Kwanini Marekani ndio inayoongoza kwa utalii 2024?

    • Author, Lindsey Galloway
    • Nafasi, BBC

Baada ya changamoto ya usafiri kutokana na janga la corona, watalii wa kimataifa wanatarajiwa kufikia viwango vya kabla ya janga la uviko 19 mwaka 2024.

Hata hivyo kukua kwa safari za kimataifa ni jambo ambalo bado halina uhakika, kutokana na mfumuko wa bei, mabadiliko ya tabia nchi na mivutano ya kijiografia, ambayo inaiweka sekta hiyo katika hali mbaya.

Lakini baadhi ya nchi na serikali zimefanya kazi za ziada kupunguza hatari hizo na kuongeza uwezo wa usafiri na utalii, kulingana na Travel & Tourism Development Index 2024 na Jukwaa la Uchumi la Dunia.

Orodha hiyo inazingatia nchi zote ulimwenguni kwa kutazama mambo kama vile usalama na ulinzi, kipaumbele cha usafiri na utalii, miundombinu ya usafiri wa anga na ardhini, maliasili na utamaduni.

Viwango vya mwaka huu vimeiweka Hispania, Japan (mshindi wa mwaka jana), Ufaransa na Australia katika tano bora, na Marekani ikiwa kileleni.

Kwanini Marekani imeshinda?

Marekani imeshinda kimataifa kutokana na mazingira yake ya biashara, miundombinu ya usafiri wa anga na maliasili.

Ushindi huja kutokana na miundombinu imara ya nchi, urahisi wa kusafiri kati ya miji, maeneo mbalimbali ya asili na kitamaduni na nyenzo zinazofaa wasafiri, kama vile miongozo ya miji, bustani na vivutio vingine.

Serikali ya shirikisho ya Marekani inatoa usaidizi wa usafiri na utalii, kwa kudumisha miundombinu imara ya viwanja vya ndege na sekta ya ndege.

Matukio makubwa ya kimataifa ya Marekani - kama Coachella, Super Bowl na Mardi Gras - pia huvutia wageni kutoka duniani kote.

Hifadhi za Kitaifa za Marekani, mbuga zake 63 zenye ekari milioni 54 (ambazo ni karibu ukubwa wa Uingereza nzima), huongeza mvuto wake wa kimataifa.

"Marekani imebarikiwa kuwa na mandhari na miji ya kuvutia kuliko nchi yoyote duniani, kuanzia milima, majangwa, maeneo ya kitropiki na kinamasi," anasema Tim Leffel, mwandishi wa kitabu The World's Cheapest Destinations.

Nchi 10 bora kwa utalii

• Marekani

• Uhispania

• Japani

• Ufaransa

• Australia

• Ujerumani

• Uingereza

• China

• Italia

• Sweden

Chanzo: World Economic Forum's Travel & Tourism Development Index 2024

Mbinu za Marekani

"Moja ya mambo yanayosukuma mafanikio ya sekta ya usafiri nchini Marekani ni juhudi za ushirikiano kati ya mashirika ya utalii ya ndani, kikanda na serikali," anasema Danielle Borja, Rais/Mkurugenzi Mtendaji wa Visit Conejo Valley.

Mashirika ya utalii kama haya mara nyingi hushirikiana na biashara binafsi kama vile migahawa na vivutio vinavyomilikiwa na watu binafsi.

Wageni zaidi inamaanisha matumizi makubwa katika mikahawa ya ndani, maduka na hoteli. Kushamiri kwa utalii huleta ajira na fursa zaidi kwa jamii.

Kulingana na Leffel, mafanikio ya utalii Marekani yanatokana na maadili mazuri ya kazi, ufanisi katika ushirikiano na mawasiliano ya kuaminika.

''Bodi za utalii za Marekani zinawajibu waandishi wa habari, wanafuatilia masoko, wanakwenda kwenye makongamano ili kuboresha kazi zao na kutafuta watu wa kushirikiana nao,” anasema Leffel.

"Wanangalia mafanikio ya wengine. Wanaangalia nje nje ya mipaka yao mara kwa mara na hawabaki kuridhika na wasafiri wa ndani tu," ameongeza.

Ofisi za wageni zilizo na makao yake nchini Marekani na mashirika ya usimamizi wa wageni pia huwa na vituo vya taarifa ambavyo hufanya kazi kidijitali.

Mafunzo na elimu kwa wataalamu wa utalii yamekuwa yakibadilika kulingana na mahitaji na mwelekeo wa sekta hiyo.

Teknolojia mpya za akili mnembe (AI) zinatarajiwa kubadilisha jinsi wasafiri wanavyotafiti na kusafiri - na Marekani kwa kawaida huwa mbele kama mtumiaji wa teknolojia mapema kuliko nchi nyingine.

Mafunzo pia yameimarishwa na usaidizi katika sekta ya utalii, haswa na mashirika kama vile Brand USA na USTA, ambayo hufanya kazi kukuza vivutio vya utalii na kushauri kuhusu viza na sera za kuingia.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na lizzy Masinga.