Uchaguzi wa Marekani 2024: Je, kuna pengo la kijinsia katika uchaguzi huo?

- Author, Katty Kay
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Kwa mujibu wa kura ya maoni, Donald Trump ana uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa wanaume, huku wanawake kwa sehemu kubwa wakisema watampigia kura Kamala Harris. Pengo la kijinsia linaweza kusaidia kuamua uchaguzi wa Marekani.
Harris ni mwanamke wa kwanza mweusi kupata uteuzi wa kugombea urais, na mwanamke wa pili wa chama cha Democratic kufika hatua hiyo.
"Ninaamini mimi ndiye mtu bora zaidi kuwa rais kwa wakati huu kwa Wamarekani wote, bila kujali rangi na jinsia," makamu huyo wa rais alisema katika mahojiano ya CNN mwezi uliopita.
Licha ya juhudi zake zote za kuepusha mjadala kuhusu jinsia yake, bado mada hiyo inaendelea kuwa suala kubwa katika kampeni hii.
Timu ya kampeni ya Harris haitasema hadharani, lakini afisa mmoja alikiri kwangu hivi karibuni kwamba wanaamini kuna "ubaguzi wa kijinsia uliofichwa" ambao utawazuia baadhi ya watu kumpiga kura mwanamke yeyote kuwa rais.
Ni 2024, ni watu wachache ambao watakuwa wajinga kumwambia moja kwa moja mkusanya data kwamba, hawafikirii mwanamke kwamba anafaa kuwa rais wa Marekani. Lakini wako tayari kuchapisha meme ya chuki dhidi ya wanawake kwenye mitandao ya kijamii.
Mtaalamu wa mikakati wa chama hicho anasema kuna siri, wapiga kura wanapowaambia wakusanya data kwamba Harris hayuko "tayari" au hafai," wanachomaanisha, tatizo yeye ni ni mwanamke.
Kuna pengo la kijinsia?

Chanzo cha picha, Getty Images
Timu ya kampeni ya Trump inasema jinsia haina uhusiano wowote. "Kamala ni dhaifu, si mwaminifu, na ni mliberali hatari, na ndiyo sababu watu wa Marekani watamkataa Novemba 5," timu hiyo ilisema wiki hii.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Lakini Bryan Lanza, mshauri mkuu wa timu hiyo ya kampeni, alinitumia ujumbe mfupi akisema ana uhakika Trump atashinda kwa sababu "jinsia ya kiume inatupa faida."
Mara ya mwisho mwanamke kugombea urais, ilikuwa ni miaka minane iliyopita – pale Hillary Clinton alipokuwa mwanamke wa kwanza kuteuliwa na Democratic.
Mengi yamebadilika kwa wanawake tangu 2016. Vuguvugu la #MeToo la mwaka 2017 liliongeza ufahamu kuhusu ubaguzi ambao wanawake wanaupitia kazini. Ilibadilisha namna tunavyozungumza juu ya wanawake. MeToo inaweza kuwa imerahisisha mgombea kama Harris kupata uteuzi.
Pengo la kijinsia limefunguliwa katika kinyang'anyiro hiki, matokeo ya kura ya maoni ya CBS News yaliyotolewa Jumapili, yanaakisi mitazamo ya Wamarekani kuhusu majukumu ya kijinsia.
CBS iliripoti kwamba wanaume wana uwezekano mkubwa wa kusema juhudi za kukuza usawa wa kijinsia nchini Marekani zimekwenda mbali sana; wana uwezekano mkubwa wa kuwa wafuasi wa Trump.
Wanawake wana uwezekano mkubwa wa kusema juhudi hizo hazijatosha - na wanaelekea kumuunga mkono Harris.
Wanaume pia wana uwezekano mdogo kuliko wanawake kufikiria Harris atakuwa kiongozi mwenye nguvu, CBS iliripoti, kwamba wanaume wengi wanafikiri Trump atakuwa kiongozi mwenye nguvu.
Kwa hivyo, kwa baadhi ya wapiga kura, uchaguzi huu wa Novemba umegeuka kuwa kura ya maoni kuhusu kanuni za jinsia.
Vijana wa kiume na kike
“Mara nyingi wanaume vijana huhisi – ikiwa watauliza maswali watapachikwa tuhuma kwamba wanachukia wanawake, wanachukia wapenzi wa jinsia moja au wabaguzi wa rangi,” anasema John Della Volpe, mkurugenzi wa kura za maoni katika Taasisi ya Siasa ya Harvard.
"Wakiwa wamechanganyikiwa, wengi hujiingiza kwenye utamaduni wa Donald Trump au Elon Musk. Wanaangalia chama cha Democratc kinawapa kipaumbele - wanawake, haki za uavyaji mimba, LGTBQ - na wanauliza 'vipi kuhusu sisi?'
Della Volpe anasema vijana anaowataja si sehemu ya baadhi ya watu wenye msimamo mkali, wengi wanaunga mkono usawa kwa wanawake, lakini pia wanahisi shida zao hazisikilizwi.
Della Volpe anachambua orodha ya takwimu zinazoonyesha jinsi vijana wa kiume leo walivyo na hali mbaya zaidi kuliko wenzao wa kike; wana uwezekano mdogo wa kuwa kwenye uhusiano, wana uwezekano mdogo wa kujiandikisha chuo kikuu kuliko ilivyokuwa zamani, wana viwango vya juu vya kujiua kuliko wenzao wa kike.
Wanawake vijana wa Marekani wakati huo huo wanasonga mbele. Wana elimu bora kuliko wanaume, wanafanya kazi kwenye tasnia ambazo zinakua na kuzidi kupata mapato zaidi kuliko wanaume.
Katika kipindi tangu Donald Trump achaguliwe kuwa rais, wanawake vijana pia wamekuwa waliberali zaidi kuliko vijana wa kiume, kulingana na kura ya maoni ya Gallup.
Katika kipindi cha miaka saba iliyopita, idadi ya vijana ambao wanasema Marekani imekwenda "mbali sana" katika kukuza usawa wa kijinsia imeongezeka zaidi ya mara mbili, kulingana na Taasisi ya American Enterprise.
Wanawake na wanaume

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa ufahamu wake kuhusu kutoridhika kwa wanaume, Trump ameziba pengo kwenye mfadhaiko huo, na katika wiki za mwisho za kampeni yake ameongeza maradufu kauli kwa wanaume. Alichapisha tena onyo kwenye mtandao wa kijamii wa Truth akidai "Uanaume unashambuliwa."
Katika mikutano yao, majibu ya Democratic kwa wanaume waliokata tamaa yanaonekana ni mgumu. Barack Obama alisema baadhi ya wanaume "hawataki wazo la kuona mwanamke kawa rais."
Katika tangazo jipya la TV, Mwigizaji Ed O'Neill amekuja na kauli ya moja kwa moja: "Kuwa mwanaume: Mpigie kura mwanamke."
Tukielekea siku za mwisho za kampeni ya uchaguzi, jinsia iko kila mahali – lakini haionekani. Donald Trump anataka uanaume kuwa ndio kitovu cha mbio hizi. Kamala Harris anakiri kuwa yeye ni mwanamke anayegombea wadhifa huo.
Katika kura ya maoni ya New York Times, Trump anaongoza miongoni mwa wapiga kura wanaume kwa 14%. Harris anaongoza miongoni mwa wanawake kwa 12%.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi












