Uchaguzi wa Marekani 2024: Je, sera za Trump na Harris zitakuwaje kuhusu Mashariki ya Kati?

sd

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Rafid Jaboori
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Kipi kitatokea Mashariki ya Kati iwapo Trump atarejea kwenye kiti cha urais? Vipi kuhusu mpinzani wake Kamala Harris?

Suala la vita vya Gaza ni jambo muhimu katika uchaguzi huu. Harris anahitaji kushinda katika jimbo la Michigan na Pennsylvania ili kushinda urais.

Na katika majimbo yote mawili kuna asilimia kubwa ya wapiga kura wa Waarabu na Waislamu ambao wanaunga mkono usitishwaji wa vita huko Gaza.

Na kuwapuuza kunaweza kusababisha kutopiga kura au kumpigia kura mgombea wa chama kingine mbali na Trump au Harris, na hilo linaweza kuongeza nafasi ya Trump kushinda.

Kwa upande wake Trump amezungumzia machache kuhusu Gaza. Lakini kauli zake haziashirii kuwa ana uhitaji wa kura za wale wanaounga mkono Palestina. Je, sera zao kwa ujumla juu ya Mashariki ya Kati zinaweza zikawa katika sura gani kwa wagombea wote wawili?

Pia unaweza kusoma

Trump na Mashariki ya Kati

sd

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Trump katika mkutano na Netanyahu

Trump alifanya ziara yake ya kwanza ya kigeni kama rais katika Ufalme wa Saudi Arabia. Anaiona Mashariki ya Kati kama eneo kubwa la maslahi na ushawishi, huku akiwaambia Wamarekani "vita vya Gaza visingetokea kama angekuwa rais wa Marekani.”

Labda ni kwa sera ya kuishinikiza Iran ambayo aliichukua wakati wa utawala wake, sera iliyosababisha kudhoofika kwa uchumi wa Iran, na pengine isingekuwa na uwezo wa kuinga mkono Hamas kiasi cha kufanya shambulio la Oktoba 7.

Trump daima anarejelea makubaliano ya kurekebisha uhusiano ambayo utawala wake uliyasimamia kati ya Israel na nchi nne za Kiarabu: UAE, Bahrain, Morocco, na Sudan, kama mafanikio makubwa ya kidiplomasia na ushahidi. Na makubaliano mengine kama hayo yatakuja ikiwa atarejea kwenye kiti cha urais.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Trump aliiondoa Marekani kwenye makubaliano ya nyuklia ambayo utawala wa mtangulizi wake Obama uliyafanya kwa miaka kadhaa. Trump aliweka sera ya shinikizo kubwa la kiuchumi kwa kuzidisha vikwazo dhidi ya Tehran.

Alitoa amri ya kuuawa Qassem Soleimani, kamanda wa kitengo cha Al-Quds cha jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran, katika pigo kubwa zaidi ambalo Iran imepokea kutoka Marekani katika kipindi chote cha miaka ya mvutano kati yao.

Wakati ambapo hali ni ya wasiwasi kati ya Iran kwa upande mmoja na Israel na Marekani kwa upande mwingine, kurejea kwa Trump kunaweza kusiwe na maana ya vita kati ya Marekani na Iran. Badala yake, Trump anadokeza kwamba anaweza kufikia makubaliano na Iran lakini kwa masharti yake mwenyewe.

Kurejea kwa Trump katika kiti cha urais huenda kukafungua milango ya hatua za kushangaza katika nchi zenye migogoro kama Iraq, Syria, Lebanon na Yemen.

Paul Salem, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mashariki ya Kati, anasema Trump anaweza kujiondoa kijeshi Syria na labda Iraq.

KwaTrump, haijalishi ni nani atamchagua kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, yeye mwenyewe ndiye atabaki kuwa mwamuzi wa mwisho kuhusu sera za nje.

Harris na Mashariki ya Kati

WESD

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kamala Harris wakati wa mkutano wake na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu

Wakati akiwa Makamu wa Rais, Kamala Harris hakuzungumzia sera za kimkakati na mipango ya Mashariki ya Kati, lakini ikiwa atashinda urais, atajikuta katika nafasi ambayo atalazimika kuizungumzia Mashariki ya Kati.

Katika miezi ya hivi karibuni, Harris ameanza kuchukua hatua zinazomtofautisha kidogo na Rais Joe Biden. Alikuwa afisa wa ngazi ya juu wa kwanza wa Marekani kutoa wito wa kusitishwa kwa mapigano huko Gaza, baada ya Washington kupinga wazo la kusitisha mapigano kwa miezi kadhaa hadi kampeni ya Israel ifikie malengo yake.

Wakati Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alipotembelea Washington Julai 2024, hotuba ya Harris kwa Netanyahu na ulimwengu ilikuwa ya wazi zaidi na yenye maamuzi, aliposema vita vikome mara moja. Hili, bila shaka, bado halijafikiwa.

Na haitarajiwi kwamba sera ya Marekani ya kuunga mkono Israel itashuhudia mabadiliko makubwa ikiwa Harris atakuwa rais, lakini mabadiliko ya harakati na mbinu yanaweza kutokea, jambo ambalo Biden hakufanikiwa.

Suala la Palestina limekuwa sehemu ya mzozo wa ndani wa Chama cha Democratic cha Harris na Biden. Mrengo wa kushoto wa chama chake unataka mabadiliko katika sera ya Marekani kuelekea Israel, na wapiga kura Waarabu na Waislamu wa Marekani, wanadai mabadiliko kwa nguvu.

Harris alijikuta uso kwa uso na changamoto hiyo, katika mkutano huko Michigan, wanaharakati wanaoiunga mkono Gaza walikatiza hotuba yake, kwa kuimba nyimbo na kuelezea upinzani wao dhidi ya sera ya Marekani. Aliwakabili kwa kutomuunga mkono yeye, ingepelekea Donald Trump kushinda na wanapaswa kutambua hilo na kumwacha aendelee kuzungumza.

Kuhusu Iran, Harris alikuwa sehemu ya utawala wa Biden, ambao ulijaribu kurejesha makubaliano ya nyuklia na Iran. Ikiwa Harris atakuwa rais, atafuata mtindo huu, lakini yeye na timu yake watalazimika kuwasilisha mipango mipya ya kusonga mbele.

Robert Satloff, mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Karibu huko Washington, anaamini rais ajaye, awe Harris au Trump, anaweza kukabiliwa na mtihani mkubwa wa kutoiruhusu Iran kumiliki silaha za nyuklia. Na kuchukua njia zote zinazohitajika kuzuia hilo kutokea.

Kuhusu sera ya Harris, ikiwa atakuwa rais, sera zake kwa mataifa ya Ghuba, haswa Saudi Arabia, zitabaki zile za enzi ya Biden, ambapo Saudia ilikuwa ni mshirika. Licha ya Biden kuanza kwa mtazamo mkali dhidi ya Saudi Arabia na kisha akarudi kwenye sera ya jadi ya kuwa mshirika wa Riyadh.

Kwa hiyo, uhusiano kati ya utawala wa Harris na Saudi Arabia huenda ukaimarika, hasa kwa vile kuna misingi ya pamoja ya kihistoria na maslahi kati ya nchi hizo mbili.

Chaguo la Harris kuhusu nani atachukua nafasi ya Waziri wa Mambo ya Nje litakuwa muhimu. Waziri wa sasa wa Mambo ya Nje, Anthony Blinken, alikuwa msaidizi wa karibu wa Biden, alipewa nafasi hiyo kwa sababu anaijua Mashariki ya Kati, haiba yake, na siasa zake. Harris anaweza kumbakisha ofisini.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla