Njia zipi ambazo Israel inaweza kujibu mashambulio ya Iran?

ytgh

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Viongozi wa ngazi ya juu wa Israel baada ya shambulio la Iran

Baada ya mashambulizi ya kihistoria ya Iran dhidi ya Israel, sasa kila mtu anasubiri majibu ya Israel. Hadi sasa, baadhi ya vyombo vya habari vya Israel vimechapisha ripoti kuhusu tofauti ya maoni kuhusu namna Israel itakavyo jibu.

Baraza la Mawaziri la Vita, ambalo pamoja na Benjamin Netanyahu na washirika wake wa mrengo wa kulia, linajumuisha idadi kadhaa ya wapinzani wake wa kisiasa.

Baada ya mashambulizi ya Iran, baraza hili la mawaziri linakabiliwa na mkawanyiko. Kundi kubwa la wenye misimamo mikali kutoka chama cha Netanyahu na vyama washirika wanataka jibu kali kutoka kwa Israel dhidi ya Iran.

Katika upande mwingine, msimamo wa kimataifa – hasa msimamo wa Wamagharibi wa kutaka Israel ijizuie kujibu, imeifanya iwe vigumu kuamua.

Lakini Israel ina chaguzi nyingi tofauti za kuijibu Iran. Sio lazima kujibu kijeshi. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza ikiwa Israel haitachukua hatua, mashambulizi ya IRGC yatakwisha.

Na wasi wasi ni kwamba, ikiwa Israel itaishambulia Iran - itasababisha vita vipana zaidi ambavyo pia vitatoa changamoto kwa maslahi ya nchi za Magharibi katika eneo hilo.

Mara ya mwisho Israel kushambuliwa na isijibu ni mnamo 1991, baada ya mashambulio ya Marekani huko Kuwait, ambayo ilikuwa inakaliwa na Iraq ya Saddam Hussein. Alirusha makombora ya Scud kwenda Israel.

Inasemaka zaidi ya raia 70 wa Israel walikufa kwa njia isiyo ya moja kwa moja ikiwa ni pamoja na mshtuko wa moyo, lakini Israel ilikubali ushauri wa Marekani na haikujibu mashambulizi.

Je, Israel itajibu?

EFDC

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Yoav Galant, waziri wa ulinzi wa Israel, anachukuliwa kuwa mshirika wa Benjamin Netanyahu
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Israel imeshambulia maeneo yenye uhusiano na Iran katika eneo la Mashariki ya Kati mara nyingi. Iran inasema itajibu mashambulizi yote kuanzia sasa na kuendelea.

Katika hali hii, Israel itataka kuiadhibu Iran huku ikikiweka kiwango cha mvutano katika hali ya chini bila kushambulia moja kwa moja ardhi ya Iran.

Lakini kuna uwezekano kwamba Israel itashambulia maeneo yenye uhusiano na Iran katika nchi jirani hasa Syria.

Shambulio katika ardhi ya Iran linaweza kuelezewa kama uchokozi na wakati huo huo linaweza kusababisha Iran kujibu mapigo.

Mojawapo ya maswali muhimu zaidi kuhusu shambulio katika ardhi ya Iran; ni vituo gani Israel itashambulia na nini itakuwa sababu ya shambulio hili.

Katika miongo miwili iliyopita, uwezekano wa Israel kushambulia vituo vya nyuklia vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umeongezeka.

Israel imehujumu kichini chini vituo hivyo. Je, sasa ni wakati mwafaka kwa nchi hii kuchukua hatua ya kuharibu vituo hivi?

Ikizingatiwa kuwa Marekani haiungi mkono shambulio la moja kwa moja dhidi ya Iran kwa sasa, uwezekano wa Israel kushambulia vituo vya nyuklia ni mdogo sana.

Shambulio kama hilo linaweza kufasiriwa kama tangazo la vita dhidi ya Iran, na Tehran haitakuwa na chaguo ila kufanya mashambulio na kujaribu kuidhuru Israel kijeshi.

Mashambulizi kwenye vituo muhimu vya jeshi la IRGC ni sawa na shambulio katika maeneo ya nyuklia na litaamsha hasira kali kutoka Iran. Lakini uwezekano wa Israel kushambulia vituo vya IRGC nao ni mdogo vileivile.

Chaguo jingine kwa Israel ni kujaribu kuwaua makamanda na wafanya maamuzi wa IRGC ndani na nje ya nchi. Ni dhahiri kwamba wale ambao wamehusika katika mashambulizi ya Iran dhidi ya Israel wanakabiliwa na hatari ya mauaji.

Israel ina historia ndefu sana katika uwanja huu. Ingawa uwezekano wa mauaji kama hayo ni mkubwa, lakini si lazima kutokea kwa muda mfupi ujao .

Kujuma miundombinu ya nchi ni chaguo jingine kwa Israel kupitia vita vya mtandao. Uwezekano wa tukio kama hilo kutokea ni mkubwa sana.

Diplomasia na chaguzi zingine

EEFDC

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, F-15 ya jeshi la Israel

Israel ina chaguzi zingine – diplomasia. Chaguzi ambayo imeleta matokeo muhimu katika miaka ya hivi karibuni. Mfano uhusiano wa Israle na Imarati na Bahrain.

Mashambulizi ya siri na hujuma za kificho za kijeshi na kiufundi dhidi ya Iran ni chaguo jingine kwa Israel, katika muda mfupi na mrefu, kama njia ya gharama nafuu ya kuishambulia Iran. Inatarajiwa kwamba mashambulizi kama hayo yataongezeka..

Israel itakuwa na chaguo pia la kupunguza hatari kwa kuimarisha vikosi vyake vya kijeshi na kuimarisha ushirikiano wake na madola makubwa kama vile Marekani, Uingereza, na Ufaransa.

Mwaka 1991, kufuatia mashambulizi ya makombora ya Iraq dhidi ya Syria, Marekani iliipatia Israel silaha za kisasa za ulinzi na mashambulizi.

Kufuatia miongo miwili ya ushirikiano wa kijeshi wa Marekani na Israel ulioanza baada ya mashambulizi ya Saddam, ulinzi wa anga wa Iron Dome ulitengenezwa mahususi kwa ajili ya Israel na mahitaji yake.

Haishangazi kwamba Israel inajaribu kuboresha Iron Dome ambayo inapambana na roketi za masafa mafupi na haifanyi kazi dhidi ya roketi za masafa marefu, haswa makombora ya balestiki.

Mashinikizo kutoka nchi za Magharibi kama vile Uingereza na Ufaransa yatachochea imani katika Israel kwamba nchi hii lazima hatimaye ijitegemee yenyewe tu katika kuhakikisha usalama wake.