikuwa nimefikia makubaliano nao. Ilibidi nilipe au kitu kibaya kingewapata."
'Wahusika hawawajibishwi'
Aprili mwaka huu wakati wa kutangazwa kwa mikakati mipya ya kupambana na usafishaji watu, Tume ya Ulaya ilikubali kuwa baada ya miaka kumi ya jitihada za kutatua tatizo hilo, sera zilizowekwa zimefeli kwa kiasi kubwa.
Jitihada za kupunguza mahitaji ya huduma zinachangia unyanyasi zilifeli , kwa mujibu wa Tume hiyo.
Serikali ya Uingereza inasema kuwa hadi Machi mwaka 2020 polisi walirekodi matukio ya uhalifu 7,770 yaliyohusu utumwa, ikiwemo ya unyanyasaji wa ajira na ngono. Lakini chini ya watu 250 walishtakiwa mwaka 2019.

Siku za mwishoni mwa juma shirika moja lisilo la serikali hutoa huduma kwa wanawake wanaofanya biashara ya ukahaba.
Kwa mfano Reden International, liko na hoteli ambapo wanaweza kupumzika na kupata kitu cha kula kabla ya kupata wateja wengine
Pia kuna jingine lijulikanalo kama Ren Van kwa sababu kweli limepakwa rangi nyekundu ndani na lina taa nyekundu na pia lina mipira ya kiume na vitambaa.
Ni mahala pa siri ambapo wanawake wanaofanya biashara ya ukahaba hupeleka wateja badala ya kwenda maeneo yaliyo hatari.
Usiku wote wanawake huwaleta wanaume kutumia huduma za gari hilo huku wahudumu wake wakitazama kwa mbali kusikia iwapo mwanamke yule anaweza kujipata kwenye matatizo.
Kwa muda wa saa 4 linaweza kutumiwa mara 28.
Biashara ya ukahaba nchini Denmark sio haramu lakini unahitajika kuwa na leseni ya kufanya kazi.
Baada ya miezi minne mitaani, akiwa amehangaika na mwenye mawazo chungu nzima na jaribio la kujiua, Jewel hakuripoti polisi.
Bado alikuwa na deni kubwa na alihofia usalama wake na wa familia yake nchini Nigeria.

Chanzo cha picha, GUADALUPE BASAGOITIA
Kisha maisha yake yakabadilika. Jewel akakutana na mwaname raia wa Denmark na wakapendana.
Wakati wa mkutano wao wa kwanza Jewel akamwambia kila kitu. Na huyo ndiye mwanaume aliyekuja kuwa mumewe.
Jewel akaondoka mitaani na mwanaume huyo akamsadia kufanya malipo ya kila wiki kwa 'madam'.
Lakini wanandoa hao walihitaji ushauri. Jewel alimfahamu yeyote ambaye angeweza kuwasaidia? akamuuliza mpenzi wake.
Jewel alikuwa na kadi ambayo Michelle Mildwater alimpa siku ya kwanza alipofanya ukahaba huko Vesterbro.
Michelle akamshauri Jewel aache kumlipa madam.
Kwa bahati nzuri hakujatokea vitendo vibaya kwake na familia yake labda huenda wasafirishaji wake si wa kundi kubwa la wahalifu.
Sasa Jewel anasubiri matokeo ya maombi ya kuishi nchini Denmark. Ameifahamu lugha na ana mtoto.
Jewel na Michelle wamekuwa marafiki. Na wakati Jewel alipofunga ndoa, mfanyakazi wa shirika lisilo la serikali la HopeNow alikuwa msaidizi wake.
"Ulikuwa wakati bora zaidi katika maisha yangu," anasema Jewel.
Jewel ana matumaini kuwa siku moja atapata elimu kuhusu biashara.
Pia anataka kujitolea kuwasaidia wanawake walio mitaani.
Kabla ya vizuizi vilivyowekwa kutokana na janga la corona Michelle Mildwater alimshauri Jewel kuandika mchezo wa kuigiza kuelezea maisha ya mwanamke aliyasafirishwa kimagendo kuonesha kwa watazamaji mjini Copenhagen.
















