BBC Africa eye: 'Ukeketaji ulimuua mpenzi wangu'
Na Tamasin Ford, BBC Africa Eye

Chanzo cha picha, Getty Images
Sierra Leone ni moja ya nchi zenye viwango vya juu zaidi vya ukeketaji wa wanawake (FGM) barani Afrika na viwango ambavyo wakati mwingine vitendo hivyo vinasababisha athari kubwa. BBC Africa Eye imekuwa ikisikia kutoka kwa mmoja wa wanaume anayeamini kuwa mpenzi wake alifariki baada ya kukatwa sehemu zake za siri.
Fatmata Turay alikuwa na umri wa miaka 19 mama yake alipomwita aende nyumbani huko kijijini kwao.
Alipaswa kushiriki utamaduni wa Bondo, ambao ni utamaduni wa karne nyingi unaohusisha nyimbo, kucheza ambapo mabinti wadogo wanatayarishwa na kuandaliwa kuingia utu uzima.
Lakini saa thelathini na sita baadaye, Fatmata alifariki dunia.
Kuanzia siku ya mazishi yake tarehe 18 Agosti 2016, mpenzi wake, mwandishi wa habari Tyson Conteh, alitumia kamera yake kurekodi matukio yote muhimu.
Baadaye kabisa huku akiitazama lensi ya camera anakuja kueleza ni kwa nini alitaka kutunza kumbukumbu ya kile kilichokuwa kikitokea.
"Nataka kutumia filamu hii ambayo inanivutia sana kuibua mjadala. Fatmata hataki kuona msichana mwingine, binti akifa. Hayo ni matakwa yake."
Alisema Fatmata amekuwa akiongea naye katika ndoto, na kumtaka afichue ukweli wa kifo chake na kukomesha mila ya ukeketaji.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ukeketaji unahusisha uondoaji wa sehemu ya siri ya nje ya mwanamke yote ama sehemu tu fulani, mara nyingi kinachoondolewa ni kisimi.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu limetaja mila hiyo kuwepo katika nchi 92, lakini imeenea zaidi katika sehemu za Afrika na Mashariki ya Kati.
Katika nchi kama Somalia, Sudan na Djibouti, aina ya ukeketeji (FGM) inayofanyika sana inaitwa 'infibulation' ambapo labia hutolewa na kisha kutumika kuziba kabisa tundu la uke, na kuacha mwanya mdogo ili kupitisha haja ndogo na damu ya hedhi. Inapofika mwanamke kuolewa, lwanalazimika kukatwa tena ili kuruhusu na kumuwezesha kuingiliwa na mumewe.
Hakuna faida za kiafya za ukeketaji (FGM). Shirika la Afya Duniani linaonya kuwa inaweza kusababisha matatizo katika mfumo wa haja n dogo, uke na hedhi, matatizo mengine wakati wa kujifungua na wakati mwingine kifo.
Nchini Sierra Leone, inakadiriwa kuwa asilimia 83 ya wanawake na wasichana wenye umri kati ya miaka 15 na 49 wamekeketwa.
Moja ya sababu kuu za utaratibu au utamaduni huu unaopigwa vita ni kupunguza hamu ya ngono ya wanawake. Ikiwa "watakatwa" ama kukeketwa, inadhaniwa italinda ubikira wao na mara tu watakapoolewa, watabaki waaminifu kwa mume zao.
"Mwanamke ambaye hajakeketwa anapenda sana ngono kuliko mwanamke aliyekeketwa. Ndio maana tunapunguza hamu kwao," alisema Aminata Sankoh, au Soweis, jina analopewa wanawake wanaofanya shughuli ya kukeketa mabinti huko Sierra Leone.
'Ilinichukua wiki kupata haja ndogo'
Conteh alipata nafasi adimu ya kutengeneza filamu kuhusu utamaduni wa Bondo, msingi wa zamani wa urembo, sanaa na tamaduni.
Ni sherehe ambapo mabinti hufundishwa kuhusu jukumu la kitamaduni la kuwa mke na mama kutoka kwa wazee wa Bondo.
Inachukuliwa kama ibada ya lazima kwa kila binti kupitia.
Hata hivyo, sehemu ya mchakato wa utamdani huo wa unyago vitendo vya ukeketeaji hufanyika. Conteh hakuruhusiwa kurekodi vitendo hivyo kwenye filamu yake.

"Katika utamaduni wetu, watu wetu kwa muda mrefu wamekuwa wakifanyiwa utamaduni huu katika jamii," alisema Ngaima Kamara, kiongozi maarufu wa Soweis.
“Usipopitia hili utaona aibu kufua na mimi mtoni, nikipita karibu yako nitakupuuza, tukikutana mahali nakwambia siongei na mwanamke ambaye hajakeketwa kama wewe, ni mgonjwa."
Katika filamu ama makala yake, Conteh alisimulia zaidi yaliyompata Fatmata siku moja baada ya kuhudhuria sherehe ya Bondo.
"Tuliukuta mwili wake ukiwa umelazwa kwenye mkeka, nje kidogo ya nyumba kwenye sakafu. Na ulikuwa umepakwa vitu vyeupe na kufunikiwa kwa rangi nyeupe," alisema.
"Unaona damu inatoka. Unaona kama kuna damu na tukagundua kuwa alikufa katika Bondo baada ya kukeketwa."
Polisi walifika na mwili wa Fatmata ukapelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti kilichopo Makeni.
Mama yake Fatmata na Soweis (mkeketaji) walikamatwa.
Siku sita baadaye, uchunguzi wa maiti ulifanywa na mwanapatholojia pekee wa Sierra Leone wakati huo, Dk Simeon Owizz Koroma.

Pia alikuwepo Dk Sylvia Blyden, waziri wa wakati huo wa maendeleo ya jamii, jinsia na masuala ya watoto.
Dk Blyden alikuwa akiunga mkono haki za wanawake watu wazima ambao kwa hiyari yao wameamua kukeketwa lakini anapinga vikali ukeketaji kwa watoto wadogo na wa kulazimishwa.
Katika taarifa yake kwa umma wakati huo, alitoa maelezo ya uchunguzi wa mwili wa Fatmata na kusema ukeketaji hauna uhusiano wowote na kifo cha Fatmata. Baadaye Soweis na Mama yake Fatmata waliachiliwa huru.
Conteh alichunguza uwezekano wa iwapo kifo cha mpenzi wake kilifichwa ili kulinda utamaduni wa Bondo. Dk Blyden anasisitiza kuwa haweza kuwa na mbadala wa ukweli wa sifa ya Bondo.
Rugiatu Turay (hana uhusiano na Fatmata Turay), alikuwa naibu waziri wa Dkt Blyden wakati huo alikuwa mwanaharakati wa muda mrefu dhidi ya ukeketaji.
Alianzisha na kuendesha Amazonian Initiative Movement, Shirika nchini Sierra Leone lililolenga kukomesha ukeketaji.
Alisema alikuwa na bahati ya kuishi baada ya kukeketwa akiwa na umri wa miaka 11.
"Watu wengi wamekufa. Tunajua, sote tunajua. Tunapaswa kuwa wakweli," alisema.
"Almanusura nife. Ikiwa nilitaka kukojoa. Ilinichukua wiki moja kuweza kujisaidia haja ndogo. Wiki moja. Hata baada ya shughuli ya kufundwa kumalizika, uke wangu ulivimba."
'Bondo itaisha'
Bi Turay alihoji kwa nini Dkt Blyden alikuwepo kwenye uchunguzi wa maiti.
“Kwanini unamruhusu waziri wako aingie chumba cha kuhifadhia maiti kufanya uchunguzi wa maiti hata kama daktari, hilo sio jukumu lake.
"Alikuwa upande wa Soweis. Hiyo inaonyesha kwamba tayari aliunga mkono upande fulani. Tunaamini kwamba matokeo, ambayo hatujawahi kuyaona, yalibadilishwa. Tunaamini hivyo. Hatuwezi kujadili maisha ya wanawake kwa ajili ya kura."
Dk Blyden alikanusha kuongea hadharani kuhusu chanzo cha kifo cha Fatmata lakini anasimama na madai yake kwamba Fatmata hakufa kutokana na ukeketaji, akisema matokeo ya uchunguzi wa mwili wake yanalingana na historia ya matibabu ya Fatmata.
Alisema hoja kwamba ukweli unafichwa ni uwongo na lina nia ovu na kuongeza kuwa uchunguzi wa mwili wake ulifanyika mbele ya macho ya familia, mashirika ya haki za binadamu, polisi na wafanyakazi wa matibabu.
Alidai kuwa ilikuwa ni wajibu wake kama waziri kuhudhuria uchunguzi wa mwili huo na akakana kuwa alifanya hivyo kwa ajili ya kujinufaisha kisiasa.
BBC Africa Eye ilimfuata Dk Owizz kuhusu masuala mbalimbali katika filamu hiyo, lakini alikataa kuzungumzia.
Miaka minne iliyopita, Bi Turay alianzisha sherehe ya kwanza ya Bondo bila ukeketaji, inayoitwa Alternative Rites au Bloodless Bondo.
Anaamini kuwa Bondo yenyewe inaweza kuisha ikiwa wanawake wataacha ukeketaji.
"Kama wanawake au mtu yeyote ataendelea kutetea ukeketaji huko Bondo, itafikia wakati Bondo itaisha. Itafikia wakati Bondo itakoma."












