'Sasa najua jinsi unavyohisi kuwa mwanamke kamili'

Chanzo cha picha, Shamsa Sharaawe
- Author, Bushra Mohamed
- Nafasi, BBC News
- Akiripoti kutoka, London
Onyo: Makala hii ina maelezo ya picha ambayo baadhi ya watu wanaweza kukerwa nayo
"Niliogopa sana wazo la kukatwa tena, ingawa wakati huu ilikuwa kwa idhini yangu. Lakini ilinibidi kufanya hivyo kwa ajili ya afya yangu ya akili.”
Shamsa Sharaawe anazungumzia uamuzi wake wa kufanyiwa upasuaji wa kurekebisha sehemu zake za uke baada ya kukatwa miaka 25 iliyopita, akiwa na umri wa miaka 6 pekee.
Ukeketaji huu wa wanawake (FGM) ulifanywa nchini Somalia na wanafamilia wake wengi na mkunga wa jadi nyumbani.
Zaidi ya wasichana na wanawake milioni 230 wamekeketwa duniani kote, kulingana na ripoti ya hivi karibuni ya Unicef.
Katika Afrika pekee, inasema hii imetokea kwa zaidi ya wanawake na wasichana milioni 140.
Nchini Somalia, Guinea na Djibouti, wasichana wengi hukeketwa - karibu 90% ya watu wote. Ni imani iliyozoeleka katika nchi hizi kwamba FGM itahakikisha ubikira wa msichana mdogo - fadhila ambayo inathaminiwa sana ndani ya nchi.
Wengi katika jamii ya Wasomali wanaamini kuwa ubikira wa wanawake na heshima ya familia yao vina uhusiano usioweza kutenganishwa. Wanaamini kuwa heshima ya familia itasalia kuwepo ikiwa wasichana watafanyiwa ukeketaji.
Wanawake ambao hawakeketwi wanachukuliwa na wengi katika jamii ya Kisomali kama wenye maadili potovu au hamu kubwa ya kufanya tendo la ndoa , ambayo wanaamini inaweza kuharibu sifa ya familia nzima.

Chanzo cha picha, Dr Adan Abdullahi
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Akikua, Shamsa alikuwa anapata maumivu makali kila alipokuwa kwenye hedhi.
"Nilitaka tu kutohisi maumivu tena," asema.
Mwishoni mwa mwaka 2023, akiwa na umri wa miaka 30, Shamsa aliamua kuangalia uwezekano wa kufanyiwa upasuaji wa marekebisho ili kukomesha uchungu wake.
Kufikia wakati huu alikuwa akiishi Uingereza na amekuwa mwanaharakati wa mitandao ya kijamii anayezungumza kupinga ukeketaji.
Ufahamu ambao wanawake wengi katika hali yake hawajui iwapo wanaweza kufanya lolote ili kuboresha maisha yao ulimfanya aazimie kuongeza ufahamu kuhusu upasuaji.
‘’ Hakuna taarifa za kutosha kuhusu upasuaji wenyewe. Ndiyo maana nazungumzia hili,’’ Shamsa anasema.
Upasuaji wa urekebishaji ili kuboresha madhumuni ya utendaji kazi na si kwa ajili ya urembo. Inajumuisha uundaji upya wa sehemu za ndani za uke na kuondolewa kwa uvimbe na tishu za kovu ili kupunguza maumivu na kurejesha maisha ya kawaida ya kushiriki mapenzi kwa mwanamke.
Katika baadhi ya matukio, ufunguzi wa uke pia hutanuliwa na kurudi kwa kawaida.
Baada ya utafiti mwingi, Shamsa alipata njia pekee ya kufanya upasuaji wake mwenyewe ni Ujerumani.
Alianzisha ukurasa wa kuchangisha pesa kupitia jukwaa la mtandaoni la uchangishaji na akafanikiwa kuchangisha $31,000 (£25,000).
Lakini, licha ya ukarimu wa wafuasi wake, ambao baadhi yao hawakuwahi kusikia kuhusu ukeketaji hapo awali, aligundua kwamba bado hakuwa na pesa za kutosha kulipia upasuaji na gharama zake.
Mwishowe, Shamsa alitumia zaidi ya $37,000 (£30,000) kupanga malezi ya binti yake, kusafiri kwa ndege hadi Ujerumani, na kufanyiwa upasuaji huo.
Hili lilimwacha katika deni -na bado ana deni la hospitali ya Euro 3800 (£3,280, $4045)
"Sijaweza kurejea kwenye mashauriano yangu ya matibabu kwa sababu kwa bahati mbaya siwezi kumudu gharama ," anasema Shamsa ambaye bado hajaonana na daktari tangu alipofanyiwa upasuaji.
"Kulipa uharibifu ambao haukujichagulia mwenyewe, au haukuunda sio sawa."

