Mjue mchezaji pekee kutoka Afrika anayewania tuzo ya Ballon d'Or mwaka huu

Ademola Lookman celebrating with the Europa League trophy

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ademola Lookman alifunga mabao 17 na kutoa pasi za mabao 10 akiwa na washindi wa Ligi ya Uefa, Atalanta
    • Author, Emmanuel Akindubuwa
    • Nafasi, BBC Sport Africa
    • Akiripoti kutoka, Lagos
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Ademola Lookman, winga huyo wa Nigeria - amechukua vichwa vya habari kote Ulaya na Afrika - kuanzia uchezaji wake akiwa na Super Eagles (Nigeria) wakati wa Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023, hadi kuisaidia Atalanta kushinda taji lao la kwanza la UEFA, nyota huyo mwenye umri wa miaka 27 anaendelea kuinuka.

Maendeleo ya Lookman yamemfanya kuorodheshwa kama mmoja wa wachezaji 30 walioteuliwa kuwania tuzo ya Ballon d'Or mwaka huu, mshindi wa tuzo hiyo ya mwanasoka bora zaidi duniani atatangazwa jijini Paris siku ya Jumatatu.

Kuwa Mwafrika pekee kwenye orodha hiyo kumeongeza uzito katika mafanikio yake.

"Ni jambo kubwa kuwa kwenye orodha na jambo kubwa zaidi kuwa Mwafrika pekee," anasema.

Moja ya wakati wa furaha kwa Lookman ilikuwa ni katika fainali ya UEFA, alifunga mabao matatu na Atalanta ikapata ushindi dhidi ya timu ya Bayer Leverkusen.

Uchezaji wake kwenye uwanja wa Aviva mjini Dublin ulionyesha ustadi wake, na akawa mchezaji wa kwanza kufunga magoli matatu katika fainali ya UEFA tangu Jupp Heynckes alipoifungia Borussia Monchengladbach katika Kombe la Uefa la 1975.

"Usiku huo ulikuwa wa kipekee," anakumbuka Lookman.

Pia unaweza kusoma

Alikotokea

Ademola Lookman celebrates a goal for Atalanta

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Kiwango cha Lookman kimepanda akiwa na Atalanta ya Italia baada ya kuchezea vilabu vinne vya Uingereza na kukaa Ujerumani.

Amekuliwa Kusini mwa London na kuanza kucheza mpira katika timu ya vijana ya Charlton Athletic.

Lookman alijiunga na Everton kwa mkataba wa pauni milioni 11 ($14.26m) alipokuwa na umri wa miaka 19, na kisha akahamia katika klabu ya RB Leipzig ya Ujerumani.

Alirudi kwenye Ligi ya Kuu ya Uingereza kwa mkopo, akianza kucheza Fulham na kisha Leicester City, lakini fowadi huyo aliimarika zaidi tangu alipohamia Atalanta mwezi Agosti 2022.

Kuhamia nchi mpya, kujifunza lugha mpya na kuzoea utamaduni tofauti wa soka kunaweza kuwa jambo la kuogofya, lakini Lookman anastawi huko kaskazini mwa Italia.

Miaka yake miwili akiwa Bergamo imekuwa ya mabadiliko na anaamini mtindo wa uchezaji wa klabu hiyo chini ya kocha Gian Piero Gasperini umempa fursa ya kuonyesha ubunifu wake uwanjani.

Kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu kumempa Lookman fursa nyingine ya kuonyesha ujuzi wake dhidi ya timu bora zaidi duniani

Mnigeria moyoni

Ademola Lookman and Victor Osimhen celebrating a goal for Nigeria at 2023 Africa Cup of Nations

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ademola Lookman na Victor Osimhen wakishangilia bao la Nigeria kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika 2023
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Licha ya mafanikio yake ya mapema akiwa na timu za vijana za England, ikiwa ni pamoja na kushinda Kombe la Dunia la Chini ya miaka 20 mwaka 2017, lakini alimuamua kuiwakilisha Nigeria katika ngazi ya juu ya soka.

"Siku zote mimi ni Mnigeria, niliyezaliwa na kukulia nchini Uingereza," anasema.

"Siku zote niko karibu na watu wangu, na utamaduni wangu. Nimekuwa nikienda na kurudi Nigeria tangu nikiwa mtoto."

Uamuzi wa kubadili utiifu na kuichezea Nigeria Mwaka 2022 - ulirahisishwa na uhusiano wake wa asili na urithi kwa nchi hiyo.

"Ni heshima kuwa na nembo ya Nigeria kifuani mwangu na kuweza kuivaa kwa fahari."

Uchezaji wake akiwa na Super Eagles umemfanya kupendwa na mashabiki na alikuwa mchezaji muhimu katika timu hiyo kuelekea mechi za Afcon 2023.

Mabao matatu ya Lookman nchini Ivory Coast yalimfanya atajwe kwa sifa katika michuano hiyo, lakini Nigeria ilichapwa 2-1 kwenye fainali na wenyeji.

Wakati mafanikio ya Lookman katika klabu yakiongezeka, Nigeria imekumbwa na changamoto mwaka huu.

Juhudi za timu kuwania kufuzu Kombe la Dunia la 2026 la Fifa - zimekosa utulivu, kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara ya wakufunzi.

Licha ya changamoto hizo, Lookman bado ana matumaini kuhusu mustakabali wa timu hiyo, wakati mechi za kufuzu Afcon 2025 zikikamilika mwezi ujao.

"Kila mtu anajua tuna kikosi kilichojaa vipaji. Na tunapocheza pamoja, tutaonyesha hilo zaidi. Sote tunafanya kazi kwa bidii kuelekea lengo moja."

Licha ya mafanikio yake mwaka 2024, Lookman hayuko tayari kupumzika. "Ninalenga [kuendelea] kupigania mambo ninayotaka."

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah