Mjue samaki wa kwanza baharini aliyetangazwa kutoweka mwaka jana

m

Chanzo cha picha, Edda Aßel, Museum für Naturkunde Berlin

    • Author, Chris Baraniuk
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Mwaka jana, samaki aina ya stigaree Java, alikuwa samaki wa kwanza kutangazwa ametoweka kwa sababu ya shughuli za kibinadamu.

"Unaweza kuwaona wakiwa wamejizika chini ya mchanga," anasema Julia Constance mwanafunzi wa udaktari wa falsafa kutoka chuo kikuu cha Charles Darwin, huko Darwin, Australia.

Desemba iliyopita, Constance na wenzake walichapisha ripoti kuhusu Java, samaki ambaye hajarikodiwa na wanasayansi kuonekana kwake kwa zaidi ya miaka 160 – na walitangaza ametoweka.

Na baya zaidi, stingaree Java ndiye samaki wa kwanza wa baharini anayetajwa kuwa ametoweka kwa sababu ya shughuli za wanadamu.

Kuna sampuli moja tu ya samaki aina hiyo katika makumbusho. Alinunuliwa na mtaalamu wa wanyama kutoka Ujerumani, kwenye soko la samaki la Jakarta, Indonesia mwaka 1862.

Sampuli hiyo ipo katika Jumba la Makumbusho la Historia huko Berlin, Ujerumani - ana urefu wa sentimeta 33 (inchi 13), pamoja na mkia wake. Ana rangi ya hudhurungi iliyofifia. Ni samaki jike lakini haijuulikani ikiwa ni mdogo au mkubwa.

Ili kujua hilo, mtu analazimika kumpasua na kuchunguza viungo vyake vya uzazi. Kwa kuwa ni sampuli pekee, hilo halitafanyika.

Pia unaweza kusoma

Walijuaje?

Kuhusu uamuzi kwamba viumbe hao sasa wametoweka, Constance anasema yeye na timu yake walikusanya rekodi za shughuli za uvuvi kutoka Indonesia tangu 2001.

Kwa kutumia habari zote walizoweza kupata kuhusu stingaree java katika data zilizotolewa na Muungano wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira (IUCN), Constance na wenzake waligundua kuwa kuna uhakika wa 93.5% kwamba stingaree Java wametoweka.

IUCN, shirika la kimataifa linalokusanya na kutoa taarifa kuhusu hali ya viumbe duniani, lilichapisha matokeo ya tathmini hiyo kwenye tovuti yake.

Diego Biston Vaz, msimamizi mkuu wa samaki katika Makumbusho ya Asili ya London - ambaye hakuhusika katika utafiti - pia anataja taarifa za uchunguzi huko Indonesia zilizokusanywa tangu 2001 na anasema "IUCN iliweza kutangaza rasmi mwaka jana kuwa samaki hao wametoweka.”

Kwanini wametoweka?

r

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wanadamu wamesababisha kutoweka kwa takribani aina 198 za viumbe wenye uti wa mgongo tangu mwaka 1900 - ikiwa ni pamoja na aina mbalimbali za samaki wanaopatikana katika mito na maziwa.

“Sababu moja ya kuamini stingaree Java ndio samaki pekee wa baharini ambaye ametangazwa kutoweka ni kwamba makazi ya baharini hutoa nafasi bora zaidi kwa viumbe kuepuka mikono ya binaadamu kwa kujiondoa kwenye maeneo tunayoyafikia,” anasema Catherine Macdonald kutoka kituo cha uhifadhi wa samaki cha Chuo Kikuu Miami.

“Samaki hao huchukua muda mrefu kuzaliana. Stingaree Java wanaweza tu kuzaa watoto mara moja au mbili kwa mwaka,” anasema Constance. Hiyo inamaanisha usumbufu wowote kutokana na shughuli za binadamu - kama vile uvuvi - unaweza kuwa na athari mbaya kwao.

Nimemuuliza ikiwa inawezekana kwamba ugonjwa fulani au tukio jingine la asili, ndilo lilisababisha kutoweka kwa samaki hao.

"Hatuwezi kusema kwa 100%" kwamba hilo haliwezekani, ingawa nadhani, kwa kiasi kikubwa, sisi ndio tulihusika."

Taarifa za Kutosha

f

Chanzo cha picha, Alamy

Maelezo ya picha, Samaki huyu hutumia muda wake kutafuta chakula katika maeneo yenye matope na mchanga karibu na miamba ya matumbawe

Sio matamko yote ya kutoweka hubaki kama yalivyo. Constance anataja kisa cha samaki (smooth handfish), kutoka kwenye maji ya pwani ya Tasmania, Australia.

Alikuwa samaki wa kwanza kutangazwa kutoweka, mwaka 2018. Hata hivyo, ripoti ya mwaka 2021 iliamua kuwa taarifa zilizotumika kuunga mkono tamko hili hazitoshi. IUCN baadaye iliorodhesha hali ya samaki huyo kuwa "haijulikani."

“Tunapaswa kuwa na taarifa za kutosha kuhitimisha kwamba samaki fulani wametoweka,” anasema Riley Pollom, meneja wa mpango wa uhifadhi wa samaki.

“Kwa sababu wanapotajwa kuwa wametoweka, juhudi zote za uhifadhi hukoma na wanaweza kutoweka kwa sababu ya tangazo hilo.”

“Ingawa wanasayansi wanaweza kuwa na uhakika juu ya kutoweka kwa stingaree Java,” anasema Pollom, “ukubwa wa bahari ya dunia unamaanisha wataalamu wanaweza kuwa wamekosa. Kimsingi, kunaweza kuwa na mengi yanayotokea nyuma yetu bila sisi kujua."

Utafutaji wa Constance wa stingaree Java haujakamilika. Msimu huu wa kiangazi hatimaye aliweza kusafiri hadi Jakarta mwenyewe kuangalia shughuli katika maeneo mawili makuu ya kuuza samaki, kwani hakuweza kufanya hivyo hapo awali wakati wa utafiti wake, kwa sababu ya vizuizi vya Covid-19.

Yeye na wenzake walitafuta katika marundo ya samaki waliovuliwa ili kumuona samaki huyo. Lakini, licha ya uzito wa tamko lake na mwenzake mwaka 2023, hatofadhaika au kukata tamaa ikiwa kutoweka huko litakuwa ni tangazo lenye makosa.

"Tunataka samaki hawa waendelee kuishi katika siku zijazo," Constance anasema. "Itakuwa jambo zuri sana ikiwa mtu atampata siku moja."

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah