Netanyahu: Tunajiandaa, yeyote atakayetudhuru, tutampiga

Chanzo cha picha, Getty Images
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameonya kuwa Israel inaendeleza vita vyake huko Gaza na iko tayari kwa matukio katika nyanja nyingine.
Alisema: "Tunajiandaa kwa matukio na changamoto kutoka nyanja nyingine, na yeyote atakayetudhuru, tutamshambulia. Tuko katikati ya vita huko Gaza, ambavyo bado vinaendelea kwa nguvu."
Aliongeza: "Tunapitia nyakati ngumu na tunaendelea na juhudi za kuwarudisha watu waliotekwa nyara."
Kauli za Netanyahu zimekuja wakati ambapo jeshi la Israel lilifanya operesheni ya kushtukiza ya kijeshi ambapo jeshi la anga lilishiriki, dhidi ya maeneo katika Ukanda wa kati wa Gaza. Jeshi lilisema kuwa operesheni hiyo ya kijeshi ilikuwa ikiendeshwa chini ya mwongozo wa kijasusi.
Jeshi la Israel lilitangaza kuwa limeanza "operesheni nyeti katikati mwa Gaza wakati wa usiku ili kuwaondoa "magaidi" kulingana na taarifa za kijasusi zilizokusanywa na jeshi, na kubainisha kuwa vikosi vya majini na anga vilishiriki katika operesheni hiyo.
UNICEF pia iliripoti kwamba moja ya magari yake yaliyokuwa yakisubiri kuingia kaskazini mwa Gaza yalipigwa na risasi za moto siku ya Jumatano.
Jeshi liliongeza: "Vikosi vyetu viligundua padi za kurushia roketi wakati wa operesheni yao ambayo waliianza katikati mwa Ukanda huo."

Chanzo cha picha, Reuters
Haya yanajiri wakati ambapo vyombo vya habari vya Palestina vilitangaza kuwa idadi ya Wapalestina waliouawa wakati wa uvamizi wa Israel kwenye kitongoji cha Al-Geneina, mashariki mwa Rafah, imeongezeka na kufikia Wapalestina sita.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Imeongeza kuwa mashambulizi ya makombora ya Israel na mashambulizi makali yalilenga maeneo ya kaskazini mwa kambi ya Nuseirat katikati mwa Ukanda wa Gaza.
Shirika la Habari la Palestina "Wafa" lilisema kuwa vifaru vya Israel viliingia kaskazini mwa kambi ya Nuseirat kutoka upande wa Mtaa wa Salah al-Din na al-Mughraqa, huku kukiwa na milio ya risasi kutoka kwenye helikopta, na uharibifu wa idadi kubwa ya minara ya makazi katika mji huo.
Wizara ya Afya huko Gaza pia ilitangaza kuwa Wapalestina 63 na watu 45 waliojeruhiwa walihamishiwa hospitali katika Ukanda huo katika muda wa saa 24 zilizopita kutokana na mashambulizi ya Israel.
Wizara hiyo imethibitisha kuwa, idadi ya vifo vya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza imeongezeka na kufikia Wapalestina 33,545, na kwamba zaidi ya Wapalestina 76,000 wamejeruhiwa tangu kuanza kwa operesheni za kijeshi za Israel huko Gaza tarehe 7 Oktoba.
Kwa upande wake Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Palestina ilitangaza kifo cha mhudumu wa dharura kwa jina Muhammad Abdel Latif Abu Saeed, kutokana na majeraha yake aliyoyapata wiki mbili zilizopita, katika shambulio la Israel huko Khan Yunis kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Mashambulizi ya Israel yalitokea wakati wapatanishi wakisubiri majibu kutoka kwa kambi zote mbili kwa pendekezo lake la hivi karibuni la utulivu ambalo ni pamoja na kuachiliwa kwa mateka walioshikiliwa huko Gaza tangu kuanza kwa vita mnamo Oktoba 7, na kuongezeka kwa hofu ya kimataifa kwamba vita huko Gaza vitaenea.
"kujidhibiti"

