‘Ulemavu wetu ndiyo nguvu yetu’: Kijiji ambacho watu wote wana upofu

xx
    • Author, Na Agnes Penda & Gem Oreilly
    • Nafasi, BBC News
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Moses Mugabe ni mwanamme wa umri wa miaka 53 anayeishi mashariki mwa Uganda. Hajui ni kitu gani kilimfanya apoteze uwezo wa kuona ila anakumbuka mara ya mwisho kuona jua likichomoza, kumbukumbu anayoienzi.

“Niliishi maisha ya kuhuzunisha baada ya kupata habari kwamba nimepoteza uwezo wangu wa kuona kabisa, na kwamba sitawahi kuona tena maishani,”anasema.

Moses ni miongoni mwa raia milioni tatu nchini Uganda walio na matatizo ya kuona kulingana na takwimu kutoka shirika la kimataifa la kuzuia upofu (IAPB)

Kote barani Afrika, watu wapatao milioni 100 hawaoni. Huku raia wengi wa Uganda wanaoishi mijini wakipata huduma za matibabu, wale wanaoishi maeneo ya mashinani hukosa kupata huduma zinazofaa za afya ya macho.

Uganda ina wataalamu wachache wa macho.

Bila matibabu, wengi kama Moses wamejitafutia njia za kuishi bila kuona.

xx

Moses anaishi na mke wake na watoto wao watatu katika Kijiji cha Luubu kilichoko kwenye fuo za ziwa Victoria.

Luubu ilikuwa shule iliyojengwa katika miaka ya 2000 kwa ajili ya Watoto waliokuwa na matatizo ya kuona. Moses anaongoza kikundi cha jamii ya vipofu cha Luubu.

Jamii hii ni ya watu 25, karibu wote hawaoni/

Jamii hii inaishi katika uwanja mmoja na wanatumia vyoo viwili kwa Pamoja.

Wao hukutana kila jumatatu chini ya mti mkubwa wa mfenesi ili kuzungumzia changamoto wanazopitia.

Moses, anayejulikana kama ‘mwenyekiti’na wenzake anaongoza mkutano.

“Tunaomba misaada ya vifaa vya kutusaidia kusikia zaidi,”mmoja wao anasema.

Mwengine anapaza sauti kuhusu ongezeko la karo ya shule.Moses anamjibu kwa utulivu.

“Msikubali kudhulumiwa haki zetu kwa vile sisi ni walemavu, tutazungumza ili kila mmoja ajue thamani yetu,” anajibu.

Mikutano hii ya kila wiki ina umuhimu mkubwa, Moses anaiambia BBC.

Tunazungumza jinsi ya kusaidiana na kuwasomesha watoto wetu. Jinsi ya kuwalisha watoto wetu, kuwavisha na vile tutakavyopata huduma bora za matibabu.”

Kuishi na upofu nchini Uganda

Huenda ikawa wakazi wa Luubu wamepoteza uwezo wa kuona kwa sababu kadhaa kama homa ya mto ama onchocerciasis, kisukari, ukambi, ugonjwa wa mtoto wa jicho na trachoma.

Lakini wengi, kama Moses hawajawahi kuelezewa hali yao na daktari.

Katika miaka ya 1990 na 2000, ugonjwa wa homa ya mto unaosababisha upofu ulienea kote mashariki mwa Uganda na hasa katika wilaya ya Mayuge.

Ugonjwa huo husababishwa na mnyoo wa majini na kusambazwa kwa binadamu kupitia kuumwa na nzi weusi waliobeba ugonjwa huo.

Makaazi yaliyoko kwenye ufuo wa ziwa kama Luubu yaliathirika zaidi.

Hata hivyo, mwaka wa 2017, baada ya kuzinduliwa kwa miradi ya kupambana na homa hiyo, homa ya mto iliisha katika wilaya ya Mayuge.

xx

Huenda ugonjwa huo haupo kama zamani, lakini Kijiji cha vipofu cha Luubu kingalipo.

“Kama jeshi kambini, tunaishi pamoja ili iwe rahisi kuungana kunapokuwa na jambo,”anasema Moses.

Zaidi ya watu milioni tatu nchini Uganda hawaoni.

Ukosefu wa huduma za matibabu ya macho.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Daktari Waiswa Julius ndiye daktari peke yake anayehudumia kaunti ya Bukatebe kunakopatikana kijiji cha Luubu.

Yeye hufanya kazi mara mbili kwa wiki katika kituo cha afya cha Mayuge na huwahudumia wakazi wa Luubu mara kwa mara.

Anasema kwamba umasikini na mazingira machafu ni baadhi ya sababu za idadi kubwa ya watu kupoteza uwezo wa kuona miongoni mwa wakazi katika eneo hilo.

Lakini dhana za kitamaduni, zinazowasukuma watu kutafuta dawa za kienyeji pia zinachangia pakubwa.

Dkt.Julius anasema kwamba imani hizi zinaweza kuwazuia watu kutafuta huduma za matibabu wanazohitaji na huwaona madaktari wakati wamechelewa mno.

“Kama serikali inaweza kuongeza idadi ya wataalamu wa macho kwa kila wilaya, nadhani itakuwa bora,”anasema.

Daktari Alfred Mubangizi ambaye ni mtaalamu wa magonjwa ambukizi katika wizara ya afya nchini Uganda anasema serikali inatoa udhamini wa masomo ya madaktari wachanga ili wawe wataalamu wa macho.

“Tunawafunza madaktari. Serikali inawahimiza kusomea shahada za uzamili katika somo la utaalamu wa macho ili tupate madaktari wengi zaidi,”

‘Ulemavu wetu ndiyo nguvu yetu’

Hadi pale kutakapokuwa na wataalamu wa kutosha wa macho katika maeneo ya mashambani nchini Uganda, Moses na jamii yake wataendelea kutegemeana.

“Kile tulichojifunza mwanzo ni umoja. Kila mtu anamhitaji mwenzake na ulemavu wetu ndiyo nguvu yetu,”anasema.

Anasema kuwa changamoto tatu zinazoikumba jamii hii ni kuepuka unyanyapaa, kukosa urithi katika familia zao na kupata mchumba.

Jamii yake pia inatia bidii kuwaelimisha watoto wao ambao pia hawaoni vizuri ama wameshapofuka hata ikimaanisha kuwapeleka katika shule za bweni zilizoko mbali na nyumbani.

Moses ana matumaini kwamba wanawe watafuzu kwa shahada za uzamili na za uzamifu. Katika kufaulu hivyo, anasema watasaidia kuondoa unyanyapaa na kuipa jamii hii kesho iliyo bora.

“Watakapokuwa wameelimika vya kutosha, hakuna atakayewaona kama vipofu. Watu wataangalia mafanikio yao badala ya kuwatenga,”anasema.

“Tutazungumzia haki zetu katika kila fursa tutakayopata, haijalishi lolote, sauti zetu zitasikika na wito wetu kujibiwa.”

Imehaririwa na Ambia Hirsi