Iran inatumia mkakati gani kuidhibiti Mashariki ya Kati?

Chanzo cha picha, REUTERS
Katika gazeti la Yedioth Ahronoth kuna makala iliyoandikwa na Avigdor Haselkorn yenye kichwa cha habari, "Kufichua Mkakati wa Iran wa Kuidhibiti Mashariki ya Kati."
Avigdor, mtaalamu wa masuala ya usalama wa taifa, anaanza makala yake kwa kusema, Iran inatumia mabilioni ya dola kusaidia washirika wake katika eneo hili.
Lengo ni kutekeleza mpango wenye tija kubwa, ambao pia umeandikwa katika katiba ya Iran, ili kuonyesha uwezo wake Mashariki ya Kati.
Matokeo ya dira hii, ambayo ilitengenezwa ili kuidhibiti Mashariki ya Kati, sasa yanaonekana yako wazi. Malengo yake ni mawili - kuunda ushawishi ili kulinda utawala wa Kishia uliozungukwa na tawala za Sunni.
Pili, ni kuyapeleka Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran nje ya Iran, chini ya itikadi ya mwanzilishi wake, Ruhollah Khomeini, ambayo ni "kueneza mapambano dhidi ya watu wenye kiburi duniani kote.”
Kulingana na mwandishi, mikakati hiyo hutumia mambo manne:
Vita vya mawakala: Licha ya mizizi ya kihistoria ya vita vya aina hii, Iran imeunda vikosi vingi (huko Gaza, Lebanon, Syria, Iraq na Yemen). Ambavyo hupigana kwa ajili ya maslahi ya taifa hilo.
Kukwepa Kuwajibika: Kutumia mawakala wa vita sio tu huilinda Iran, pia inairuhusu kukwepa sheria za vita na kukwepa kuwajibika kwa sababu wale wanaofanya mapigano halisi ni "makundi huru."
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mataifa, haswa yale yaliyotia saini Mkataba wa Geneva 1949, hufuata sheria za vita hata wakati wa kupigana na "makundi ya kigaidi," ingawa makundi ya mawakala hayafuatia mkataba huo.
Mbinu za Kale za Vita: Wakati Israel inatumia mabilioni ya fedha ili kupata na kutengeneza silaha za teknolojia ya hali ya juu ili kudumisha ubora wa jeshi lake, Iran, iliyo chini ya vikwazo vikali vya kimataifa, inatumia teknolojia za hali ya chini za bei nafuu.
Malengo tofauti: Mashambulizi ya mawakala wa Iran yanalenga kufikia malengo tofauti kabisa na malengo ya kijeshi ya Israel.
Wakati IDF kwa ujumla inalenga kuharibu uwezo wa adui wa kupigana, makundi hayo yanapigana kudhoofisha nia ya Waisraeli ya kupigana.
Mwandishi anahitimisha kwamba Iran imeunda mkakati uliofanikiwa wa kutanua ushawishi Mashariki ya Kati baada ya kuchukua udhibiti wa nchi nne - Lebanon, Syria, Iraq, na Yemen - hata hivyo, mpango huo unakabiliwa na changamoto baada ya matukio ya Oktoba 7.
Kupitia vita vyake dhidi ya Hamas na Hezbollah, Israel huenda itazuia mpango mzima wa kijiografia wa Iran. Hivi sasa inasambaratisha mkakati wa makundi ya Iran.
Lakini ili kushinda mzozo huo, baada ya kushinda vita dhidi ya Iran, mwelekeo wa itikadi za kidini lazima pia ukabiliwe.
Kura ya maoni juu ya serikali za Magharibi

Chanzo cha picha, REUTERS
Gazeti la Washington Post lina makala iliyoandikwa na mwandishi wa habari wa masuala ya Ulaya Lee Hockstadter, yenye kichwa cha Habari, “Kwa Nini Machafuko Mapya ya Kisiasa Barani Ulaya Yatampendeza Putin?”
Mwandishi anawazia tabasamu kwenye uso wa Rais wa Urusi Vladimir Putin kutokana na machafuko ya hivi karibuni yaliyotikisa Ulaya.
Nchi mbili zenye ushawishi mkubwa barani Ulaya, Ufaransa na Ujerumani, ziko katika hatua ya mwisho ya kuporomoka kisiasa - kufuatia ushindi wa kishindo wa Wafaransa wanaounga mkono Urusi katika uchaguzi wa Bunge la Ulaya.
Nchini Ujerumani, mrengo wa kulia, ambao unaunga mkono Urusi, ulipata kura nyingi kuliko chama cha Kansela Olaf Scholz.
Mwandishi anadokeza kwamba uchaguzi wa Ulaya kimsingi ni kura ya maoni kwa serikali za kila nchi, na hakuna chama kilichoweza kushinda hata asilimia 15 ya kura katika uchaguzi wa Jumapili.
Na hakuna hata chama kimoja chenye wingi wa kuliongoza bara hilo mbele ya tishio la Urusi.
Anaeleza kuwa Macron, aliyekuwa akijaribu kuuhamasisha muungano wa Ulaya kutuma wakufunzi wa kijeshi nchini Ukraine wiki iliyopita, bado hajapata mafanikio hadi sasa, kuhamasisha muungano huo.
Schulz, ameshindwa kuendesha muungano wa vyama vitatu, pia hana ushawishi madhubuti mjini Berlin, kwani wawekezaji wa kigeni wanaidhihaki serikali yake na kuielezea kama ya "kijinga," ambayo inaharibu uchumi.
Huku Putin, kwa mtazamo wa mwandishi, akionekana kudhamiria zaidi kuutisha, kuuvuruga na kuusambaratisha muungano wa nchi za Magharibi, ambao tayari unakabiliana na migawanyiko ya ndani na kusambaratika kwa makubaliano ya kisiasa katika mipaka yake.
Hili lilimfanya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Anthony Blinken, kuonya kuhusu kampeni ya Kremlin, ambayo alisema inajumuisha sio tu mashambulizi ya mtandaoni, lakini pia "kuharibu usambazaji bidhaa na kupuuza mipaka ya baharini na nchi kavu hadi katika eneo la Baltic."
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla












