Marufuku kuyatembelea maeneo haya duniani

Muda wa kusoma: Dakika 4

Kwa watalii ulimwenguni, hakuna sehemu nyingi zilizobaki ambazo hawajazitembelea, kuzisikia, au kusisitiziwa kwa 'hashtag' kuzuru maeneo hayo.

Lakini haijalishi umetalii kiasi gani, bado kuna maeneo ambayo hujayafika. Ingawa sehemu nyingi za dunia ziko wazi kwa watalii na wageni, kuna maeneo ambayo umma kwa ujumla hauruhusiwi kufika.

Marufuku hii inatokana na masuala ya usalama na kisheria au sababu za kisayansi, lakini kinachofanana ni kwamba ni marufuku kutembelea maeneo hayo yote.

Hifadhi ya mbegu ya kimataifa ya Norway

Kunapotokea janga la kimataifa, wanadamu na wanyama wako katika hatari ya kupoteza maisha na kuharibu mazao muhimu ya kilimo.

Kwa bahati nzuri, kuna Global Seed Vault, jengo kubwa zaidi la uhifadhi wa mbegu ulimwenguni kote lililojengwa nchini Norway mwaka 2008.

Ikiwa kwa sababu fulani dunia italazimika kupanda mazao yake yote tena, mbegu zilizohifadhiwa katika hifadhi hii zitasaidia pakubwa.

Mbegu hizi huwekwa kwenye vyombo maalum na kufungashwa kwa njia ya kuzilinda dhidi ya unyevu.

Hifadhi hiyo iko kwenye kisiwa cha mbali zaidi katika visiwa vya Svalbard nchini Norway, Spitsbergen.

Ipo kwenye kina cha mita 120 kwenye mlima ulio takriban kilomita 1,300 kutoka Ncha ya Kaskazini na mita 130 juu ya usawa wa bahari.

Katika hali kama hizi, siku zote linasalia kuwa kavu, na barafu nene, ya kudumu inayozunguka husaidia kuhifadhi mamia ya maelfu ya sampuli za mbegu zilizohifadhiwa.

Sababu nyingine eneo hili lilichaguliwa ni kwamba hakuna tetemeko la ardhi linaloweza kutokea eneo hili.

Mbegu zinahifadhiwa na kutunzwa kwa kufuata mipango mizuri iliyowekwa lakini hakuna wageni wanaruhusiwa kutembelea mahali hapa.

Hifadhi hiyo inapewa ulinzi wa juu ili mbegu zilizo ndani ziweze kubaki humo kwa maelfu ya miaka ikiwa kutakuwa na ulazima wa kufanya hivyo.

Pia unaweza kusoma:

'Ilha da Queimada Grande,' au Kisiwa cha Nyoka

Kisiwa hiki chenye ukubwa wa hekta 43 karibu na pwani ya Brazil si mahali ambapo watalii wangependekezwa kuzuru.

Ni nyumbani kwa nyoka mwenye sumu anayeitwa 'golden lancehead viper' ambaye sumu yake ni kali sana hivi kwamba inaweza kuua ndege anayemwinda.

Inakadiriwa kuwa kuna wastani wa nyoka watano kwa kila mita ya mraba ya kisiwa hicho, na ndiyo maana serikali ya Brazil hairuhusu mtu yeyote kuingia eneo la Ilha da Queimada Grande, linalojulikana kama 'Snake Island', ikiwa ni mbinu ya kuonyesha tahadhari.

Kuingia kwenye kisiwa kunaruhusiwa tu kwa wanasayansi na watafiti, na lazima waambatane na daktari ili kusafiri kwenye kisiwa hicho.

Wale wanaopenda kutazama aina hii ya nyoka wanaweza kufanya hivyo mahali pengine huko Brazil, ambapo wanahifadhiwa katika vituo maalum.

Pango la Lascaux huko Ufaransa

Mnamo mwaka1940, vijana wanne waliokuwa wakitafuta mbwa wao aliyepotea kwenye shimo waligundua pango la Lascaux kusini mwa Ufaransa.

Katika tukio hili la bahati nzuri, kupoteza mbwa wao kuliwapeleka kwenye pango lililojaa michoro ya wanyama kama vile farasi na kulungu.

Kazi hizo zina zaidi ya miaka 17,000 na ni mojawapo ya mifano ya kazi bora zaidi zilizohifadhiwa za sanaa ya kabla ya historia, ikiwa na jumla ya michoro 600 na mingine 1,000 iliyopo pangoni.

Pango hilo lilipogunduliwa, Vita vya Pili vya Dunia vilikuwa vimeanza tu. Miaka minane baadaye, Pango la Lascaux lilifunguliwa kwa wageni ili waweze kuona michoro ya mababu zao kwa karibu.

Mnamo 1963, pango la Lascaux lilifungwa kwa umma kwa sababu ya ukuaji wa ukungu kwenye kuta za pango.

Hii ilikuwa tishio kwa michoro hiyo ambayo ilikuwa imehifadhiwa hadi ugunduzi wake. Ukungu uliendelea kukua hata baada ya idadi ya wageni kuwa ndogo.

Baada ya miaka 60 ya tukio hili, wageni hawakuruhusiwa kuingia ndani ya pango hilo, lakini pango kama hilo limetengenezwa karibu na hilo kwa watalii kutembelea.

Uluru, mahali patakatifu katika jangwa la Australia

Uluru, pia inajulikana kama 'Ayers Rock', ni mwamba ambao umekuwa kivutio cha watalii nchini Australia kwa miaka mingi, lakini hivi karibuni sehemu hiyo imeongezwa kwenye orodha ya maeneo ambayo ni marufuku watu kuyatembelea.

Wageni na watalii hapo awali wameweza kupanda kilele cha mita 348, ingawa katika majira ya joto hii ilimaanisha kustahimili joto kali la karibu nyuzi joto 47 na kupanda juu ya miinuko haikuwa rahisi.

Uluru ni eneo takatifu kwa watu wa Anangu, ambao wanatunza mwamba huo na kwa muda mrefu wametaka wageni kuepuka kuupanda kwa kuheshimu imani zao.

Ombi hili liliungwa mkono na ombi kutoka kwa wasimamizi wa Hifadhi ya Kitaifa ya Uluru-Kata Tjuta, na uamuzi wa kupiga marufuku wageni kulizuru ulifanywa mnamo 2017.

Mnamo tarehe 25 Oktoba 2019, watalii wa siku ya mwisho waliruhusiwa kupanda mwamba huo kabla ya marufuku ya jumla, foleni ndefu ya watalii wenye hamu ya kuupanda walipewa fursa ya mwisho kufanya hivyo.

Katika utamaduni wa Anangu, Uluru ni ishara ya kuwepo kwa viumbe vya kufikirika kwenye ardhi ambayo ilikuwa bado haina chochote na haikuwa na viumbe wenye maisha.

Viumbe wa kufikirika walipitia eneo hilo wakiunda vitu vingine katika maeneo mbalimbali njiani, kama mwamba wa Uluru.

Wageni bado wanaweza kuja kwenye Hifadhi ya Kitaifa ya Uluru-Kata Tjuta, lakini wanaweza tu kuona mwamba mtakatifu kwa mbali na hawaruhusiwi kuukanyaga.