Jinsi uhusiano wa Obama na Harris ulivyosaidia kuwakuza kisiasa

Chanzo cha picha, Getty Images
Walikutana miaka 20 iliyopita huko California na tangu wakati huo wamefanya kazi pamoja kuendeleza taaluma zao za kisiasa.
Barack Obama, 63, na Kamala Harris, 59, wamekuwa katika mizunguko ya kisiasa inayoingiliana tangu alipokuwa akipigia kampeni Useneti wa Marekani mnamo 2004.
Harris alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kuunga mkono ugombea wake na, miaka michache baadaye, mnamo 2008, alijitolea kwenye kampeni iliyomfanya Obama kuwa rais wa kwanza mweusi wa Marekani.
Sasa mshirika wake wa chama cha Democratic anarudisha neema hiyo kwa kumuunga mkono kuwa rais wa kwanza mwanamke nchini humo.
"Mpendwa wangu, rafiki yangu mpendwa," ni mojawapo ya maneno ambayo Obama ametumia hadharani kumrejelea, akiweka wazi kuwa uhusiano wao unaenda zaidi ya uwanja wa kisiasa.
Akiongea katika Kongamano la Kidemokrasia mwezi Agosti, rais huyo wa zamani alisema Harris "hakuzaliwa na fursa," akivuta uhusiano kati ya maisha yake na yale ya mgombea.
Na huku kampeni zikiisha, Obama ameahidi kufanya "kila linalowezekana" kumsaidia kushinda urais , ikiwa ni pamoja na ushauri wa kimkakati, uchangishaji fedha na juhudi za kuwafanya watu wakapige kura kwenye uchaguzi Novemba 5.
Hapa kuna nyakati sita muhimu katika uhusiano wa kisiasa wa Harris na Obama.
1. Obama anazindua kampeni yake kuelekea Ikulu ya White House mnamo 2007

Chanzo cha picha, Kamala Harris - Facebook
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Harris, ambaye wakati huo alikuwa wakili wa San Francisco, alikuwa miongoni mwa umati wa zaidi ya watu 15,000 wakati seneta huyo alipotangaza nia ya kushangaza ya mbio za kuelekea Ikulu ya White House kwenye ngazi za Ikulu ya Jimbo kuu katika mji mkuu wa Illinois wa Springfield mnamo Februari 2007.
Kisha aliendelea kubisha hodi na kutafuta pesa kwa ajili ya Obama kabla ya mchujo wa 2008 Iowa, na baadaye kuhudumu kama mwenyekiti mwenza wa kampeni yake huko California.
Obama alishiriki naye miaka miwili baadaye, wakati Harris alipogombea wakili mkuu wa California dhidi ya Steve Cooley wa Republican, wakili maarufu wa Los Angeles.
Wakati huo, mtangazaji wa PBS Gwen Ifill alikuwa amemtaja kama "Barack Obama wa kike," lakini Harris alisalia katika kinyang'anyiro kikali.
Ili kuipa kampeni yake msukumo mwingine, Obama, ambaye alishindwa katika Bunge la Congress mwaka huo wa uchaguzi, ilimpa muda wa kutokea kwenye mkutano wa hadhara huko Los Angeles mnamo Oktoba 2010, ambapo alimtaja Harris kama "mpendwa, rafiki yangu mpendwa."
"Nataka kila mtu afanye sawa naye," aliuambia umati. Harris alishinda kwa chini ya asilimia ya moja, na kujiweka tayari kuelekea kushika nafasi ya juu.
2. Hotuba ya Harris katika kongamano la 2012

