Raman Raghav: Muuaji aliyeachiwa na Polisi na kwenda kuua watu wengi zaidi

Chanzo cha picha, LILY KULKARINI
Katika jiji la Mumbai - Raman Raghav aliua watu tisa. Aliwaambia polisi kwamba alifanya mauaji hayo. Lakini, polisi walifikiri afya yake ya akili haikuwa nzuri na alikuwa akijisemea tu. Lakini miaka ya baadaye, aliifanya Mumbai na nchi nzima kutetemeka – aliuwa watu 40.
Bila silaha zozote za kisasa aliwaua kikatili watu wasio na hatia kwa kuwapiga kwa mawe vichwani. Aliwapiga baadhi yao hadi kufa kwa vitu vya chuma.
Kumekuwa na filamu na sinema kuhusu mauaji yake ya kikatili na ya kinyama. Muuaji huyo aliwaambia polisi kwamba Mungu ndiye aliyemwamuru kufanya mauaji ya kikatili. Mambo mengi aliyowaambia polisi yaliandikwa katika magazeti ya wakati huo.
Mauaji ya Kikatili

Chanzo cha picha, LILY KULKARNI
Unaweza kukumbuka jinsi Mumbai ilivyokuwa wakati huo kwenye sinema za zamani za miaka ya 1960. Ingawa haikuwa na watu wengi kama ilivyo leo, bado lilikuwa jiji kubwa. Watu walikuwa wakija hapa kutoka kila pembe ya nchi.
Kati ya 1965-66 watu kadhaa katika njia za watembea kwa miguu na vibanda vilivyo karibu na barabara waliuawa mfululizo. Watu wasiojulikana walikuwa wakivamia watu waliolala katika maeneo ya wazi gizani. Jumla ya watu 19 wanaoishi karibu na njia ya Reli ya Kati ya GIP walishambuliwa siku moja na 9 kati yao walikufa papo hapo.
Awali polisi walishuku kuwa mtu fulani aliyechanganyikiwa anaweza kuwa alifanya mauaji hayo. Lakini hakuna hata mmoja kati ya manusura wa shambulio hilo aliyewaona washambuliaji wao. Kwa hiyo ilikuwa vigumu sana kumtambua mhalifu.
Uchunguzi ulianzishwa juu ya mashambulizi haya. Polisi pia walikuwa wakishika doria nyakati za usiku. Siku chache baadaye, polisi walimkamata mtu anayeitwa Raman Raghav. Lakini polisi wakamwachilia kutokana na ukosefu wa ushahidi.
Baada ya miaka miwili

Chanzo cha picha, LILY KULKARNI
Miaka miwili baadaye Raman Raghav yuleyule almaarufu 'Sindhi Dalwai' almaarufu 'Thambi' almaarufu 'Anna' almaarufu 'Veluswami' alirudi Mayanagar na kuwaua kikatili watu maskini wasio na hatia.
Katikati ya 1968, mauaji yalianza tena kutokea katika mitaa ya Mumbai. Mwanamume mmoja alianza kuwapiga watu wasio na hatia waliolala barabarani kwa zana nzito vichwani.
Ingawa rekodi za polisi zinasema Raman Raghav almaarufu Sindhi Dalwai alifanya mauaji ya watu 24, idadi halisi ilikuwa kubwa zaidi kwenye vyombo vya habari. Kesi hiyo ilikuja mikononi mwa Ramakant Kulkarni, afisa wa polisi mchanga aliyeteuliwa karibuni.
Ramakant Kulkarni kisha alistaafu kama Mkurugenzi Mkuu wa Polisi wa Maharashtra. Baada ya kustaafu, aliandika kitabu 'Footprints on the Sand of Crime.' Imeandikwa kwa kina jinsi Raman Raghav alivyokamatwa katika kesi ya mauaji.
Alivyokamatwa tena
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ramakant Kulkarni alipokagua rekodi za polisi za Mumbai, aligundua kuwa mwanamume mmoja alikuwa amezuiliwa kwa mahojiano kuhusiana na mauaji ambayo yalifanyika miaka miwili iliyopita.
Jina la mtu huyo ni Raman Raghav. Ramakant Kulkarni alionyesha shaka kwamba anaweza kuwa mshtakiwa katika kesi ya sasa pia. Kwa hiyo, uchunguzi ulianza. Lakini Raman Raghav alijulikana kwa majina mengi wakati huo.
Kwa kuwa ni mhalifu wa mitaani, hakuna uwezekano wa kuwa na anuwani ya makaazi. Haikuwa rahisi kupekua jiji lote la Mumbai siku hizo kumtafuta mtu ambaye anazurura mitaani. Wakati huo huo hawana ushahidi thabiti dhidi ya Raman Raghav.
Hata hivyo, Raman Raghav mwishoe alikamatwa na polisi. Inspekta Alex Fialow aliiambia 'Crime Wire' jinsi Raman Raghav alivyokamatwa.
"Nilikuwa na mchoro wa muuaji mfukoni mwangu. Nilikuwa nikisubiri basi la kwenda kituo cha polisi siku hiyo. Muda huohuo akaja mtu mmoja akiwa amevalia kaptura ya kaki na shati la bluu, sawa na mtu aliye kwenye mchoro,'' alieleza Fialo.
"Alionekana akiwa na mwamvuli, hata hivyo mvua hainyeshi wakati huo, nikamuuliza anatokea wapi, akajibu kutoka Malad. Watu wanne waliuawa huko siku mbili zilizopita. Hii ikaongeza shaka," aliongeza.
Alipofikishwa kituo cha polisi na kuhojiwa, alikuwa na miwani na kidole gumba cha chuma kuzuia sindano isimpige fundi cherehani. Mshona nguo pia aliuawa katika mauaji ya Malad. Raman Raghav alikamatwa Agosti 27, 1968. Baadaye alikiri makosa yake katika mahakama.
Alifungua kinywa baada ya kula kuku

Chanzo cha picha, LILY KULKARNI
Hakuna shaka kwamba Raman Raghav alishindwa kujizuia. Kulingana na kitabu cha Ramakant Kulkarni, mdomo wa Raman Raghav haukufunguka kwa urahisi. Mtihani wa kweli kwa polisi ulianzia hapo.
Alipoulizwa unataka nini? 'Kuku' alijibu. Kwa hiyo wakamletea kuku. Baada ya hapo aliomba kuletewa mafuta ya manukato na kioo. Akapaka mafuta kichwani mwake. Kisha akaanza kuzungumza.
Kisha akawapeleka polisi maeneo ambayo alikuwa amefanya mauaji. Pia alionyesha mahali ambapo rungu la chuma alilolitumia kwa mauaji aliliwekwa. Pia, aliahidi atasema yote mbele ya hakimu.
Adhabu gani apewe?

Chanzo cha picha, LILY KULKARNI
Raman Raghav alikiri waziwazi makosa yake katika mahakama ya chini. Mahakama iligundua kuwa hakuonekana kuwa na akili punguani. Adhabu ya kifo ilitolewa. Hata hivyo, hukumu hii ya kifo inapaswa kuthibitishwa na Mahakama Kuu. Kesi hii ilikwenda Mahakama Kuu.
Je, Raman Raghav alikuwa akiugua ugonjwa wowote wa akili na hali yake ya kiakili ilikuwaje wakati wa uhalifu huo? Mahakama Kuu iliteua timu ya madaktari wa magonjwa ya akili ili kujibu maswali hayo.
Aliambia mahakama kwamba alifuata maagizo ya Mungu. Anaeleza kwamba Mungu aliniambia niwaue wote. Ilionekana kwamba akili yake haiko sawa. Kwa hivyo hukumu ya kifo ikageuzwa kuwa kifungo cha maisha jela na Mahakama Kuu mnamo Agosti 4, 1987.
Baada ya kuhukumiwa kifungo cha maisha alihamishiwa jela ya Yerawada huko Pune. Aprili 1995, Raman Raghav alifariki katika Jela ya hiyo kutokana na kufeli kwa figo












