Je Urusi imekuwa ikinunua kisiri injini za ndege za Ukraine kupitia Iran?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ndege aina ya An-74i inatumika kwa madhumuni ya kijeshi na ya kiraia.

Mashirika ya kijasusi ya Ukraine yaliripoti wiki hii kwamba yalifichua mpango wa kusafirisha injini za ndege ya kijeshi ya An-74 kutoka Ukraine hadi Iran.

Simulizi hii isingekuwa ya kushangaza kama si mpokeaji wa mwisho wa injini hizi.

Kama ilivyojulikana na BBC, wachunguzi wa Ukraine wanadai kwamba Iran imekuwa ikitumika kama nchi ya kati tu ilhali Urusi anaweza kuwa mnunuzi halisi.

Habari hii ilianza mwaka 2011, wakati shirika la ndege la Lviv Airlines lilifutiliwa mbali nchini Ukraine. Kisha mali zote za shirika hili la ndege zilipaswa kuhamishiwa kwenye mfuko wa mali ya serikali, lakini kulikuwa na usiri mkubwa hali ya kwamba serikali ilifichwa huku sehemu ya mali ya shirika hilo ikipelekwa katika mikoa mingine kwa uuzaji zaidi.

Kwa hivyo injini mbili za ndege za turbojet za D-36 zilikuwa mikononi mwa wajasiriamali wawili kutoka Dnieper ambao walikuwa wakijishughulisha na usafirishaji wa mizigo kwenda nchi za Asia na Afrika.

.

Chanzo cha picha, Zaporisk Prosecution office

Maelezo ya picha, Injini aina ya D-36

Vipuri vya ndege nchini Ukraini viko chini ya udhibiti wa mauzo ya nje, kwa hivyo haingewezekana kuviuza hivyo hivyo. Walipanga kuvificha na kuvitoa nje chini ya vipengele vya mabomba ya gesi kwa kutumia nyaraka za kughushi. Kwa hili, wanunuzi wa kigeni waliahidi kulipa $ 400,000 kwa kila injini.

Kulingana na vyanzo vya mamlaka ya uchunguzi, hii inaweza kuwa mpango wa magendo kwa ajili ya kusafirisha bidhaa za kijeshi kutoka Ukraine hadi Urusi kupitia nchi tatu. Kwa uwezekano wote, ununuzi huo ulikusudiwa kwa ndege za usafirishaji wa jeshi la Urusi.

D-36 ni injini ya ndege ya turbojet yenye mzunguko wa pande mbili, iliyozalishwa kwa wingi nduliwa katika kiwanda cha Zaporizhzhya Motor Sich mnamo 1977 kwa ajili ya ndege ya Antonov.

.

Chanzo cha picha, Zaporiska Prosecution office

Na mnamo Oktoba 2022, SBU ilimtia kizuizini rais wa shirika hili, Vyacheslav Boguslavev. Anashukiwa kuwa Motor Sich iliipatia Urusi injini na vipuri kinyume cha sheria, ambazo zilitumika kutengeneza na kukarabati ndege aina ya helikopta za Urusi ambazo zilishiriki kikamilifu katika uvamizi kamili wa Ukraine.

Kulingana na wachunguzi, injini zilizotengenezwa na Ukraine zilipatikana katika helikopta za Urusi zilizoanguka, ambayo inamaanisha kuwa Urusi ilinunua vifaa muhimu kupitia nchi za tatu, ili kukwepa vikwazo na marufuku.

Kwa hivyo, inaonekana kwamba Moscow inaendelea kutafuta njia za kununua vipuri muhimu vya zana zake za kijeshi kutoka Ukraine.

Je, nini cha ajabu kuhusu injini ya An-74? Uchanganuzi wa mwanahabari wa BBC kuhusu masuala ya kijeshi Pavel Aksyonov

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

An-74 ni muundo wa polar wa ndege ya usafirishaji ya An-72, ndege iliyofanikiwa sana ya usafirishaji na nyepesi iliyotengenezwa katika Ofisi ya Ubunifu ya Antonov miaka ya 1970. Kwa sababu ya kumiliki eneo lisilo la kawaida la injini juu ya ndege, ndege hii inaweza kutua kwenye njia ndogo,ambazo ni duni.

Wakat iwa baridi, mwaka 2019 waandaaji wa kambi ya Arctic ya Urusi "Barneo" hawakuweza kukodisha ndege hii ya Ukraine na msafara wake ulighairiwa , kwa sababu ndege nyingine hazikuweza kutua kwenye barabara ya barafu.

Sifa za hali ya juu za ndege hii ya usafirishaji ziliifanya kuwa ndege maarufu sana - licha ya umri wake mkubwa. An-72 na 74 zinaendelea kufanya kazi katika nchi nyingi. Nyingi za ndege hizi ziko Urusi na Iran. Zinatumiwa na waendeshaji wa kijeshi na raia.

Iran na Urusi ziko chini ya vikwazo vya kimataifa, ambavyo vimeathiri, miongoni mwa mambo mengine, hali ya ndege zao. Urusi, ambayo imekuwa ikijaribu kutengeneza ndege nyepesi ya Il-112V kwa jeshi lake la anga katika miaka ya hivi karibuni, haijawahi kufanikiwa kwa sababu ya shida za maendeleo na ajali ya 2021.

Usafiri wa anga wa Urusi unakabiliwa na matatizo zaidi na zaidi chini ya vikwazo hivyo, lakini ikizingatiwa kwamba An-74 ni ndege yenye sifa za kipekee ambayo ni vigumu kuchukua nafasi yake, haishangazi kwamba Warusi wanafanya kila jitihada ili kuimarisha ndege zake zilizozeeka kuendelea kufanya kazi .