Chanzo cha picha, Getty Images
Obama alimpa Harris nafasi ya kuzungumza katika Kongamano la Kitaifa la Kidemokrasia la 2012 huku rais akitafuta kuchaguliwa tena.
Tayari alikuwa amejitengenezea jina huko California kama mtu wa kwanza wa rangi au mwanamke kuhudumu kama wakili wa jimbo la San Francisco. Pia alikuwa mwanamke wa kwanza mweusi na mwanamke mwenye asili ya Asia Kusini kuchaguliwa kuwa wakili mkuu wa serikali.
Akiwa mwanasheria mkuu, aligonga vichwa vya habari kwa kusimamia kidete mazungumzo ya kufikia suluhu ya kifedha kati ya wanasheria wakuu wa serikali na benki zinazohusika na mgogoro wa mikopo ya nyumba, na kupata zaidi ya dola bilioni 25 kwa niaba ya wamiliki wa nyumba.
Katika mkutano huo, Harris alizungumza kuhusu mafanikio yake, akiandika hadithi yake binafsi, akimsifu Obama kwa kuwatetea Wamarekani wakati wa mzozo wa makazi na kumshambulia mpinzani wake wa Republican, Mitt Romney, kama mshirika wa Wall Street.
"Tunahitaji kusonga mbele," alisema katika hotuba yake, maneno ambayo amerudia katika kampeni yake ya 2024.
"Rais Obama atapigania familia zinazofanya kazi. Atapigana kusawazisha uwanja wa kiuchumi na kutoa kila Mmarekani fursa sawa na familia yangu."
Hotuba yake ilikuja muda mfupi kabla ya matamshi ya Rais wa zamani Bill Clinton na kumfanya apate nafasi ambayo hakika ilivuta hisia za Wanademokrasia wa kitaifa, watu wenye ushawishi na wafadhili wakuu.
3. Obama anamuita "mwanasheria mkuu aliye mrembo zaidi''

Chanzo cha picha, Getty Images
Ingawa Obama alimuunga mkono Haris kimyakimya alipopanda ngazi za siasa za California, alishangaza kila mtu mwaka wa 2013 alipomwita "mwanasheria mkuu mrembo zaidi nchini."
"Lazima uwe mwangalifu, kwanza kabisa, kusema kwamba yeye ni mzuri, anayejitolea na mwenye kujiamini, na ndivyo ungetarajia kutoka kwa mtu anayesimamia sheria na kuhakikisha kuwa kila mtu anatendewa haki," rais wa wakati huo alisema katika hafla ya uchangishaji fedha huko San Francisco.
"Pia ni mwanasheria mkuu mrembo zaidi nchini."
Saa kadhaa baadaye alimpigia simu Harris kumuomba msamaha kwa maoni hayo.
"Hao ni marafiki wa zamani na marafiki wazuri na hakutaka kudharau kwa vyovyote vile" mafanikio yao, msemaji wa Ikulu ya wakati huo Jay Carney baadaye aliwaambia waandishi wa habari.
4. Obama anamuunga mkono anapowania useneta mwaka wa 2016
Mnamo 2016, katika kilele cha mamlaka yake ya Democratic na kukaribia mwisho wa muhula wake wa pili akiwa rais, Obama aliingilia kati kinyang'anyiro kikali cha Seneti ya California kumuunga mkono Harris, ambaye alikuwa akitangaza nia kuchukua nafasi ya Seneta Barbara Boxer aliyekuwa anaondoka.
Mnamo Julai mwaka huo, yeye na makamu wake wa rais, Joe Biden, walitangaza rasmi kumuunga mkono Harris, ambaye alikuwa akigombea dhidi ya Mdemokrat mwenzake na Mbunge wa Marekani Loretta Sanchez.
Katika mfumo wa msingi wa California, wagombea wawili walio na kura nyingi zaidi huingia kwenye uchaguzi mkuu, bila kujali chama wanachowakilisha.
"Kamala ni mwendesha mashtaka wa muda mrefu na mwenye mteja mmoja: watu wa jimbo la California. Hiyo ndiyo njia ambayo atachukua katika Seneti ya Marekani," Obama alisema katika taarifa iliyotolewa na kambi ya Harris.
Biden alisema alimfahamu kupitia mwanawe Beau Biden, ambaye, alipokuwa mwanasheria mkuu wa Delaware, alianzisha urafiki naye.
Harris alishinda uchaguzi kwa raha na akawa mwanamke wa pili mweusi kuhudumu katika Seneti ya Marekani.
5. Ushindi wa 2020 na makamu wa rais wa kwanza mwanamke

Chanzo cha picha, Getty Images
Kampeni za msingi za urais za 2020 za Harris zilianza na tukio katika mji wake wa Oakland, California, mbele ya umati wa watu 20,000 mnamo 2019.
Sawa na wagombea wengine wa uteuzi wa chama cha Democratic, alikutana na Obama kutoa hoja yake kuhusu kugombea kwake.
Lakini Obama, ambaye makamu wake wa rais alikuwa akitayarisha azma ya kugombea urais, alitaka kujiondoa kwenye kinyang'anyiro cha kisiasa na kusubiri hadi chama kitakapomchagua mgombea wake kabla ya kutoa uidhinishaji
Kambi ya Harris iliporomoka katika kipindi cha chini ya mwaka mmoja, na Joe Biden alimpa aina fulani ya zawadi ya kisiasa kuwa mgombea mwenza wake.
Obama alimuunga mkono Biden uteuzi wa Harris.
"Kumchagua makamu wa rais ni uamuzi mkubwa wa kwanza ambao rais hufanya. Unapokuwa katika Ofisi ya Oval, ukizingatia masuala magumu na kujua kwamba uamuzi unaofanya utaathiri maisha ya nchi nzima, unahitaji mtu pamoja nawe. ambaye ana uamuzi na tabia ya kufanya chaguo sahihi," Obama alisema katika taarifa yake.
Tangu 2020, Obama amekuwa akiwasiliana mara kwa mara na Harris, akitoa ushauri na kutenda kila anapoomba.
6. Uungaji mkono wa Obama mwaka wa 2024 baada ya Biden kujiuzulu

Chanzo cha picha, Harris 2024 Campaign
Barack Obama na mkewe, Michelle, walisubiri siku kadhaa kumuidhinisha Harris baada ya Joe Biden kujiuzulu kuwa mgombea tena, hadi ilipobainika kuwa hakuna wapinzani na kwamba yeye ndiye chaguo la chama.
Wanandoa hao walichapisha video yao wakimwita kutangaza rasmi kumuunga mkono kwenye kampeni yake.
"Tumefahamiana kwa miaka 20. Nimekutazama ukiwa bora katika kila nafasi uliyoshikilia," Obama alimwambia kwenye simu.
"Kuona tu kazi hiyo ngumu inatambulika ni jambo ambalo tunalifurahia sana. Kwa hivyo jambo kuu tulilotaka kusema ni kuwa tutafanya kila kitu kumsaidia kuwa rais."
Wawili hao wamekuwa na mawasiliano ya karibu katika miezi ya hivi karibuni, huku Obama akiunga mkono kampeni yake, ikiwa ni pamoja na ushauri wa kisiasa na kimkakati, kutafuta fedha na juhudi za kuhamasisha watu kupiga kura.
Harris pia ameomba usaidizi wa washirika wengi wa muda mrefu wa Obama katika kuendesha kampeni yake.
Eric Holder, ambaye aliwahi kuwa mwanasheria mkuu wa Marekani chini ya Obama, aliongoza juhudi za kuhakiki orodha ya Harris ya wagombea makamu wa rais, huku David Plouffe, meneja wa kampeni wa Obama mwaka 2008, sasa ni mmoja wa washauri wake wakuu.
Kambi ya Harris pia imeajiri washirika wengine wa Obama, akiwemo Jennifer O'Malley Dillion, meneja wake wa kampeni, na mshauri mkuu Stephanie Cutter. Aliyekuwa mkurugenzi wa mawasiliano wa Obama Jennifer Palmieri pia anamsaidia mume wa Harris, Doug Emhoff.
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga na kuhaririwa na Ambia Hirsi












