Mfalme aliyekatazwa kumuona mama yake


Mfalme Joshua amekalia kiti cha ufalme cha Yoruba mjini eneo la Odo Owa nchini Nigeria

Chanzo cha picha, Joshua Adegbuyi, Olota wa Odo Owa

Maelezo ya picha, Mfalme Joshua alikuwa kwa njia panda ya kulinda desturi na kuishi maisha ambaye kumuona mamake ni marufuku kwake.
    • Author, Ahmed Ambali
    • Nafasi, BBC Africa
    • Akiripoti kutoka, Lagos
    • Author, Opeyemi Adeoti
    • Nafasi, Freelancer
    • Akiripoti kutoka, BBC Yoruba, Lagos
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

“Usiku wa kuamkia kutawazwa kwangu, viongozi wa kuteua mfalme walinipeleka kwa mama yangu kwa kile nilichojua itakuwa ni mara ya mwisho,” anasema Mfalme Joshua Adegbuyi Adeyemi, mfalme wa kiasili wa Odo Owa katika ardhi ya Wayo nchini Nigeria.

“Aliniombea, maneno yake yalijawa na upendo na tahadhari. Baada ya usiku huo, sijauona tena uso wake.”

Mfalme Joshua anazungumzia desturi ya kale ya Kiyoruba inayosema kwamba mfalme wa Odo Owa lazima atenganishwe milele na mama yake.

“Sikuwahi kutaka kuwa mfalme,” anasema.

“Nilijua inamaanisha sitoweza kumuona mama yangu tena.”

Majaaliwa ya Ufalme

Licha ya kuzaliwa katika familia ya kifalme, Mfalme Joshua anasema alikuwa na ndoto ya kuwa mhadhiri wa chuo kikuu, akifanya kilimo kwa upande na akiishi kwa furaha na mama yake na watoto wake.

Anakumbuka akiwa kijana,kiongozi wa kanisa alimwambia kuwa kuhusu maono aliyoyaona ambapo aliona Joshua akichukua jukumu la uongozi baadaye maishani.

Kwa furaha na ujasiri kutokana na ufunuo huo, Joshua alijua alikuwa akiitwa kuwa kiongozi wa kanisa. Hii ilimfanya kuwa na azma ya kufuata shahada ya uzamili katika dini.

Lakini alipojipanga kumwambia mama yake kuhusu masomo yake, alipokea habari za kukata tamaa.

‘’Viongozi wa kuteua mfalme walikuja kunipa habari kuwa mfalme amefariki,”anasema.

‘’Sikuwa na muda wa kumuelezea uamuzi wa viongozi wa kuteua mfalme. Mizimu ilikuwa ishazungumza, na ilikuwa muda wangu kuwa mfalme."

Mfalme Joshua alijipata katika njia panda kati ya kuhudumia watu wake na kutokumwona mama yake tena kwa maisha yake yote.

Ilikuwa ni uamuzi aliokuwa na muda mdogo wa kuufikiria. Kwa shinikizo, alikubali haraka kiti cha wazee wake na kuwa mfalme.

Mwiko wa kizamani

‘‘Mfalme ni kama baba ,mhifadhi wa kiroho ambaye analinda watu wake kutokana na janga lolote,’’anasema Ifayemi Elebuibon, mtaalam wa masuala ya mila za jamii ya Yoruba.

Katika ardhi ya Yoruba,wafalme wanachaguliwa kutoka nyumba za kifalme,na wadhifa huo unaendelea kuheshimiwa.Mtawala mkuu huzungukwa na desturi na mwiko ambazo zinachukuliwa kuwa takatifu.

‘‘Kuna ufanisi wa kuwa mfalme,lakini mfalme ni kama ngao wa kulinda maovu na balaa zisiwafike wakaazi. Anapaswa kujitolea na kujinyima vingi ili kuwe na usawa katika jamii.’’

Yemi Elebuibon, Balozi na mtaalam wa mila ya Yoruba
Maelezo ya picha, Wahifadhi wa asili kama vile Elebuibon anaamini wafalme ni ngao ya kulinda watu wake dhidi ya majanga na wanapaswa kujitolea kutumikia jamii.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Elebuibon anasema kuwa hadhi hii ya kipekee inahifadhiwa na miko ambazo hufanya kazi ya kulinda mfalme na kumwezesha kuwa na uhusiano na nguvu za kimungu.

“Mara anapokuwa mfalme, wote wako chini yake, wakiwemo wazazi wake,” anasema.

Dkt. Reuben Akano kutoka Chuo Kikuu cha Jimbo la Kwara anakubaliana na haya , akisema mwiko zinazomhusu mfalme zinatokana na uzamani na zinatakiwa kulinda jamii kutokana na madhara.

“Binadamu hawakuamka tu kusema wanataka mwiko,” anasema.

“Huwezi kukubali kuwa mfalme kisha urudi nyuma kusema hutaki kufuata desturi. Hilo haiweze.”

