Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Nini chanzo cha mzozo unaokua kati ya Iran na Israel?
- Author, Na Yusuph Mazimu
- Akiripoti kutoka, BBC Dar es Salaam
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Mashambulizi ya hivi karibuni yanayoripotiwa kufanywa na Israel dhidi ya Iran yamezua taharuki kubwa duniani, yakionesha wazi undani na hatari ya mzozo wa muda mrefu kati ya mataifa haya mawili yenye ushawishi mkubwa Mashariki ya Kati.
Milipuko mikubwa ilisikika kote Tehran siku ya Ijumaa Juni 13, 2025, huku Israel ikitangaza kuwa imelenga maeneo ya nyuklia na vituo vya kijeshi.
Mashambulizi hayo pia yalipiga mji wa Kermanshah magharibi mwa Iran, ambapo wakazi walisema walisikia milipuko na kuona moshi mweusi ukipanda juu ya jiji. Haikubainika mara moja ni nini hasa kililengwa. Milipuko pia ilisikika karibu na mji wa Tabriz nchini Iran, ingawa hali halisi huko bado haijawa wazi.
Ili kuelewa kinachoendelea leo, ni muhimu kurudi nyuma na kuchunguza mizizi ya uhasi na mzozo huu, ambao umejengeka juu ya historia tata, siasa za kikanda, na tofauti za kiitikadi.
Mizizi ya kihistoria ya mzozo
Awali, kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ya mwaka 1979, Israel na Iran zilikuwa na uhusiano mzuri na wa kimkakati. Iran chini ya Mohammad Reza Pahlavi, ilikuwa mshirika muhimu wa Marekani na Israel katika kudumisha utulivu Mashariki ya Kati.
Hata hivyo, mapinduzi ya kiislamu yaliyomleta Ayatollah Ruhollah Khomeini madarakani yalibadilisha kabisa sera ya nje ya Iran. Serikali mpya ilipitisha itikadi ya kupinga Uzayuni na kuitambua Israel kama "taifa haramu la Kizayuni" lililochipua katika ardhi ya Kiislamu. Kuanzia hapo, Israel ilianza kuonekana kama adui namba moja, na mzozo wa Palestina ukawa kiini cha sera ya kigeni ya Iran.
Mpango wa nyuklia wa Iran tishio la kudumu?
Mojawapo ya vyanzo vikuu vya mzozo baina ya nchi hizi ni mpango wa nyuklia wa Iran. Israel, pamoja na washirika wake kama Marekani, ina hofu kubwa kwamba Iran inatumia mpango wake wa nyuklia kwa malengo ya kijeshi, ikikusudia kutengeneza silaha za nyuklia. Kwa Israel, ambayo inajiita taifa la Wayahudi, tishio la Iran kuwa na silaha za nyuklia linaonekana kama tishio la kuwepo kwake. Inahofu mpango huo huenda ni kwa ajili ya kuisambaratisha.
Kwa mantiki hiyo, haishangazi mashambulizi haya mampya ya anga yalilenga maeneo yenye kufanyika michakato ya nyuklia. Baada tu ya mshambulizi, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alisema kuwa Israel ililenga kituo kikuu cha kurutubisha urani huko Natanz na mpango wa kombora la balistiki la nchi hiyo, pamoja na wanasayansi wakuu wa nyuklia na maafisa.
Makubaliano ya nyuklia ya 2015 (JCPOA - Joint Comprehensive Plan of Action), yaliyolenga kuzuia Iran kutengeneza silaha za nyuklia kwa kubadilishana na kulegeza vikwazo, yalitoa matumaini kidogo.
Hata hivyo, kujiondoa kwa Marekani kuika makubaliano hayo mwaka 2018 chini ya utawala wa Donald Trump wakati huo kuliufanya mpango huo kudhoofika. Tangu wakati huo, Iran imeongeza kiwango chake cha urutubishaji wa urani, na ripoti za Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) zimeonesha wasiwasi mkubwa, zikizidi kuongeza hofu ya Israel na washirika wake.