Chanzo cha picha, Dr Reham Awwad
Suluhisho la upasuaji?
Kuna aina nne tofauti za FGM zenye viwango tofauti vya ukali. Aina ya kwanza ni kuondolewa kwa sehemu ya uke au yote. Aina ya pili ni kuondolewa kwa sehemu au sehemu nzima ya ndani (midomo ya ndani inayozunguka uke), na kutolewa kwa (mikunjo ya nje ya ngozi) ya sehemu ya ndani ya uke
Aina ya tatu inahusisha kupunguza mwanya wa uke kwa kutengeneza kizibo, kinachoundwa kwa kukata na kuweka upya sehemu ya ndani ya uke. Aina ya nne, ambayo ni kali zaidi, inahusisha kuondoa kila sehemu ya ndani ya uke na kushona tishu zilizobaki pamoja.
Katika miongo michache iliyopita, madaktari wa upasuaji wameanza kutengeneza mbinu mahususi za matibabu ili kujaribu kurekebisha uharibifu uliofanywa na ukeketaji.
Mnamo 2004, upasuaji wa kwanza wa ukeketaji ulianzishwa na daktari wa magonjwa ya mkojo wa Ufaransa, Dk. Pierre Foldès. Tangu wakati huo, madaktari wengine wa upasuaji wameunda mbinu tofauti za urekebishaji
Hata hivyo, katika Afrika, ambapo mahitaji ni makubwa, upatikanaji wa huduma za upasuaji ni mdogo. Kwa sasa huduma hiyo inapatikana nchini Kenya pekee ambapo wagonjwa wanapaswa kulipa kutoka mfukoni mwao au nchini Misri, ambapo mashirika yasiyo ya kiserikali yanaweza kulipia gharama kwa baadhi ya walionusurika.
Katika bara Ulaya baadhi ya nchi hutoa upasuaji huo kwa gharama ya chini sana. Uundaji upya wa sehemu za uke hulipwa na bima ya afya ya umma nchini Ubelgiji, Ujerumani, Ufaransa, Uswidi, Ufini na Uswizi. Inapatikana pia nchini Uholanzi.
Kulingana na daktari bingwa wa upasauaji wa kurekebisha ukeketaji nchini Kenya, huduma hiyo inazidi kuongezeka katika baadhi ya nchi za magharibi.
"Kuna wapasuaji wachache wa Uropa na Marekani ambao hutoa huduma kwa jamii zilizohamia huko " anasema Dk Adan Abdullahi, daktari wa upasuaji anayeishi Nairobi.
"Lakini si kila daktari wa upasuaji anaweza kufanya upasuaji huu. Ni mgumu na kila mgonjwa ni tofauti.
Dk Abdullahi anasema wanawake wenye kila aina ya ukeketaji wanaweza kufaidika na utaratibu huo, lakini wanawake wanaopata afueni zaidi ni wale walioathirika zaidi.
"Ina athari chanya katika uzazi, hasa kwa aina ya tatu ambayo inahusishwa na kupungua kwa sehemu ya uke," anasema.
Anasema masuala mengine kama vile maumivu wakati wa ngono, yanaweza kuboreshwa kwa kiasi kikubwa au kuponywa baada ya upasuaji, akiongeza kuwa wagonjwa wake mara nyingi hupata hali ya kujistahi "na hisia ya ukamilifu."