Wakati mfalme Joshua alipomuona mamake mzazi mara ya mwisho,viongozi wa kuteua mfalme walimfanyika tambiko kadhaa kama vile kumuagiza aregeshe ‘’Oja’’ kwa mama yake.

Tukizungumzia ‘’Oja’ni kipande cha kitambaa kilichotumika kumfunga mtoto mgongoni mwa mama yake ili kumruhusu kutembea bila ugumu na kumuwezesha kuwa karibu na mtoto wake.

Kurudisha Oja inahusishwa na kufunga mlango wa uhusiano wa mama na mtoto, na kumtayarisha mfalme kwa jukumu mbele yake.

“Utengano huu na mama yake au wazazi wote huashiria mpito wa mfalme kutoka kwa kiumbe wa kawaida kuwa ‘Kabiyesi’, maana yake ni mtu ambaye hawezi kuulizwa lolote,” anasema Elebuibon.


Bi Deborah Titilayo Adeyemi,mama wa mfalme Joshua Adeyemi.

Chanzo cha picha, Joshua Adegbuyi, Olota of Odo Owa

Ili utawala wake uwe na mafanikio na ustawi, Elebuibon anasema Mfalme Joshua lazima afuate miko hii.

“Jambo la mwiko ni kwamba anayekiuka hawezi kuwa ndiye anayekumbana na madhara yote,” anaeleza.

“Huenda ni watoto wake au kutatokea machafuko na mizozo katika nchi. Haya yote huja na madhara makubwa. Hakuna mfalme anayetaka hili kwa watu wake.”

Pamoja na miko hii, Mfalme Joshua hawezi kuona maiti, mtoto mchanga, wala kujamiiana na mkewe wakati wa mchana.

Lakini marufuku ya kutomwona mama yake ni desturi ambayo imemgusa Mfalme Joshua zaidi.

“Sikujua kitu kingine isipokuwa upendo kutoka kwa mama yangu nilipokuwa mtoto,” anasema Joshua.

“Alilipa ada yangu ya shule na akanikuza kuwa nilivyo leo. Najisikia mnyonge kuwa siwezi kumwona kwa sababu desturi inasema hivyo.”

Wakati mmoja, hamu ya Mfalme Joshua kumwona mama yake ilikuwa kubwa kiasi kwamba alijitolea kukiuka desturi, bila kujali madhara yake.

“Nilitaka kumwona kwa lazima,” anasema.

Hata hivyo, kamati ya wanaoteua mfalme, wakiwa na hofu ya madhara ya kitendo hicho, walihakikisha kuwa mkutano haukutokea kwa kumfungia ndani ya kasri na kumficha mama yake.

Kujipata njia panda


Mfalme Abdulrasheed Akanbi ni mtawala wa jamii ya Iwo,mjini Yoruba aliyejikita katika uislamu

Chanzo cha picha, King Abdulrasheed Akanbi

Ari ya Mfalme Joshua ya kudumisha mila na a desturi ni ya kipekee wakati ambapo baadhi ya wafalme wa Kiyoruba wanajitenga na hawatilii maanani desturi kama hizi.

Mfalme Abdulrasheed Adewale Akanbi wa Iwo, mji wenye mizizi ya Kiislamu, amekosoa umuhimu wa baadhi ya mwiko, na kusababisha mvutano miongoni mwa vigogo wa asilia wakichukulia matamshi yake kama ya kukufuru.

Kwa mfano,mwaka wa 2016, Mfalme Abdulrasheed aliamuru kuondolewe sanamu ya Ogun, mungu wa chuma na ubunifu wa Yoruba, iliyoingizwa katika lango la kasri, akisema, “Vyumba vya kifalme lazima viwe safi na visiwe na sanamu yoyote.”

Baada ya sanamu hiyo kuondolewa, waabudu wa Ogun walishindwa kutoa dhabihu kwa mungu huyo. Walitishia maandamano ya watu milioni moja dhidi ya mfalme lakini hatimaye walitupilia mbali wazo hilo.

Hadi leo, hakuna jambo lolote baya lililotokea kwa Mfalme Abdulrasheed kwa kuvunja mwiko huo na anaendelea kusema dhidi ya desturi za kidini za jadi.

Huko Odo Owa, hakuna mfalme aliyevunja desturi inayomzuia mfalme wa sasa kumwona mama yake.

“Kama ningetaka kuwa kama baadhi ya wafalme wenzangu, ningekuwa nimesitisha sheria hii. Lakini nilikubaliana na viongozi wa kuteua mfalme kwamba tutafuata desturi ya nchi yetu,” anasema Mfalme Joshua.

“Nataka kubadilisha sheria, lakini siwezi,” anasema.

Mfalme Joshua anasema anatamani kwamba katika siku za baadaye, mtu mwingine atakuwa na ujasiri wa kuondoa marufuku hii, lakini sio yeye mwenyewe kufanya hivyo.

Kwa huzuni, utii wa Mfalme Joshua kwa desturi ulileta maumivu kwani alivyokuwa mfalme, hakumwona mama yake tena.

Alifariki tarehe 25 mwezi Julai, 2023.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Ambia Hirsi