Waridi wa BBC: 'Maisha yangu yalivyobadilika nilipojifungua watoto wanne wasio na uwezo wa kuona'

Elizabeth Chemsilet
Maelezo ya picha, Elizabeth Chemsilet
    • Author, Anne Ngugi
    • Nafasi, BBC Swahili

Katika Boma lake Elizabeth Chemsilet lililopo Chepalungu Kaunti ya Bomet nchini Kenya, kicheko ndicho kinachokaribisha kikosi cha BBC nyumbani kwake.

Tulizuru boma hili ili kukutana na mama huyu mwenye miaka 74 ambaye amepiga moyo konde na kuendeleza maisha yake licha ya kuwa mama wa watoto wanne ambao wanaishi na upofu kati ya tisa aliojifungua.

''Kila nilipojifungua watoto wangu walipishana mmoja hana uwezo wa kuona na huku mwingine akiwa sawa, hadi mtoto wa mwisho, kwa ujumla nina watoto wanne ambao hawana uwezo wa kuona,” anasema Elizabeth.

Mama huyu anasema kuwa wakati alipojifungua mtoto wake wa kwanza David hakufahamu kuwa alikuwa na upofu, hadi wakati alianza kutambaa na kuona jinsi alivyokuwa anajikwaa kila wakati, mwanzo hali hio ilimsumbua mno ila alitulia wakati alipojifungua mtoto wake wa pili na akawa yuko sawa , cha kuhuzunisha mtoto watatu alizaliwa akiwa na upofu na hapo hapo mama huyu alianza kujiuliza maswali mazito shida ilikuwa wapi kwani alikuwa sasa amepata wana wawili ambao hawakuwa na uwezo wa kuona

Mtindo huo huo uliendelea kwani alikuwa anajifungua mtoto mmoja mwenye upofu na aliyefuata anakuwa yuko sawa hadi nilipojaliwa kitinda mimba

Hawa watoto wenye 'upofu' ni akina nani?

Kutoka kulia: David Rotich, Emily Chepkorir, Margaret Chepkurui na Chesimet Chelang’at.
Maelezo ya picha, Kutoka kulia: David Rotich, Emily Chepkorir, Margaret Chepkurui na Chesimet Chelang’at.

David Rotich ambaye ndiye kifungua mimba ana miaka 48 , yeye ni baba wa watoto watano ambao wote wako sawa vile vile amehitimu kama mwalimu wa chekechea. Naye Emily Chepkorir ni mtoto wa tatu na ana ujuzi wa kufuma fulana.

Margret Chepkori ni mtoto wa tano ni mtaalam wa kukanda na hatimaye Chesimet Chelang’at pia ni mwalimu wa shule ya chekechea. Wote sasa ni watu wazima na wamekubali hali yao kama walivyozaliwa .

Mama yao anasema kuwa imekuwa ni safari isiyo na kifani jinsi ya kulea watoto wanne ambao hawana uwezo wa kuona.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Elizabeth anasema kuwa kuna wakati alianza kuhoji Mwenyezi Mungu -Ni kwa nini alijaalia kujifungua watoto wenye ulemavu wa macho, hakupata jawabu ila anasema amani ambayo amekuwa nayo ni jawabu tosha kuwa alikubali hatma hiyo na kuhakikisha kuwa wanawe wana maisha kama ya wenzao.

''Nilianza utafiti na kujaribu kujua ni kwa nini nilikuwa nazaa watoto wasioona kuna wakati nilikuwa na hoji mungu kimoyomoyo ni kwanini haya yanipite, niliendelea na kilimo ili kuwawezesha wana wangu wenye upofu kwenda shule maalum.” alisema Elizabeth.

Elizabeth alihakikisha wanawe hao wamejiunga na shule bora za walemavu nchini Kenya katika maeneo ya Mombasa, Meru na Kisumu mtawalia, anasema kuwa kuna wale walikuwa wanamkosoa ni kwanini anakubali watoto wawe mbali na nyumbani ilhali walikuwa na ulemavu wa macho.

Anajivunia kuwa hakusikiliza maneno ya baadhi ya wakosoaji wake kwani hatimaye lengo la wanawe wamepata elimu lilitimia licha ya changamoto alizopitia.

''Sasa mimi nimeanza kuzeeka na ombi langu ni kuwa kila mmoja wao atajaaliwa familia , hawa wanangu wa kike ambao hawaoni hakuna aliyeolewa inanipa wasiwasi kwani ningependa pia kuwaona wajukuu,” anasema Elizabeth.

tt

Changamoto ambayo Elizabeth anazungumzia ni ya unyanyapaa unaotokana na dhana zinayohusishwa na ulemavu hasa kwa familia zinazoishi vijijini.

Kwa mfano mama huyu anasema kuna wale ambao wanalinganisha tukio la yeye kujifungua watoto wanne wasio na uwezo wa kuona kuwa ni uchawi au laana. Hata hivyo Elizabeth anaamini mtu yeyote anaweza kujipata katika hali kama yake.

Amekuwa akizungumza na wanawake haswa ambayo ndio huathirika sana wakati wanajifungua watoto wenye ulemavu na kuwaambia hatua ya kwanza ni kukubali hali na kutafuta njia ya kuishi na hali hii na kutafuta ushauri na matibabu kwa mtoto wao.

Cha msingi anasema upendo ni muhimu wakati mtu anapokabiliana na hali hizo.