Bigmouth buffalo: Samaki wa ajabu anayeishi kwa karne bila ya kuzeeka

fd

Chanzo cha picha, Alec Lackmann

    • Author, Hannah Seo
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Utafiti wa hivi karibuni unaonyesha samaki aina ya bigmouth buffalo wana maisha marefu na huzidi kuwa na afya bora kadiri wanavyozeeka. Lakini wanasayansi wana wasiwasi kuwa idadi yao inazidi kupungua.

Katika ufuo wa Ziwa Rice huko Minnesota, Marekani katika mwezi wa Mei, unaweza kuona makundi makubwa ya samaki hawa katika mimea kwenye maji yenye kina cha futi chache.

Hawa ni samaki wa bigmouth buffalo, na ndio samaki wa maji baridi wanaoishi kwa muda mrefu zaidi duniani. Wengine wanaishi kwa zaidi ya miaka 100.

Kila mwaka, samaki hawa - ambao wanaweza kuwa na uzito wa zaidi ya 50lb (23kg) - hutaga na kuzaana katika ziwa Rice.

Samaki hawa wana asili ya Amerika Kaskazini na wanapatikana Kusini mwa Saskatchewan na Manitoba nchini Canada hadi Louisiana na Texas nchini Marekani. Hawavuliwi sana kwa ajili ya kitoweo, hivyo sio muhimu kiuchumi.

Pia unaweza kusoma

Umri mrefu na afya bora

f

Chanzo cha picha, Alec Lackmann

Maelezo ya picha, Utafiti imeonyesha idadi kubwa ya samaki hawa katika Ziwa Rice huko Minnesota walizaliwa kabla ya mwisho wa Vita vya Pili vya Dunia

Utafiti katika miaka mitano iliyopita, unaonyesha wapo wanaoishi hadi umri wa miaka 127. Pia hawaonekani kuzeeka kadiri umri unavyosonga. Na ndio sababu ya kutopotea kwao hata baada ya vizazi vya kupungua.

"Ni mojawapo ya samaki wa kale duniani, na hakuna usimamizi au ulinzi wa spishi hii," anasema Alec Lackmann, mtafiti wa samaki katika Chuo Kikuu cha Minnesota, Duluth.

Lackmann aliongoza utafiti huo, uliochapishwa 2019. Kabla ya utafiti, ilifikiriwa kuwa samaki hao waliishi tu umri wa miaka 26.

Hutambua umri wa samaki kwa kutumia otolith, maumbo kama mawe yanayopatikana katika masikio ya aina nyingi za samaki. Kwa kuyapasua na kukata vipande vidogo vidogo, wanasayansi wanaweza kuhesabu na kuchambua umri sahihi wa samaki.

Utafiti uliochapishwa mwaka 2021, ulichunguza afya ya samaki hawa na kugundua kuwa hawazeeki kutokana na ukubwa wao wa umri, na badala yake wanazidi kuwa na afya bora.

Britt Heidinger, mtafiti na mwanabiolojia katika Chuo Kikuu cha Jimbo la Dakota Kaskazini, anasema samaki hawa wanaonekana kuimarika namna mwili unavyofanya kazi na kinga ya mwili huboreka kadiri wanavyozeeka.

"Bado kuna mengi ambayo hayajulikani kuhusu jinsi samaki hawa wanavyoweza kuwa na afya njema wakiwa na umri mkubwa," anasema Heidinger.

Wako wapi samaki wachanga?

dx

Chanzo cha picha, Alec Lackmann

Maelezo ya picha, Samaki hawa huzaa kwa mafanikio kila msimu katika Ziwa la Rice, lakini ushahidi unaonyesha samaki wachanga hutoweka
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kuna fumbo jingine linalojitokeza katika utafiti huu. Kwa kuwa idadi kubwa ya samaki waliotumika kama sampuli ya utafiti, walikuwa ni wenye umri mkubwa. Swali: Je, wako wapi samaki wachanga?

Katika utafiti wa Lackmann na wenzake, waliripoti 99.7% ya samaki waliotumika kama sampuli - 389 kati ya samaki 390 ni wenye umri mkubwa - zaidi ya miaka 50. Umri wa wastani ni 79, ikimaanisha samaki wengi katika kundi hili walizaliwa kabla ya mwisho wa Vita vya Pili vya Dunia.

Lakini kilichoshangaza, licha ya samaki hao kuzaana kwa mafanikio kila mwaka, na kuzaa samaki wachanga wengi, samaki hao wachanga hawaonekani. Samaki wachanga hawajaonekana kwa wingi kwa zaidi ya miaka 60, anasema Lackmann.

Watafiti wanaamini sababu ya kupunguza huku kwa samaki wachanga ni uwezekano wa kuwindwa na spishi zingine wanaozaa katika ziwa hili. Lakini utafiti zaidi unahitajika kujua ukweli wa hilo.

Kwa hakika, hadi sasa, hakuna anayejua jinsi pengo la sasa la miaka 60 lilivyoibuka. Na kwakuwa kizazi cha sasa kinazidi kuwa na umri mkubwa, samaki hawa wanaweza kuwa hatarini kutoweka.

Ulinzi na ufahamu ni muhimu, anasema Lackmann. Wataalamu wanatumai majimbo kama Minnesota yataweka mipaka inayohitajika katika uvuvi, wakati wanasayansi wanajifunza zaidi jinsi ya kuisaidia spishi hii.

Nadharia moja ya kwa nini samaki wachanga wanatatizika kuwa wakubwa ni kwamba kunaweza kuwa na aina fulani ya usumbufu wa makazi kupitia ujenzi wa mabwawa, anasema Lackmann.