Bayraktar TB2: Ifahamu silaha hii iliyopata soko kubwa barani Afrika

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ndege isiyo na rubani

Mataifa mengi ya Afrika yanazidi kununua ndege za kivita zisizo na rubani za Uturuki ili kupambana na makundi yenye silaha baada ya kuthibitisha kuwa zina ufanisi katika migogoro mbalimbali duniani, kulingana na mchambuzi Paul Melly.

Wakati Ukraine ilipoimarisha vita dhidi ya uvamizi wa Urusi nchini humo , na kabla ya kupokea silaha nzito nzito kutoka kwa washirika wake wa Magharibi , kulikuwa na silaha moja ambayo serikali ya Kyiv ilikuwa ikiitumia – nayo ni ndege isiyo na rubani ya Bayraktar TB2.

Silaha hii iliyotengenezwa nchini Uturuki tayari ilikuwa imethibitisha ufanisi wake baada ya kuisaidia Azerbaijan kulishinda jeshi la Armenia na kukomboa eneo kubwa la vita vya Nagorno-Karabakh 2020.

Lakini wanaovutiwa na silaha hii hawako Ulaya Mashariki pekee.

Wiki za hivi karibuni zimeshuhudia shehena ya Bayraktar TB2 ikipelekwa katika bara la Afrika hususan Magharibi mwa Togo, ambapo taifa hilo linajitahidi kuwazuia wapiganaji wa kijihadi kutohamia katika taifa hilo kutoka Burkina Faso.

Mwezi Mei, Niger ilipata nusu dazeni ya ndege hizi zisizo na rubani zinazoweza kutumika kwa wingi kwa bei nafuu kwa ajili ya operesheni zake za kijeshi dhidi ya makundi ya waasi katika eneo la Sahel kusini mwa Jangwa la Sahara, na karibu na Ziwa Chad.

Wateja wengine wa bara Afrika wamejumuisha Ethiopia, Morocco na Tunisia, wakati Angola pia ikiwa na niya kununua.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Bayraktar TB2

Lakini Bayraktar TB2 ni silaha ya aina gani?

Bayraktar TB2

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Bayraktar TB2

Ndege hizi zisizo na rubani zinasemekana kuwa na uwezo mkubwa ikilinganishwa na zile zinazoundwa na mataifa mengi.

Iliundwa na Bayraktar Pamoja na mwana wa kambo wa rais wa Uturuki Tayyib Erdogan.

Waundaji hao kwasasa wanafanya opersheni zao nchini Uturuki , Qatar, Ukraine na Azerbaijan.

Bayraktar TB2 yenye uziko wa kilo 150 imeundwa kutekeleza mashambulizi na inaweza kusafiri kwa umbali wa kilomita 300.

Kulingana na kampuni iliotengeneza ndege hiyo, ina urefu wa mita 12 na inaweza kubeba mafuta ya lita 300.

Ndege hiyo ina uwezo wa kubeba makombora makubwa manne.

Teknolojia ya Bayraktar TB2

Ina mfumo wa kiufundi wa hali ya juu ambao unaweza kutoa suluhu zote ambazo mmiliki wake anaweza kuhitaji wakati wa vita - mfumo unaojumuisha kila kitu .

Mfumo huu una data ya ardhini, kamera zinazoweza kunasa mbali, msingi wa hali ya Juu wenye moduli za Jenereta na Trela. Vilevile silaha hiyo imethibitishwa kuwa na uwezo wa kuruka saa 400. Tangu mwaka 2014, imefanikiwa kutekeleza operesheni zake chini ya usimamizi wa jeshi la Uturuki.