Jumanatono wiki hii bodi ya magavana ya Shirika la kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) iliilaani Iran kwa mara ya kwanza katika miaka 20 siku ya Alhamisi baada ya nchi hiyo kukataa kushirikiana na wakaguzi.
Mara baada ya hapo, Iran ilitangaza mara moja kuwa itaanzisha kituo cha tatu cha kurutubisha urani nchini humo na kubadilisha baadhi ya mipango kuwa ya kisasa zaidi.
IAEA) imethibitisha pia kuwa shambulizi la Israel la sasa limelenga kituo cha kurutubisha urani cha Iran huko Natanz. Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa X, Mkuu wa IAEA, Rafael Mariano Grossi, alinukuliwa akisema: "IAEA inafuatilia kwa karibu hali inayoendelea nchini Iran. ... Shirika lina mawasiliano na mamlaka za Iran kuhusu viwango vya mionzi. Pia tuko katika mawasiliano na wakaguzi wetu nchini humo."
Vita baridi ya mamlaka ya kikanda (Proxy Wars)
Mbali na mpango wa nyuklia, Iran na Israel zinapigana "vita baridi" ya mamlaka katika eneo lote la Mashariki ya Kati. Iran inaelezwa imejenga mtandao mpana wa vikundi inavyoviunga mkono kama vile Hezbollah nchini Lebanon, Hamas na Islamic Jihad huko Gaza, na Houthis nchini Yemen) ikivipa silaha, fedha, na mafunzo. Lengo la Iran ni kuimarisha ushawishi wake na kuunda "ukanda wa upinzani" dhidi ya Israel na Marekani.
Israel inapinga vikali ushawishi huu, ikiona vikundi hivi kama vitisho vya moja kwa moja kwenye mipaka yake. Hali hii imesababisha Israel kufanya mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya maeneo yanayohusishwa na Iran na Hezbollah nchini Syria na Lebanon. Vita hivi baridi vya nyuma ya pazia mara nyingi hujumuisha mashambulizi ya kimtandao (cyber attacks), mauaji yaliyolengwa ya wanasayansi au maafisa wa kijeshi, na operesheni za kijasusi.
Mtazamo wa kiitikadi, kidini na kujiweka kando kwa Marekani
Inatajwa pia sababu ya tofauti za kiitikadi na kidini pia zinachochea mzozo huu. Iran inafuata Uislamu wa Kishia na inaongozwa na serikali ya kidini inayoamini katika mapambano dhidi ya ubeberu na Uzayuni. Kwa upande mwingine, Israel inajitambulisha kama taifa la Wayahudi, likiwa na mizizi mirefu ya kidini na kihistoria katika eneo hilo.
Uwepo wa Yerusalemu na msikiti wa Al-Aqsa, ambao ni patakatifu kwa waislamu na wayahudi, pia linazidisha mvutano wa kidini na kisiasa.
Jambo lingine, Marekani imekuwa mshirika mkuu wa Israel, ikitoa msaada mkubwa wa kijeshi na kisiasa. Kujiondoa kwa Marekani chini ya Rais Donald trump kwenye JCPOA kulichochea Iran kuanzisha tena shughuli zake za nyuklia zilizokuwa zimesitishwa, na hivyo kuzidisha wasiwasi wa Israel.
Mataifa mengine ya Ulaya na mataifa ya Kiarabu yenye msimamo wa wastani pia yana wasiwasi juu ya mpango wa nyuklia wa Iran na ushawishi wake wa kikanda, lakini yanatofautiana kuhusu njia bora za kukabiliana na vitisho hivyo. Juhudi za kidiplomasia za kupunguza mvutano zimekuwa changamoto kubwa, hasa kutokana na ukosefu wa imani kati ya pande zote zinazopingana.
Kwa mashambulizi ya Ijumaa Juni 13 aliyofanywa na Israel nchini Iran yanaashiria hatua hatari zaidi ya kuzidisha mzozo huu wa muda mrefu. Katika mazingira haya tete, uwezekano wa kutokea kwa mgogoro mkubwa wa wazi unaongezeka, ukiwa na athari kubwa kwa Mashariki ya Kati na ulimwengu mzima.
Imeandaliwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali