Vita vya Ukraine: Ndege ya kivita ya Urusi yasambaratisha jiji la nchi hiyo kwa bahati mbaya

Chanzo cha picha, Getty Images
Wizara ya ulinzi mjini Moscow imesema ndege ya kivita ya Urusi ilishambulia kwa bahati mbaya mji wa Belgorod ulioko karibu na mpaka wa nchi hiyo na Ukraine.
Gavana wa eneo la Vyacheslav Gladkov alisema shambulio hilo limesababisha shimo kubwa lenye upana wa takriban mita 20 (futi 60) katikati mwa jiji.
Wanawake wawili walijeruhiwa na majengo kadhaa kuharibiwa vibaya, alisema.
Ndege hiyo ya kivita aina ya Su-34 ilirusha bomu la anga kwa bahati mbaya, haikuwa lengo kushambulia mji huyo, wizara ilisema.

Chanzo cha picha, Getty Images
Tukio hilo lilitokea saa 4:15 usiku kwa saa za ndani (19:15 GMT) siku ya Alhamisi kuamkia Ijumaa, mashirika ya habari ya Urusi yalisema.
Uchunguzi unaendelea.
Picha na video kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha maeneo ya vyumba vilivyoharibiwa na mlipuko huo, huku picha moja ikionyesha gari likiwa juu ya paa la jengo moja.

Chanzo cha picha, Getty Images
Belgorod - jiji lenye watu 370,000 - liko karibu maili 25 (kilomita 40) kutoka mpaka wa Ukraine. Liko kaskazini mwa mji wa pili wa Ukraine, Kharkiv, na watu huko wamekuwa wakiishi kwa hofu ya mashambulizi ya makombora ya Ukraine tangu Urusi iivamie Ukraine mwaka jana.
Ndege za Urusi pia huonekana mara kwa mara kwenye anga la jiji hilo zikielekea Ukraine.