Chanzo cha picha, Reuters
Huku Israel na Hamas wakionekana kushikilia matakwa yao kuhusu pendekezo jipya la mapatano katika Ukanda wa Gaza, hofu inaongezeka kwamba vita ambavyo vimekuwa vikidumu kwa muda wa miezi sita vitaenea katika eneo hilo.
Wakati wa mazungumzo ya simu na mwenzake wa Iran, Hossein Amir Abdollahian, siku ya Alhamisi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock alitoa wito wa "kuzuiwa" ili kuepusha "ongezeko jipya la mapigano kikanda" katika Mashariki ya Kati.Wizara yake ilisema
Siku ya Alhamisi, Urusi ilizitaka Iran na Israel zijizuie kufuatia vitisho vya Tehran kwa Israel baada ya shambulio dhidi ya ubalozi wake mdogo.
Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alisema wakati wa mkutano na waandishi wa habari: "Ni muhimu sana kwa kila mtu kujizuia ili kuzuia kuyumbisha eneo ambalo tayari halijatulia."
"Makubaliano ya mezani"

Chanzo cha picha, EPA
Siku ya Alhamisi, serikali ya Israel iliishutumu Hamas kwa "kuupa kisogo" mpango" unaokubalika sana" wa kufikia mapatano katika Ukanda wa Gaza, ambao uliwasilishwa siku kadhaa zilizopita na kundi la wapatanishi.
Msemaji wa serikali ya Israel David Mincer alisema wakati wa mkutano na waandishi wa habari: "Kuna ofa nzuri sana mezani, na Hamas inaendelea kuupa kisogo."
Wakati huo huo, alikosoa "shinikizo la kimataifa kwa Israeli," ikizingatiwa kwamba inaongoza kwa "kusaidia Hamas na kuiweka mbali" na mazungumzo.
Haya yanajiri wakati mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas, Ismail Haniyeh, akithibitisha siku ya Jumatano kwamba kuuawa kwa wanawe watatu katika shambulio la anga la Israel huko Gaza hakutabadili msimamo wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu, ambayo imekuwa ikidhibiti Ukanda wa Gaza tangu 2007, katika mazungumzo.
Haniyeh alisema: “Madai yetu yako wazi na mahususi na hayatakubaliwa. Ikiwa inaaminika kuwa kulenga wanangu ... katika kilele cha mazungumzo haya na kabla ya majibu ya harakati kufika, itawasukuma Hamas kubadili msimamo wake, basi ni udanganyifu. Misimamo imewekwa, haibadiliki kwa hali yoyote ile.”

Chanzo cha picha, Reuters
Harakati ya Hamas ilitangaza siku ya Jumatano kwamba watoto watatu wa Ismail Haniyeh na wajukuu zake wanne waliuawa katika shambulio la bomu lililolenga kambi ya wakimbizi ya Pwani katika Jiji la Gaza, ambapo familia hiyo ilikuwa ikiwatembelea jamaa katika siku ya kwanza ya Eid al-Fitr.
Israel ilithibitisha kuuawa kwa wana wa Haniyeh, na jeshi lilisema katika taarifa yake kwamba yeye na Idara ya Usalama Mkuu (Shin Bet) "iliondoa wanachama watatu wa tawi la kijeshi la Hamas katikati mwa Ukanda wa Gaza.
Licha ya kuweka makataa ya saa 48, siku ya Alhamisi, Hamas na Israel hazikutoa jibu lolote kuhusu pendekezo la kusitisha mapigano lililowasilishwa na wapatanishi siku ya Jumapili, huku pande zote mbili zikiwa katika shinikizo kubwa bila hata mmoja wao kuonekana tayari kuchukua hatua ya kujiondoa.
Pendekezo lililowasilishwa mjini Cairo na wapatanishi wa Marekani, Misri na Qatar awali liliweka masharti ya kusitisha mapigano ya wiki sita na kuachiliwa kwa mateka 42 wa Israel ili kubadilishana na kuachiliwa kwa Wapalestina 800 hadi 900 wanaozuiliwa na Israel, kuingia kwa lori 400 hadi 500 za chakula. misaada ya kila siku, na kurudi kwa waliofurushwa kutoka kaskazini mwa Gaza.
Hamas inadai Israel iondoe vikosi vyake kutoka maeneo yote ya Ukanda wa Gaza, kuruhusu kurejea kwa waliokimbia makazi yao, na kuongeza mtiririko wa misaada, wakati Umoja wa Mataifa unasema kwamba idadi ya watu wote, ambayo ni takribani watu milioni 2.4 wana njaa.
Katika hatua hii, Netanyahu anakataa ombi la Hamas la usitishaji vita, na amesisitiza mara kwa mara kwamba amedhamiria "kuondoa" vikundi vya Hamas vilivyokusanyika kwa maoni yake huko Rafah kusini kabisa mwa Ukanda, ambapo Wapalestina milioni moja na nusu wamekimbia vita.