Chanzo cha picha, Haja Bilkisu
'Hali ngumu kwa mwili wako'
Haja Bilkisu, raia wa Ujerumani kutoka Sierra Leone, amefanyiwa upasuaji wa kurekebisha ukeketaji mara kadhaa. Anawahimiza waathiriwa wengine kutafiti kwa kina hasa utaratibu wowote unaweza kuhusisha kabla ya kuendelea.
"Kurekebisha sio tu kujenga upya sehemu ya uke," anasema.
"Wanawake wengi waliokatwa wana makovu, wana makovu mazito. Unapaswa kujadiliana na daktari wako. Unawezaje kuondoa makovu? Unaweza kufanya nini ili kufanya sehemu yako iwe sawa zaidi?"
Anaeleza hilo si muhimu sana kwa kujamiiana tu bali pia kwa kuzaa.
Kila moja ya upasuaji wa Haja ilichukua karibu masaa sita kufanya.
"Hiyo ni hali ngumu kwa mwili wako, bila shaka. Umewekwa chini ya anesthesia(Dawa ya kukutia ganzi). Unapaswa kutumia dawa baadaye. Sikuweza kutembea kwa wiki tatu kwa jumla,” anasema.
Kwa sababu ya makali ambayo upasuaji unaweza kuyaleta kwenye mwili wako, madaktari wengine wana nia ya kukuza taratibu zisizo za upasuaji.
Dk Reham Awwad ni mwanzilishi mwenza wa kliniki nchini Misri, Restore, iliyoanzishwa mwaka 2020 ili kutoa matibabu mbalimbali kwa walionusurika ukeketaji.
Dk Awwad anasema alihamasishwa kuanzisha kituo chake cha afya baada ya kukutana na kisa cha ukeketaji alipokuwa bado ni mhudumu wa matibabu. Hii ilimpelekea kukamilisha mafunzo maalum ya upasuaji katika matibabu kwa manusura.
Anasema kwamba ingawa upasuaji unaweza kuleta ahueni, ukeketaji wakati mwingine ni mbaya sana hivi kwamba, hata kukiwa na mbinu za juu zaidi za upasuaji, hakuna mengi yanayoweza kufanywa kurejesha utendaji kazi wake.
"Sidhani kama upasuaji ndio jibu la kila mtu," anasema.
"Kwa kweli tumepunguza idadi ya upasuaji unaohitaji kufanywa."
Dk Awwad anasema kuwa karibu nusu ya wagonjwa wanaotibiwa na kliniki yake sasa wanatumia matibabu yasiyo ya upasuaji kuongeza mtiririko wa damu katika eneo hilo. Hii ni pamoja na matibabu ya kisaikolojia ili kupambana na kiwewe kwa wanawake wanaokatwa sehemu za siri katika umri ambao wanaweza kukumbuka masaibu hayo.
Anaelezea kuna taratibu chache ambazo zinaweza kujaribiwa ambazo si za upasuaji - kama vile plasma yenye wingi wa chembe chembe za damu, mchakato unaotumika sasa katika nyanja mbalimbali za matibabu.
"Plazima [inaweza] kusababisha kuzaliwa upya na kusisimua kwa kuongezeka kwa mtiririko wa damu na kupunguza uvimbe katika maeneo unayoidunga," anasema, ingawa anatahadharisha kuwa gharama ya matibabu haya inamaanisha kuwa hazipatikani kwa wengi wanaohitaji.

Chanzo cha picha, BBC
Mwili mpya
Kwa wale wanaochagua upasuaji wa marekebisho, matokeo yanaweza kuwa yenye kihisia.
Kwa Haja kutoka Sierra Leone, ilichukua muda kuuzoea mwili wake mpya.
‘’Mara ya kwanza nilipoona uke wangu nilijawa na hisia kwa sababu kwangu ilikuwa kama hii sio yangu,” anasema.
“Nilikeketwa nikiwa na miaka minane. Sikuwahi kutazama sehemu hiyo ya mwili.’’
Sasa katika ahueni, Shamsa anasema licha ya madeni yake, anafurahi kwamba aliwekeza katika upasuaji huo.
"Nilipopata nafuu, ilinibidi kujifunza jinsi ya kuishi na sehemu yangu mpya ya uke " anasema.
"Lakini sasa najua jinsi unavyohisi kuwa mwanamke kamili."
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah na kuhaririwa na Seif Abdalla








