Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Changomoto za kuishi kama mpenzi wa jinsi moja katika nchi ya Kiislamu
Huku Thailand ikichukua hatua ya kihistoria kukaribia kuhalalisha ndoa za watu wa jinsi moja, jamuiya ya LGBTQ+ nchini humo wanaimbia BBC kuwa ingawa wanakaribisha hatua hiyo, bado kuna safari ndefu.
"Naunga mkono mswada huo lakini kama ningekuwa na familia, pengine ningehama na kuishi mahali pengine," Alif, mpenzi wa jinsi moja kutoka jiji la Yala kusini mwa Thailand anasema.
Ingawa amejitokeza kwa wanafamilia wake wa karibu, Alif anasema hajawahi kumtambulisha mpenzi wake.
Anakiri kuwa anatatizika na uamuzi huo wake na hataki BBC itumie jina lake halisi.
Kijana huyo mwenye umri wa miaka 25 anaishi katika mojawapo ya majimbo manne ya kusini mwa Thailand ambako wakazi wengi ni Waislamu.
Eneo hilo la kusini mwa nchi lilikuwa likiongozwa na kiongozi wa Kiislamu, na watu wengi walioishi huko walikuwa Waislamu wa Malaysia. Lakini mwanzoni mwa Karne ya 20, eneo hilo likawa sehemu ya Thailand. Ubuddha kwa sasa ndio dini kubwa inayofuatwa nchini Thailand.
Alif anasema matendo, mazungumzo, na mavazi yake ni ya mwanamume Muislamu wa kawaida. Lakini ana wasiwasi jamii ikijua mwelekeo wake wa kijinsia, anaweza kutengwa.
Hiyo ni licha ya bunge la chini la Thailand kupitisha mswada wa kutambuliwa kisheria kwa ndoa za jinsia moja.
Bado inahitaji idhini kutoka kwa Seneti na uidhinishaji wa kifalme ili kuwa sheria. Lakini hilo linatarajiwa kufanyika mwishoni mwa 2024, hatua ambayo itaifanya Thailand kuwa nchi pekee ya Kusini Mashariki mwa Asia kutambua ndoa za wapenzi wa jinsi moja.
Naiyana Supapung, ambaye anahudumu katika kamati ya baraza la chini kuhusu usawa wa ndoa, anaiambia BBC kwamba ingawa sheria mpya itawapa Waislamu haki ya kufunga ndoa za jinsi moja, anaonya: "Imamu anaweza kukataa kufanya Nikah [ sherehe ya ndoa ya Kiislamu]."
Alif pia anadhani kuwa ni jambo lisilowezekana kwamba jumuiya ya Kiislamu anamoishi inaweza kukaribisha sherehe za wapenzi wa jinsi moja, akisema: "Nilisikia watu wakilinganisha watu wa LGBTQ+ na wanyama siku moja nje ya msikiti baada ya sala ya Ijumaa. Nilishtuka kusikia matamshi hayo makali ya chuki."
Sheria hiyo mpya, iliyopitishwa na wabunge 400 kati ya 415 waliopo, itaelezea ndoa kama ushirikiano kati ya watu wawili, badala ya kati ya mwanamume na mwanamke. Na itawapa wanandoa wa LGBTQ+ haki sawa za kupata akiba ya kodi ya ndoa, kurithi mali, na kutoa idhini ya matibabu kwa washirika ambao hawana uwezo.
Chini ya sheria, watu waliooana wa jinsi moja wanaweza pia kuasili watoto. Hata hivyo, baraza la mawaziri halikupitisha pendekezo la kamati kutumia neno “wazazi” badala ya “baba na mama”.
Thailand tayari ina sheria zinazopiga marufuku ubaguzi kuhusu utambulisho wa kijinsia na mwelekeo wa kijinsia na kwa hivyo, inaonekana kama mojawapo ya mataifa ya Asia yanayokubali jumuiya ya LGBTQ+.
Lakini imechukua miaka mingi ya kufanya kampeni kwa wapenzi wa jinsi moja kukaribia usawa wa ndoa.
Majaribio ya hapo awali ya kuhalalisha ndoa za jinsi moja yalifeli licha ya kuungwa mkono na umma. Utafiti wa serikali mwishoni mwa mwaka jana ulionyesha kuwa asilimia 96.6 ya waliohojiwa waliunga mkono mswada huo.
Sheria hiyo mpya itaimarisha sifa ya Thailand kama kimbilio la jamaa kwa wanandoa wa LGBTQ+ katika eneo ambalo mitazamo kama hiyo ni nadra, na mwenyekiti wa kamati ya baraza la chini kuhusu usawa wa ndoa, Danuphorn Punnakanta, aliliambia bunge wakati akiwasilisha rasimu ya mswada huo: "Hii ni mwanzo wa usawa. Sio suluhu kwa kila tatizo lakini ni hatua ya kwanza kuelekea usawa. Sheria hii inataka kurudisha haki hizi kwa kundi hili la watu, sio kuwapa haki."
Mwanaume muislamu mwenye umri wa miaka 27 ambaye ni mpenzi wa jinsi moja ambaye alizaliwa katika jiji la Songkla, kusini mwa Thailand hana imani kuwa sheria hii italeta mabadiliko mengi eneo anamoishi.
Hataki kutumia jina lake halisi, kwa hivyo tumemwita Wael. Anaambia BBC mara nyingi anaonewa kwa sababu ya mwelekeo wake wa kijinsia.
Wael anasema alilelewa na binamu zake ambao mara nyingi walimpaka vipodozi na kumvalisha nguo za wasichana, jambo ambalo halikupendeza kwa wazazi wake ambao walikuwa Waislamu wenye msimamo mkali.
Anasema marafiki wa wazazi wake walichukizwa sana kwa "kuwa na hisia tofauti" na mara kwa mara aliulizwa kuhusu jinsia yake wakati akiwa mdogo.
Kuwa katika jumuiya ya LGBTQ+ "hakufai kuwa makosa" Wael anashangaa na ingawa anakaribisha sheria mpya anasema: "Sitaki kuolewa."
Wael anasema itakuwa vigumu sana kwake kueleza wazazi wake kuwa anaoa mtu wa jinsia sawa na yake, kwa sababu kwa Waislamu wengi wanaoishi Thailand, licha ya sheria hii mpya "ni makosa katika ulimwengu wao".
Imetafsiriwa na Jason Nyakundi na kuhaririwa na Ambia Hirsi